Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Dk. Naiz akionesha jinsi wanavyofanya upimaji kuchunguza magonjwa ya moyo wa mtoto aliyeko tumboni. 

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara nyingine tena imefanya upimaji wa moyo wa mtoto aliye tumboni mwa mama yake, kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo.

Upimaji huo umefanywa leo katika taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Naiz Majani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Naiz amesema kuna faida lukuki iwapo mjamzito ataamua kufanya kipimo maalumu.

"Tunatumia Ultra sound kama kawaida kufanya kipimo hiki, lakini inakuwa ina tofauti kidogo... hatutumii mionzi yoyote, hivyo hakuna madhara anayoweza kuyapata mama au mtoto wake aliye tumboni," amesema.

Ametaja faida hizo kuwa ni kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo, na kuwaondoa kwenye masumbufu wanayoweza kuyapata kutokana na kuchelewa kupata matibabu.

"Kwa mara ya  kwanza tuliwafanyia kipimo hicho wajawazito 25 mwishoni mwa mwaka jana ambapo watano kati yao mimba zao zilikutwa na matatizo.

"Wajawazito hao wanatarajiwa kujifungua wakati wowote kuanzia sasa na watoto hao wataanza kufuatiliwa kwa ukaribu na kupewa matibabu ya haraka," amesema.

Amesema waliamua kuanza kufanya kipimo hicho baada ya kugundua watoto kadhaa hufikishwa katika taasisi hiyo wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha wao kushindwa kuwapatia matibabu.

Amesema inakadiriwa katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja anakuwa amezaliwa na magonjwa ya moyo.

"Mwaka jana inakadiriwa walizaliwa watoto milioni moja, kwa msingi huo watoto wapatao 12,000 walizaliwa na magonjwa haya lakini tuliowaona kliniki yetu ni kati ya 700 hadi 750 pekee," amesema.

"Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo yanatakiwa kutibiwa mapema, lakini wanakuja umri umeshakwenda tunashindwa kuwasaidia," amesema.
 http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/3401124/medRes/1305356/-/11tcbm6z/-/pichamoyo.jpg
Amesema kwa kufanya kipimo hicho wana uwezo wa kuona asilimia 90 ya magonjwa ya moyo.

"Kwa asilimia 10 tu hatuwezi kuona, tatizo kubwa kwa watoto ni matundu. Mtoto akiwa tumboni mwa mama yake kuna baadhi ya moyo wake huwa na baadhi ya matundu ambayo hata hivyo pindi anapozaliwa yanapaswa kuzibika.

"Sasa kama tukiona hali hiyo na akazaliwa yakawa bado yanaonekana moja kwa moja tunajua hilo ni tatizo," amesema.

Amesema wanaweza pia kuona iwapo milango ya moyo wa mtoto ina tatizo au la.

"Kipindi mwafaka kwa ajili ya kufanya kipimo hiki ni pale mimba inapokuwa na wiki 18 hadi 22, kwa nchi za wenzetu wamepiga hatua zaidi, kwa sasa wapo kwenye majaribio wakigundua mtoto ana tatizo wanalitibu mara moja akiwa huko huko tumboni," amesema.

Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema dhumuni kubwa la kuanzisha huduma hiyo ni kugundua matatizo hayo mapema.

"Tunahamasisha kina mama wajitokeze, Tanzania sasa imepiga hatua kubwa, tunafanya hivi kwa sababu asilimia 85 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji ni watoto.

"Na hawa ndiyo tunaowategemea kuwa Taifa la kesho, tusipowagundua na kuwatibu mapema maana yake ni kwamba watakuja kuwa mzigo kwa Taifa miaka ijayo," amesema.

Amefafanua kwamba miaka ya nyuma si  kwamba magonjwa ya moyo hayakuwapata watoto bali hayakuweza kugundulika kutokana na uhaba wa wataalamu, vifaa.

"Watoto wengi walikufa kwa kile kilichoelezwa ama ni typhoid, nimonia au surua, leo hii wataalamu tupo, tulikwenda kujifunza kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea ili tuisaidie nchi yetu, magonjwa yote ya moyo yanatibika," amesisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement