Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MATUKIO ya watu kujiua yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini, ni matukio yanayoshtua na kuogopesha mno pindi tunapoyasikia.

Kwa sababu si jambo rahisi hata kidogo mtu kuamua na kutekeleza hatua ya kuukatisha uhai wake (kujiua) mwenyewe mara nyingi jamii huwa inabaki ikijiuliza maswali mengi.

Kwa mfano unakuta watu wakijiuliza imekuwaje hadi marehemu ameamua kuchukua uamuzi huo ambao wengi huwa tunautafsiri kuwa ni mgumu.

Maswali hayo ndiyo yaliyoyotusukuma kufanya mahojiano na Msaikolojia Tiba wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Isack Lema.

Akizungumza anasema hali hiyo huweza kujitokeza iwapo mtu anakuwa ameugua ugonjwa uitwao kitaalamu sonona (depression) na akakosa mtu wa kumpa msaada unaostahili.

“Sonona ni miongoni mwa magonjwa ya akili, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) watu wengi wanapitia hali ya huu ugonjwa lakini si wote ambao wanatambua na kutafuta tiba sahihi kwa sababu hawajui,” alisema.

Anafafanua kwamba sonona ni ugonjwa wa akili ambao upo katika kundi la magonjwa ya hisia.
“Ni ugonjwa ambao hutokana na masuala mbalimbali ambayo tunayapitia kila siku ndani ya jamii,” anasema Lema (pichani) ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa na Afya ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Magonjwa mengi ya akili huanza kutoka kwenye vitu ambavyo ni vya kawaida kwenda kwenye vile vitu ambavyo si vya kawaida,kwa mfano ugonjwa wa sonona huathiri utendaji kazi wa akili ya mtu, hisia za mgonjwa husika, mwitikio wa mwili na tabia yake kwa ujumla,” anasema.

Dk. Lema anasema sonona ni ugonjwa ambao mara nyingi mtu anayeugua huishia kuumia lakini jamii inayomzunguka inaweza isielewe nini kinachoendelea katika maisha ya muhusika.

“Wakati mwingine hata mgonjwa mwenyewe anaweza asielewe jitu kinachoendelea katika maisha yake hivyo anakuwa akiumia mwenyewe moyoni mwake,” anasema.
Dalili

Anasema zimegawanyika katika makundi mbalimbali, ikiwamo dalili za kiakili, kimwili, kihisia, kitabia.

“Tunapozungumzia akili tunamaanisha ni jinsi gani mtu anavyoweza kuzifanyia kazi zile taarifa anazozipata kila siku na jinsi gani anavyoweza kufikiria, kumbukumbu zake na jinsi anavyoweza kuchukua maamuzi.

“Sasa mtu anayeugua sonona, katika akili yake huwa ni mtu anayewaza mawazo hasi, huwa si mtu wa kuwaza mawazo chanya na anawaza hasi kutokana na yeye mwenye, mazingira aliyonayo na jinsi anavyoyatazama mazingira yajayo,” anasema.
Anatoa mfano “Unakuta mtu mwenye sonona anawaza kwamba hana thamani au maisha si kitu, hayana maana yoyote au duniani si mahala pazuri pa kuishi,” anasema.

Anasema mtu anayeugua sonona hata akikutana na jambo ambalo ni chanya katika maisha yake mara nyingi huona limetokea tu kwa bahati mbaya.

“Anaweza kuwaza hivyo akichukulia kwamba limetokea kwa sababu watu hawampendi au kwa sababu maisha yake hayana maana yoyote ndiyo maana linapotokea jambo zuri yeye hachukulii kwamba ni jambo ‘positive’ kwa upande wake,” anasema.

Dk. Lema anasema watu wanaougua sonona huwa wanapoteza kumbukumbu hata kwa jambo amezungumza na mwenzake muda mfupi uliopita.

“Hii ni dalili nyingine, mara nyingi huwa wasahaulifu, umakini wao katika vitu wanavyovifanya nao huwa unapungua  au unapotea kabisa, kwa mfano ikiwa ni mwanafunzi ambaye alikuwa anauwezo wa kusoma ukurasa mmoja kwa dakika tano pekee kama anaugua sonona unakuta hawezi tena kusoma kwa dakika hizo labda ukurasa mmoja atausoma kwa dakika kuanzia 20 na kuendelea,” anasema.

Anaongeza “Ikiwa ni mfanyakazi unaweza kukuta alikuwa na uwezo wa kufanya kazi zake kila siku kama kawaida lakini, akipata tatizo hili utakuta anashindwa kufanya zile kazi zake kama ilivyokuwa awali.

“Au unakuta anatumia muda mrefu kufanya kitu kile kile ambacho alikuwa na uwezo wa kutumia muda mfupi kabla hajaugua,” anasema. https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjNefDke5JUcldVrS1pggFrAaMntu5i6_Pwl48TDn9mopY1TiARxUZHzOiReSnZ7EK3mB9kldUZcKXeyuDE_WNHWyiCfp6Zq4pQEhAaEl6T-DU7jFxHMRYca2b8alA99vU5u9l3BQZGz45x/s1600/KAMBA.jpg
Anasema kwa sababu mtu anakuwa ametawaliwa na mawazo hasi akilini mwake hufikia hatua ya kuona maisha hayana thamani kwake na hivyo kuanza kupata mawazo ya kutaka kujidhuru.

“Ndipo hapo utakuta mtu anafikia uamuzi wa kujaribu kujiua na hadi inafikia hatua hiyo unaweza kukuta wale waliomzunguka wanakuwa bado hawajajua nini kinachoendelea, hizi zote ni dalili za kiakili,” anasema.

Anasema kwa kuwa sonona ni ugonjwa wa kihisia, hivyo mgonjwa huanza kupata dalili za awali za kihisia.

“Mara nyingi mtu mwenye sonona huwa na huzuni sana, wakati mwingine huwa ni mtu wa hatia, kwa mfano anaweza akazungumzia jambo ambalo limetokea na akajilaumu kwa jambo hilo utadhani ni yeye amelitenda kumbe hajatenda,” anasema.

Anasema wengine huwa ni watu wenye jazba, kiasi kwamba wanapoulizwa jambo dogo hughafirika lakini baada ya muda hujikuta wakiomba msamaha.

“Huwa wakati mwingine unakuta anarudi kuomba msamaha kwamba hakukusudia lakini baada ya muda ile hali inamtokea tena na anakuwa haelewi kwanini inamtokea tena,” anasema.

Dalili za kimwili

Anasema mtu mwenye sonona anakuwa anakosa usingizi au kupata ‘usumbufu wa usingizi’.

“Hali ya usumbufu wa usingizi imegawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza ni yule mtu ambaye  anaenda kitandani lakini akijaribu kulala anakosa usingizi, anajikuta anakaa muda mrefu kabla ya kupata usingizi,” anasema.

Anafafanua kundi la pili ni yule mtu ambaye akienda kulala hupata usingizi lakini akishtuka usiku wa manane anakaa muda mrefu bila kupata tena usingizi.
 
“Kwa sababu anakosa usingizi, unakuta anakaa muda mwingi akiwaza mambo mengi yanayomtokea katika maisha yake anakuwa hawezi kulala tena,” anasema.

Anataja kundi la tatu ni yule mtu ambaye hupata usingizi kwa muda mrefu kuliko kawaida yake.

“Yaani kwa mfano alizoea kulala saa tatu usiku na kuamka saa 12 alfajiri lakini ghafla anajikuta anashindwa kuamka katika muda ule aliozoea pengine anapitiliza hata hadi saa tatu na kuendelea,” anasema.

Kukosa hamu ya kula chakula

Daktari huyo anasema hii nayo ni dalili nyingine ambayo mtu anayeugua sonona huipata.

“Wapo ambao hujikuta hamu ya kula inapungua, kwa kuwa wanakula kiwango kidogo cha chakula matokeo yake uzito wa mwili wake hupungua, ingawa wapo wengine pia ambao hujikuta hamu ya kula chakula inaongezeka lakini wengi huwa inapungua,” anasema.

Uchovu wa mwili

“Hii nayo ni dalili nyingine mtu hupata uchovu wa mwili, wengi hulalamika kupata maumivu ya viungo vya mwili, maumivu ya kichwa, mgongo na sehemu zingine za mwili,” anasema.

Anaongeza “Huwa wanadhani kuna tatizo kwenye miili yao na kwa kuwa huwa hawapati usingizi, mwisho wa siku unakuta miili yao haipo ‘active’ katika kufanya kazi mbalimbali.

