Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) inatarajia
kufanya kampeni maalumu ndani ya mwaka huu ya kuhamasisha jamii kutambua jinsi
ya kuepuka mama kuzaa mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Mkurugenzi wa Tiba wa MOI, Dk. Samwel Swai ameeleza hayo mapema leo
alipozungumza na waandishi wa habari walipotembelewa na viongozi wa dhehebu la
Shia ambao wameahidi kusaidia matibabu ya watoto 40 yaatakayogharimu Sh milioni
sita.
“Tatizo hili lipo kwa muda mrefu sasa nchini, leo idadi
imeongezeka kwa sababu jamii imepata uelewa, tunajitahidi kuwatibu kwa kadri ya
uwezo wetu, tiba yao ni mtambuka na ina vitu vingi mno kuikamilisha, tunahitaji
damu ya kutosha, usafiri wa kuwatoa huko walipo, dawa za usingizi na vifaa vya
kutosha ili kuwahudumia,” amesema.
Dk. Swai (anayezungumza) amesema wamejitayarisha kuwasaidia wale waliowaandaa huku
lengo lao kwa sasa ikiwa ni kutoa elimu kwa wananchi.
“Ni tatizo linaweza kuzuilika kwa kutumia lishe (folic acid)
ambayo hupatikana kwenye baadhi ya vyakula lakini tunatoa vidonge maalumu vya
folic acid, mama anatakiwa ameze miezi mitatu kabla ya kubeba ujauzito,”
amesema.
Amesema pia wamekusudia kupata wodi maalumu na wataalamu
watakaoshughulika kuwasaidia watoto hao peke yao.
“Tukihamia rasmi huku jengo jipya kule kwenye jengo la zamani
tutaweka chumba kimoja cha upasuaji maalumu kwa ajili ya watoto hawa peke yao,”
ameweka wazi.
Amesema jumamosi hii wanatarajia kuwafanyia upasuaji kati ya
watoto 25 hadi 30 ambao tayari wameandaliwa.
Chapisha Maoni