NA CATHERINE SUNGURA, WIZARA
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametembelea kituo cha Afya
cha Gairo na kukabidhi mabati 100 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF).
Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo hicho.
Hii ni
kufuatia ahadi yake aliyoitoa Julai, mwaka huu alipofanya ziara ya
kikazi wilayani Gairo kukagua utoaji wa huduma za Afya.
Akikabidhi mabati hayo jana Waziri Ummy alisema kipaumbele chake
cha kwanza ni afya ya mama na mtoto" hivyo atahakikisha huduma kwa mama
wajawazito na watoto zinaimarika katika vituo vya kutolea huduma za afya
vya umma kote nchini.
Hivyo aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Gairo
kusimamia vyema utoaji wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kwani kufanya
hivyo kutatatua takribani asilimia 70 ya changamoto za afya nchini.
Aliiagiza halmashauri itumie vyanzo vyake vya mapato vya ndani
kununua baadhi ya vifaa tiba kama x - ray na ultra - sound ili kuboresha
huduma za uchunguzi wa wagonjwa.
Waziri Ummy pia aliuelekeza uongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Gairo kuhakikisha inaunda kamati za afya za vituo na
wahakikishe zinatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo matumizi mazuri
ya dawa.
"Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Dr John Pombe Magufuli imetoa kipaumbele kwa sekta ya afya hususani
upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya," alisema.
Akitoa mfano wa Halmashauri
ya Wilaya ya Gairo alisema, mwaka wa fedha wa 2015/16 walitengewa kiasi
cha shilingi milioni 89 lakini mwaka huu wa fedha wa 2016/17 bajeti ya
dawa imeongezeka hadi kufikia milioni 198 na hadi sasa wameshapatiwa
shilingi milioni 115.
Aliwataka viongozi wa Halmashauri hiyo kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo ili tuweze kuwa na dawa
za kutosha katika vituo vya afya.
Aliwataka pia viongozi hao wasimamie na wahamasishe
wananchi wajiunge na mfuko wa afya ya Jamii - CHF, ambapo kimsingi bima
hii inawasaidia sana wananchi kupata huduma za afya pindi wanapohitaji
kupata huduma za matibabu hususani wanapokuwa hawana fedha taslimu.
"Wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu kutokana
ukweli kwamba gharama za matibabu zinaongezeka kila siku. Hakikisheni pia mnawatambua wazee wote wasiojiweza na kuwapatia
vitambulisho ili viwasaidie wakati wanapohitaji kupata huduma ikiwemo
huduma za afya," aliwahimiza.
Hata hivyo, alipongeza ubunifu uliofanywa na uongozi wa
mkoa wa Morogoro kwa kuanzisha mfumo ujulikanao kama JAZIA, utaratibu
huo unatumika kuhakikisha dawa zote zinakosekana kupitia Bohari ya Dawa,
zinanunuliwa kupitia vyanzo vingine vya mapato ili kuhakikisha zote
muhimu zinapatikana kwenye vituo vya matibabu.
Chapisha Maoni