*Unachopaswa kuzingatia ni usafi pekee
*Zinatarajiwa kuzinduliwa Machi, mwaka huu nchini
NA
VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MWILI wa binadamu hupitia mabadiliko mbalimbali katika
ukuaji wake, kipindi hicho cha mabadiliko ya mwili huitwa balehe, uhusisha
mabadiliko yote ya kimwili, kimawazo na kihisia.
Mabadiliko hayo huwapata jinsi zote mbili, ya kike na kiume
pale wanapotoka utotoni kuingia utu uzima. Ni katika kipindi cha mabadiliko ya
mwili ambapo msichana huanza kupata damu ya hedhi.
Hatua hiyo muhimu uitwa kupevuka(kuvunja ungo), hedhi ni kipindi
maalumu katika maisha ya mwanamke aliyefikia umri wa kuzaa.
Kwa kawaida mzunguko wa hedhi hutokea kila mwezi na kila
mwanamke anao mzunguko wake ni hapo ambapo mwili hujiandaa kwa hali ya kupata
ujauzito.
Hedhi
hutokeaje
Zipo ovari mbili (vifuko vya mayai) katika mwili wa mwanamke,
moja upande wa kushoto na nyingine kulia ambazo hutengeneza mayai ya uzazi ambayo
husafirishwa hadi katika mji wa mimba kupitia mirija ya uzazi.
Kila mwezi ovari moja huachilia yai mchakato ambao huitwa
kitaalamu ovulation na wakati huo mabadiliko ya homoni huuandaa mji wa mimba (uterusi)
kutengeneza ukuta mpya uitwao endometrium kwa ajili ya kujiweka tayari kwa
mapokezi ya mimba inayoweza kutungwa.
Yai linalofika katika uterasi iwapo halitarutubishwa na
mbegu ya mwanamume, ukuta huo humeguka na kutoka nje ya mji wa mimba kupitia
ukeni ukiwa pamoja na damu.
Kitendo hicho ndicho huitwa hedhi (menstruation) au
mzunguko wa hedhi (menstruation cycle).
Inaelezwa kwamba wasichana wengi huanza kupata hedhi yao ya
kwanza wakiwa na miaka tisa na kuendelea na mara nyingi mwanamke hukoma hedhi
anapotimiza umri wa miaka 45 hadi 50.
Ingawa ni kipindi muhimu katika maisha ya mwanamke lakini
huwa kina changamoto ambazo hukumbana nazo na hutofautina kati ya mwanamke
mmoja na mwingine.
Wapo ambao hupata hedhi kwa siku tatu na wengine huenda hadi
saba na miongoni mwao wapo pia ambao hupata hedhi nyepesi na wengine nzito.
Wapo pia ambao hupata hedhi pasipo kukabiliana na matatizo
yoyote lakini wengine hupata hedhi kwa uchungu na masumbufu mengi, kama kuumwa tumbo,
mgongo, kichwa, kiuno na mengineyo.
Mwanamke anashauriwa kujiweka safi mwili wake wakati wote
hasa akiwa katika kipindi hicho cha kipekee.
Kwa kipindi kirefu wanawake wengi wamekuwa wakitumia njia
ya asili hasa mabibi zetu wakitumia vipande vya kanga, vitambaa au vitenge
vilivyokatwa kwa ustadi kujihifadhi wakati wa hedhi.
Lakini kukua kwa teknolojia kukapelekea kutengenezwa taulo
za kisasa za kutumia na kutupa ambazo huuzwa kwa bei tofauti tofauti madukani.
Hali
ilivyo nchini
Nchini Tanzania suala la hedhi salama hasa kwa wasichana
hasa waliopo shuleni linatajwa kuwa bado ni kitendawili na changamoto kwa walio
wengi hususan vijijini.
Inaelezwa kuwa wasichana wengi wanapokuwa katika kipindi
cha hedhi hushindwa kuhudhuria masomo yao ipasavyo kwa zaidi ya siku tatu hadi
tano kwa mwezi hiyo.