“Hufanya kazi kwa taratibu mno, tofauti na awali kiasi cha watu waliomzunguka kumshangaa, pamoja na dalili hizo wakati mwingine huambatana pia na suala la homoni za mwili, wengine hupatwa na ile hali ya usumbufu na wapo ambao hamu ya kujamiiana hupungua.

“Sasa pata picha mgonjwa huyu ni mwanandoa na mwenzake anamuhitaji lakini yeye hamu hana tayari kunakuwa na usumbufu unaojitokeza, iwapo mtu anakuwa hajabaini kwamba hiyo ni dalili ya sonona anaweza kudhani mwenziye anamfanyia makusudi, kumbe ni mgonjwa,” anasema.

Dalili za kitabia.

Dk. Lema anasema watu wanaougua sonona huwa wanatabia ya kujiondoa au kujitenga kwenye jamii, wanapenda kukaa maisha yao wenyewe.

“Inaweza kwenda hadi kwenye mawasiliano, unaweza kumpigia simu na asipokee, anakuwa hajisikii kabisa kupokea simu. Au kama alikuwa anapendelea kufanya vitu fulani mfano, kuangalia vipindi mbalimbali kwenye runinga anakuwa aangalii tena, anakuwa amejitenga na wakati mwingine huwa wanafanya vitu vingi kwa kujilazimisha,” anasema.

Tafiti

Anasema zinaonesha watu wengi wapo katika hatari ya kupata sonona kutokana na mambo waliyoyapitia katika maisha yao.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiGNk7lpyBKBQ-AmaOY34sz0Yju4BUFhBIIDHMIQYZ7CDVBPpsciBnwy9bQesEUlfoPBBIxfvFAVHljLsJnzYmi99FvyBDazwB7b3WC7XGjNXwB-1aXYvP66XyyEKZxCP3nfxVzhCIoYuA/s640/jeneza.jpg
Mambo yanayochangia

Anasema yapo mengi mfano kufiwa na wapendwa au watu wa karibu au kupotelewa na kitu cha thamani sana maishani.

“Kuna wakati fulani mtu unajikuta unakuwa na migogoro ya nafsi katika nafsi yako, yaani mfano unatamani jambo fulani liende vile unavyotaka lakini inakuwa kinyume chake, kwa hiyo unakuwa unajiuliza maswali mengi,  au unakuwa na migogoro na watu wengine.

“Kuna hali ya kutengwa na jamii pia, sasa mtu anapotengwa na matukio mengine kutokea katika maisha yanamfanya kuwa na ile hali ya huzuni (hapa inakuwa bado haijafikia kuwa ugonjwa).

“Kwa mfano, watu walikuwa kwenye uhusiano na ukavunjika, wakati ambapo hawa wawili hawajajiandaa kuondoka kwenye uhusiano, wanaweza kupata hali ya huzuni na kujiuliza kwanini uhusiano wao umevunjika.

“Na wakipitia hii hali ya huzuni wataanza kupata dalili nilizozitaja awali, kuvunja uhusiano si kitu kizuri, ila mtu kupitia zile dalili ni hali ya kawaida,” anasema.

Anaongeza “Lakini huyu mtu hawezi kuwa mgonjwa wa akili mpaka ile hali imeendelea si chini ya miezi mitatu.

Sababu nyingine

“Wengine hupata sonona, labda kwa vile amezaliwa katika familia ambayo ina hali ya uhatarishi ya kupata sonona, kwa sababu ni miongoni mwa magonjwa yanayorithiwa katika familia,” anasema.

Anafafanua “Lakini hatuwezi kuugua hadi tutakapofikia kile kiwango cha juu cha msongo wa mawazo kinachoweza kutufanya tuugue.
Ni vigumu kumtambua mgonjwa

Anasema hiyo ni kwa sababu mara nyingi mtu anapokwenda huwa hajielezi kwamba anajisikia huzuni, ameachwa au amefukuzwa kazi.

“Wengi hujieleza kwamba wanajisikia maumivbu ya kichwa, mwili, hawapati usingizi, sasa huyu mgonjwa akikutana na mtaalamu ambaye hafahamu dalili za magonjwa ya akili, anaishia kumpima magonjwa mengine kama malaria lakini mtu wa aina hii akitibiwa huwa haponi, kwa sababu anaugua sonona,” anasema.

Matibabu sahihi

Anasema mtu akigundua na kufika kwa wataalamu wa saikolojia humpa tiba sahihi na kupona kabisa.

