Vijana wakijidunga dawa za kulevya
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KUNA wimbi la wasanii nchini kutumbukia katika matumizi ya
dawa za kulevya za aina mbalimbali na upo mjadala kwanini wamekumbwa na ‘pepo’
hilo.
Wengi wanahoji sababu zinazowafanya wasanii kuingia katika
mkumbo huo licha ya kuwa wana uwezo wa kutumia vipaji vyao kujipatia fedha
halali.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili,Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Dk. Cassian Nyandindi ametaja sababu kuu inayochangia kundi
hilo kuingia katika janga hilo.
Akizungumza na matukionamaisha hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, Dk. Nyandindi alisema wengi hufanya hivyo kwa kigezo cha kuondoa aibu
usoni eti wakati wanapokuwa wakitumbuiza jukwaani.
“Kuna sababu nyingi zinazochangia mtu kutumbukia katika
matumizi haya, wapo ambao hupata vishawishi toka kwa ndugu, marafiki zao wa
karibu, kuna ambao hutumbukia kutokana na kupata matatizo ya kisaikolojia, wengine
hutumia ili kukidhi haja zao na malezi mabovu.
“Lakini kwa hawa wenzetu wasanii wengi wanadhani kwamba anapotumia dawa za kulevya uwasaidia
kuondoa aibu ili waweze kufanya vema pindi wanapopanda jukwaani,” alisema.
Daktari huyo alisema awali mtumiaji huona kuna manufaa
pasipo kujua kuna hatari kubwa mbele yake.
“Wapo ambao hujikuta wakitumia dawa kupita kiasi jambo
ambalo hufanya wapoteze fahamu au hata kupoteza maisha,” alisema.
Aliongeza “Mtu aliyezidisha kiwango cha dawa utaona analala
sana, anasinzia kila mara, anakoroma, mapigo yake ya moyo yanakuwa chini kuliko
kawaida, uwezo wake wa kupumua (breathing rate) unashuka chini, kwa kawaida
huwa dakika 16 hadi 20 lakini hawa hufikia hadi dakika chini ya 12, ni hatari,
pia muda mwingi huonekana wakiwa wamening’iniza kichwa chini (head bending),”
alisema.
Alisema watu wanaotumia dawa za kulevya huanza kuonesha
dalili ambazo kitaalamu zinaitwa ‘with draw features’ wenyewe (watumiaji) wanaita
alosto.
Dawa za kulevya zilizowahi kukamatwa na Jeshi la Polisi Tanzania
“Hasa pale anapokosa dawa anapata maumivu ya mwili
yaliyopitiliza, maumivu ya tumbo, kuharisha, kutetemeka, kutokwa na jasho
jingi, kamasi, machozi na kukosa usingizi ni miongoni mwa athari zinazowapata watumiaji
wa dawa za kulevya,” alisema.
Alisema kiujumla matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri
mfumo wa ubongo.
“Hadi sasa kuna takribani watu 3,500 ambao ni waathirika wa
dawa za kulevya wanaopatiwa huduma ya methadone katika vituo vinne vilivyofunguliwa
nchini.
“Kituo cha Muhimbili kilikuwa cha kwanza kufunguliwa mwaka Februari
2011, Novemba 2012 kikafunguliwa cha Mwananyamala, Machi 2014 Temeke na Zanzibar
2015,” alisema.
Daktari huyo alisema kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2014 ya Tume
ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (NACP) inakadiriwa kuwa watu 550,000
nchini wanatumia dawa ya kulevya ya heroin.
“Kati ya watumiaji hao, 50,000 hujidunga sindano na kati ya
idadi hiyo asilimia 50 wanaishi katika jiji la Dar es Salaam, katika jiji hilo Wilaya
ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi wa dawa za kulevya,”
alisema.
Dk. Nyandindi alisema ripoti hiyo inaeleza mikoa mingine
iliyo na idadi kubwa ya waathirika wa dawa za kulevya ni Arusha, Tanga,
Kilimanjaro, Dodoma, Mbeya, Pwani, Mwanza na Morogoro.
Alisema kwa kuwa wengi hujidunga sindano inachochea kuongezeka
kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.
“Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya (NACP), kiwango cha
maambukizi ya VVU kwa kundi hili ni asilimia 20 hadi 50 wakati kwa kundi la
jumla (general population) ni asilimia 5.1 hii ni kwa sababu wakishajidunga
sindano hushindwa kufanya maamuzi sahihi na kujikuta wakifanya ngono zembe,”
alisema.
Aliongeza “Matumizi ya dawa za kulevya uchochea pia mtu
kupata homa ya ini (Hepatit B na C) na kwamba kiwango cha maambukizi ya kifua
kikuu ni kikubwa kwa kundi hilo.
“Lakini siku hizi kwa kuwa uingizwaji wa dawa umezibitiwa
wapo ambao wanaona watumie njia mbadala ya kupunguza alosto kwa kunywa ama
pombe kali au dawa za usingizi jambo ambalo linaongeza tatizo,” alisema.
Chapisha Maoni