Hali hiyo inasababishwa na hofu ambayo huwakumba wakiwa
katika kipindi hicho, ya kuchafua sare za shule na kuhofia kuchekwa na kutaniwa
na wanafunzi wenzao hasa wa kiume walio chini kiumri.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa ikiwemo ile ya
haki elimu ya mwaka 2013, kutohudhuria kwao masomo huchangia kuzorotesha kwa
kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi husika.
Abuni taulo
za kufua
Hali hiyo ndiyo iliyomchochea mjasiriamali Jenipher Shigoli
kufanya utafiti akiwa na nia ya kuja na mbinu itakayowasaidia wasichana kutohofia
na kuhudhuria masomo yao pasipo kujali kipindi cha hedhi.
“Kitaaluma ni mwanasheria pia ni mwanadiplomasia lakini
napenda mno ujasiriamali, nimekuwa nikijihusisha na utengenezaji wa bidhaa za
usafi tangu mwaka 2013, kupitia biashara hiyo nimeweza kupata tenda za
kusafisha vyoo vya shule mbalimbali nchini kupitia kampeni ya choo salama
inayoendeshwa na kampuni ya Malikia ambayo mimi ni Mkurugenzi wake,” anasema.
Anasema kupitia kampeni yake hiyo ameweza kufika katika
shule nyingi za mkoa wa Dar es Salaam, Dodoma na Iringa.
“Nikiwa katika shughuli hizo za kampeni ya choo salama
ndipo nikagundua kwamba wasichana wengi hasa kwa shule za kule vijijini
hushindwa kuhudhuria masomo wakiwa katika kipindi cha hedhi kwa hofu ya
kuchafuka na kuchekwa,” anasema.
Nini
kilimsukuma kubuni taulo hizo
Shigoli anasema alipata nafasi ya kuwahoji baadhi ya
wanafunzi ambao walimueleza kuwa ili kujihifadhi hutumia manyoya ya kuku, udongo,
magunzi ya mahindi, ugali au soksi.
“Wapo ambao walinieleza huwa wanatumia vitambaa vya kanga
au vitenge lakini wataalamu wa afya wanasema si salama kwa afya kwani rangi
inayotumika kutengeneza bidhaa hizo kwa kawaida huchuja zinapokuwa zimelowa
majimaji.
“Walimu nao walinieleza kuwa wapo wanafunzi wengi ambao
huacha masomo na kuamua kukaa nyumbani kwa sababu ya hedhi, kwani hata wale
wanaovaa vitambaa huwa hawapo ‘comfortable’ na hali ambayo huwaathiri kisaikolojia,”
anasema.
Anasema ni kutokana na adha hizo wanazokabiliana nazo
wasichana hasa wa huko vijijini ndizo zilizonifanya nikae chini na kutafuta
jinsi ya kuwasaidia.
“Kwa kuwa wengi wanashindwa kumudu gharama za kununua taulo
za kutumia na kutupa nilipata wazo la kutengeneza taulo za kutumia zaidi ya
mara moja,” anasema.
Alifanikishaje
wazo lake
Anasema baada ya kupata wazo hilo aliwashirikisha watu
mbalimbali wakiwamo wataalamu wa maabara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Shirika la kuhudumia viwanda vidogo
(SIDO) ambao walimsaidia.
“Walinishauri na tulichukua muda wa miezi sita hadi
kukamilisha bidhaa hizo,” anasema.
Malighafi
ni pamba halisi
Shigoli anasema taulo hizo zimetengezwa kwa ustadi wa hali
ya juu na kwa kutumia pamba halisi, kitambaa na nailoni maalumu ambayo huweza
kupokea damu ya hedhi hadi kiwango cha mililita 30 hadi 40.
“Uwezo huo unalingana na ule wa taulo zingine zinazouzwa
huko madukani, na huweza kuvaliwa kati ya saa sita hadi saba. Baada ya saa hizo
unalazimika kuifua na kuianika ikauke vizuri kwa ajili ya kuitumia tena na
hudumu hadi mwaka mmoja,” anasema.
Atunukiwa
tuzo
Anasema kupitia bidhaa yake hiyo aliweza kuibuka mshindi
katika shindano la kusaka wabunifu barani Afrika mwaka jana linalosimamiwa na
taasisi ya ‘African Entrepreneur Award’.
“Niliibuka mshindi wa kwanza na nilizawadiwa kiasi cha Dola
150,000 sawa na Shilingi milioni 300 za Kitanzania,” anasema.
Serikali
yampa eneo la kiwanda, mtaji
Jenipher anasema anaishukuru serikali kupitia Wizara ya
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu kwani imenipatia mtaji wa Sh
milioni 30 ili kukuza biashara yake hiyo.
“Kupitia Wizara hiyo nimepewa eneo la kutosha kujenga
kiwanda huko Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hizi tunatarajia
kukizindua ifikapo Machi, mwaka huu,” anasema.
Anasema tayari pia ameshapeleka barua Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwamba anatarajia atapata
ushirikiano wa kutosha aisaidie jamii yake.
Jenipher anawasihi watanzania hasa wanawake kutokuwa na
wasiwasi juu ya taulo hizo alizobuni.
“Nimepitia taratibu zote kisheria, zimepimwa na Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) na zimeonekana zina ubora, nimeenda pia Mamlaka ya
Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) nimepewa ‘certificate’ na kama nilivyoeleza
awali kuna wataalamu ambao nashirikiana nao kutoka UDSM na SIDO,” anasema.
Mbegu za uzazi za mwanaume zikikimbilia kwenye yai kutengeneza mtoto
Simulizi
ya Monica
Monica Elius (si jina lake halisi) anasema ni zaidi ya
mwaka mmoja sasa tangu aanza kutumia taulo hizo za kufua na kwamba amebaini
tofauti kubwa ikilinganishwa na zile za kutumia na kutupa.
“Sikujua kama kuna mbunifu Mtanzania ambaye ameanza
kuzitengeneza pia taulo za aina hii nchini, maana nilianza kuzitumia muda mrefu
sasa umepita na nilikuwa najua kwamba zinatoka nje na kuletwa kama msaada.
“Nina dada yangu ambaye mume wake alikuwa akifanya kazi
katika kambi ya wakimbizi iliyopo Ngara mkoani Kigoma, wanawake na wasichana
waliokuwa wakiishi katika kambi hiyo walikuwa wakigawiwa na mashirika ya
misaada,” anasema.
Alianzaje
kuzitumia
“Awali nilikuwa natumia taulo za kawaida zinazouzwa
madukani, lakini kila nilipotumia nilikuwa napata muwasho mkali mno, hali yangu
ilikuwa mbaya,” anasema.
Anasema alikuwa analazimika kwenda hospitalini kupima na
kupewa matibabu kila mara ingawa haikugundulika tatizo lilikuwa nini hadi
anapatwa na hali ya namna hiyo.
“Nakumbuka kuna wakati nilikuwa mkoani Morogoro nilitokewa
na hali hiyo nikaenda katika dispensary moja na kumuelezea daktari niliyemkuta,
alinipima na kugundua kuwa nina mzio na hizi taulo za kawaida.
“Hivyo alinishauri ninunue kanga mpya nikate vipande vya
kunitosha au ninunue gozi (kitambaa
maalumu ambacho hutumika kufunga vidonda)
pamoja na pamba ili nijitengenezee taulo zangu mwenyewe,” anasema.
Wasichana wengi hupata maumivu ya tumbo wakiwa katika siku za hedhi
Gozi
ni gharama kubwa
Anaongeza “Hata hivyo nilishindwa kumudu hilo kwani nilikuwa
natumia fedha nyingi kununua gozi peke yake ni kati ya shilingi 25,000 hadi
30,000 na pamba ni kati ya shilingi 25,000 hadi 30,000 kwa hiyo nilihitaji kati
ya shilingi 60,000 hadi 70,000 niweze kupata bidhaa hizo ili nitengeneze taulo
za kutumia miezi mitatu hadi minne, ni gharama kubwa mno.
Anasema siku moja akiwa na dada yake huyo alimshangaa kuona
anahangaika kutengeneza vitambaa vya kujihifadhi jambo ambalo lilimlazimu
kumsimulia sababu za kufanya hivyo.
“Alinishangaa, ikabidi nimsimulie ndipo akaniambia atanipatia
hizo taulo za kufua, sikuamini kama zipo hadi siku aliponiletea,” anasema.
Anasema taulo hizo huuzwa kati ya Sh. 5,000 hadi 8,000 na
kwamba tangu ameanza kuzitumia ameondokana na ile hadha ya kupatwa muwasho
katika sehemu zake za siri.
“Unaona kama hii niliyobeba (akimuonesha mwandishi wa
makala haya) ina mwaka sasa lakini bado naitumia, haijachoka kama unavyoiona,”
anasema.
Uzoefu
wake
Monica anasema taulo hizo zimetengezwa na malighafi ya
pamba pekee na kitambaa maalumu hali ambayo inaifanya kuwa laini na murua
wakati wote anapokuwa ameivaa.
“Yaani ni laini kiasi kwamba unajisikia raha ukiwa umeivaa hakuna
michubuko wala huwezi kujihisi harufu mbaya unapokuwa umeitumia, hata ukipata
muwasho si kama ule unaotokea ukiwa umevaa taulo zile za kutumia na kutupa,”
anasema.
Anasema hiyo ni kwa sababu taulo hizo hazijatengenezwa na
kemikali yoyote zaidi ya pamba na kitambaa hicho maalumu.
Anaongeza “Kwa kawaida huwa zinakaa taulo nne katika pakiti
moja, mbili huwa ni nzito kwa ajili ya kutumia katika kipindi ambacho damu ya
hedhi huwa nyingi na nyingine mbili ni nyepesi kwa ajili ya kutumia katika
kipindi wakati hedhi ikiwa si nyingi.
Zinafuliwaje?
Anasema suala la usafi wa taulo hiyo ni wa muhimu
kuuzingatia ili mtumiaji asipate matatizo mbalimbali ya kiafya kama vile
muwasho na hata harufu mbaya.
“Huwa nafualia sabuni ya unga, naona ndiyo inafaa zaidi
kuliko zingine. Hii unapaswa kuifua na kuisuuza vizuri kwa maji mengi, ukisuuza
na maji kidogo ikikauka unaikuta ina alama za mistari zimekatisha katikati,”
anasema.
Anaongeza “Alama hizo hufanya muonekano wake kuwa wa
kuudhi, uzuri ni kwamba unapoifua na kuianika kukiwa na jua kali haichukui
zaidi ya saa mbili unaikuta tayari imekauka na unaweza kuivaa tena.
Anaongeza “Nampongeza huyo mbunifu Mtanzania kwa kuliona na
kulifanyia kazi wazo hilo, ni taulo nzuri hata ukiwa safarini, wanawake tukiwa
safarini na kupatwa na hali hiyo kama sehemu uliyopo hakuna maji huwa ni shida
kubwa.
“Lakini ukiwa safarini na ukawa umetumia taulo hii ni
tofauti na zile za kutupa, ukijisafisha hubaki na harufu, unahifadhi vizuri
taulo yako na kwenda kuisafisha nyumbani pindi unapofika,” anasema.
Anasema taulo hizo zinasaidia kupunguza gharama kwani mtu
anaponunua huweza kukaa nazo hadi mwaka mzima.
“Naona ni mkombozi hasa kwa wenzetu walioko vijijini ambako
tunajua ni kazi mtu kupata shilingi 2,000 au 3,000 ya kununua pakiti ya taulo za
kawaida.
“Akinunua hii kwa shilingi 5,000 au 8,000 anakuwa na kazi
ya kuzingatia ufuaji safi na anazitumia mwaka mzima, lakini kupanga ni kuchagua,
kila mmoja ana maamuzi yake, binafsi nazipenda, ninapoivaa najisikia huru na
mchangamfu wakati wote nikiwa kwenye siku zangu,” anasema.
Daktari
Daktari Bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), (jina linahifadhiwa kwa sasa anasema kipindi cha hedhi
ni muhimu kwa afya ya mwanamke.