“Huwa tunampa mgonjwa dawa tiba ambazo humsaidia kurejesha usingizi na kumrejesha katika hali yake ya kawaida, tunampa pia tiba za kisaikolojia ambazo humsaidia kwenye kufikiria na tunamtibu kwa njia ya kazi.

“Tiba za kisaikolojia zitamsaidia kumtoa katika hiyo hali, kisha tutamfanyia tiba ya kitabia na baadae atarudi katika hali yake ya kawaida kabisa,” anasema.

https://pbs.twimg.com/media/C6UpQLiWYAAIMx-.jpgWHO 

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na matokeo yake kutangazwa kuwa taarifa rasmi ya Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2014 inaeleza katika kila sekunde 40 mtu mmoja duniani hujiua. Ripoti hiyo inaonesha Tanzania kuwa nchi ya nane katika orodha ya nchi zinazoongoza  watu wake kujiua.


Utafiti huo ulifanyika katika nchi 172 duniani kwa miaka 10, Shirika hilo lilieleza kwamba tabia ya watu kuficha takwimu na kufuatilia matukio ya vifo inachelewesha uchukuaji hatua wa kudhibiti tabia hiyo ya kujiua na kwamba halitiliwi maanani wala kujadiliwa kutokana na kunyanyapaliwa na kuwepo kwa imani potofu zinazohusishwa na vifo hivyo.

WHO ilitaja tabia ya watu kujiua ni tatizo kubwa la kiafya duniani ambalo kwa sasa linalohitaji hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yake.

Ripoti hiyo inaonesha katika mwaka 2012 nchi zenye kipato kikubwa ziliongoza kwa mauaji ya aina hiyo ikiwa na vifo asilimia 12.7 kwa kila watu 100,000 huku nchi za kipato cha chini na kati zikiwa ni asilimia 11.2 kwa kila watu 100,000.

Lakini kutokana na nchi za kipato cha chini na kati kuwa na wingi wa watu, wao ndio waliochukua nafasi kubwa ya vifo hivyo, kwani robo tatu ya matukio kwa wastani yapo katika nchi hizo.

Hata hivyo ripoti hiyo inaonesha, nchi za Kusini Mashariki mwa Asia zikiwemo Korea Kaskazini, India, Indonesia na Nepal ndizo zilifanya theluthi moja ya waliojiua duniani.

Vifo vya kujiua katika nchi tajiri vinaelezwa kuwa wastani wa robo ya vifo vinavyotokea duniani kote vya aina hiyo, inataja njia kubwa  inayotumika karibu duniani kote ni kutumia sumu za mashambani, kujinyonga, kujipiga risasi na kuruka kutoka katika majengo marefu tabia ambayo ipo zaidi katika nchi za Asia, hasa maeneo ya miji.

Inakadiriwa kwamba watu zaidi ya 800,000 hufa kwa kujiua lakini pia wapo watu wengi wanaojaribu kujiua kwa namna tofauti, wastani wa dunia wa watu kujiua upo kwa asilimia 11.4 kwa kila watu 100,000 huku wanaume kama wanawake kwa idadi sawa hujaribu kujiua.

ripoti hiyo inataja nchi ambazo zinaongoza kwa vifo vya kujiua ni Guyana (asilimia 44.2 kwa kila watu 100,000), ikifuatiwa na Korea Kaskazini na Korea Kusini (asilimia 38.5 na 28.9 kwa kila 100,000).

Nchi nyingine ni Sri Lanka (28.8), Lithuania (28.2), Suriname (27.8), Msumbiji (27.4), Nepal na Tanzania (24.9 kila mmoja), Burundi (23.1), India (21.1) na Afrika Kusini (19.8). Nchi nyingine ni za Russia na Uganda (zote zikiwa na wastani wa 19.5), Hungary (19.1), Japan (18.5) na Belarus (18.3).

Katika nchi zenye kipato sababu kubwa inatajwa kuwa ni matatizo ya afya ya akili hasa msongo wa mawazo ambao husababisha asilimia 90 ya vifo vya kujiua ukilinganisha na asilimia 60 katika nchi za Asia kama China na India.

Lengo la WHO ni kupunguza idadi ya wastani wa kujiua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2020, ingawa utafiti unaonesha kuna changamoto kubwa kwani vifo hivyo kutokea katika makundi ambayo yanaonekana kutengwa, wengi wakiwa masikini, wenye matatizo mbalimbali na wanaoishi katika hali ya kutothaminiwa au kukubalika katika jamii.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement