NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
VIJANA wengi nchini bado hawawezi kuandika wasifu wao wanapofikia hatua ya kutafuta ajira na hivyo
kujikuta wakiisha kunakili wasifu wa watu wengine hasa zilizowekwa mtandaoni hatua
ambayo imeelezwa kuwa haifai.
Aidha, vijana ambao huhitaji kujiajiri nao hushindwa kutengeneza
wazo zuri, kulifanya liwe bora na jinsi gani wanaweza kutumia fursa za kibenki
zilizopo kupata mikopo kuendelea mawazo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha
Tanzania (FSDT), Sostenes Kewe alisema hayo jana alipozungumza kwenye uzinduzi
wa mpango wa mafunzo ya ujasiriamali na ajira kwa vijana kwa njia ya mtandao
uitwao Noa Ubongo.
“Vijana wana ndoto za kupata maendeleo lakini wengi
hujikuta ndoto zao hazitimii kutokana na sababu mbalimbali, kwa mfano wale
wanaotaka kutafuta ajira tumegundua hawajui kuandika wasifu wao matokeo yake
wananakili za watu wengine na kukosa kazi.
“Wanaotaka kujiajiri nao hawajui kutengeneza na kuliboresha
wazo la biashara, sasa kupitia mpango huu wa Noa Ubongo watapata elimu hii
kupitia njia ya mtandao,” alisema.
Kewe alisema utafiti kuhusu Elimu ya Mambo ya Fedha wa
mwaka 2014 unaonesha asilimia 58 ya watanzania hawajibidiishi katika kutafuta taarifa
mbalimbali kwa kujisukuma wenyewe.
Alisema utafiti huo unaonesha pia asilimia 68 hawana ule
uthubutu wa kutafuta elimu ya mambo ya fedha na hivyo kushindwa kuchangamkia
fursa nyingi zilizopo huko.
“Kwa hiyo huu ni wakati mwafaka kwa vijana na watanzania
kwa ujumla kufuatilia vipindi vya Noa Ubongo ili waweze kupata elimu ya
kibiashara ambayo itawasaidia kutoka kimaisha,” alisema.
Naye Nisha Sanghvi wa Khanga
Rue Media, alisema wameamua kutumia njia ya mtandao kwani ni rahisi kuwapata
vijana wengi kuwafikishia ujumbe huo walionao.
“Noa Ubongo ni chaneliya kwa
ajili ya vijana ambayo inawafundisha ujuzi utakaowasaidia kuongeza uwezo wao,
kubadili mtazamo wao na itakayowasaidia kuboresh kifedha maisha yao ya baadae,”
alisema.
Chapisha Maoni