“Mwanamke anapokuwa katika siku zake hulazimika kutumia
taulo hizo ambazo kazi yake kuu ni kupokea ile damu inayotoka, kama hatavaa
maana yake ni kwamba itapitiliza kuchagua nguo zake.
“Taulo za kutumia na kutupa jinsi zilivyotengenezwa zina
‘layer’ maalumu kwa ndani ambayo hufyonza damu ya hedhi, hulazimu kubadili mara
nyingi (kiasi cha kila baada ya saa nne) hasa inapokuwa inatoka kwa wingi,”
anasema.
Kaimu
Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Egid Mubofu anasema ni kweli
shirika hilo lilipokea maombi ya kupima taulo hizo za Elea hata hivyo bidhaa
hiyo bado haijaruhusiwa kuingizwa sokoni.
“TBS
tulipokea maombi kutoka kampuni ya Malkia ambao ni wazalishaji wa bidhaa za
Elea. Upimaji wa awali wa bidhaa hiyo ulifanyika na matokeo yalionesha kuwa
bidhaa hiyo haikidhi kiwango cha bidhaa husika ambacho ni TZS 1659:2014, hivyo
mzalishaji akatakiwa kufanyia marekebisho bidhaa hiyo,” anasema.
Mubofu
anasema mpaka sasa mzalishaji wa
bidhaa hiyo hajafanyia marekebisho bidhaa hiyo, hivyoTBS bado haijathibitisha
ubora wa bidhaa hiyo.
“Bidhaa za pedi ziko katika orodha ya bidhaa za
lazima, hii ni kutokana na madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza endapo
bidhaa hizo hazitakidhi matakwa ya kiwango husika. Hivyo basi bidhaa za aina
hii hazipaswi kuingizwa sokoni mpaka hapo ubora wake utakapothibishwa,”
anasisitiza.
Kauli ya Shigoli
Mbunifu wa taulo hizo, Shigoli anasema bidhaa
yake hiyo bado hajaiingiza sokoni kuanza kuwauzia wateja.
Anasema kwa sababu anaboresha eneo lake la kiwanda kama ambavyo ametakiwa na Shirika la Viwango Tanzania
(TBS)
“Bado
sijaingiza sokoni bidhaa ya Elea, kwa sababu TBS wamenitaka nihakikishe
naboresha kwanza eneo langu la kiwanda, hivi sasa najenga kiwanda huko Kibaha
mkoani Pwani ambapo eneo nimepewa na serikali,” anasema.
Anasema
baada ya kukamilisha kiwanda chake hicho maofisa wa TBS watakwenda tena
kumkagua kujiridhisha kabla ya kumpa kibali cha kuweka nembo ya ubora katika
bidhaa yake hiyo.
“Natarajia
ujenzi wa kiwanda utakamilika ifikapo Machi, mwaka huu na tutazindua bidhaa
yetu rasmi, nitakapopewa ruhusa ya kuweka nembo ya ubora na itaanza kupatikana
sokoni,” anasema.
“Sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kuangalia zile pedi ambazo vijana wanaweza kutumia mwenzi mmoja, miwili hata mwaka mzima, hata kwa miaka miwili. tunaendelea kuangalia tafiti mbalimbali kuhusu usalama wa hizi pedi ambazo zinaweza kuzitumia kwa muda mrefu,” alisema.
Aliongeza, “Kwa hiyo tunaangalia kama na sisi tunaweza kuziruhusu kuingia nchini na sisi tuziingize sokoni. Lengo letu ni kuangalia usalama kwanza kabla hatujaziruhusu kutumika.
Alisema
serikali inahimiza wazazi na walezi wa watoto wa kike wanapoona mabadiliko
yametokea kwa mabinti zao wawafundishe namna ya kujitunza kwa kutumia vifaa
ambavyo vipo na vinapatikana kwa urahisi sambamba na kuwapa elimu zaidi ili
wawe wasafi na kujiepusha na magonjwa yakuambukizwa.
Chapisha Maoni