Na Leonard Mang'oha, Dar es Salaam
WAANDISHI wanne wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited wamepitishwa
kuwania tuzo za umahiri katika uandishi wa habari (EJAT), imefahamika.
Tuzo hizo, ambazo huhusisha waandishi wa habari wa magazeti, redio,
luninga, wapiga picha na wachora vibonzo, litafanyika Aprili 29, mwaka
huu jijini Dar es Salaam.
Waandishi waliopitishwa kupitia kazi mbalimbali zilizochapishwa katika
gazeti la MTANZANIA ni pamoja na Mhariri wa habari wa gazeti hilo,
Bakari Kimwanga, waandishi Veronica Romwald, Rodrick Ngowi na Nora
Damian, ambaye pia ni mshindi wa tuzo hizo katika kipengele cha
mwandishi bora wa habari za sayansi na teknolojia 2015.
Veronica pia ni mmiliki na mwendeshaji wa blog hii ya matukionamaisha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tuzo hizo, Kajubi Mukajanga,
alisema waandishi hao wanaungana na wengine 62 kutoka vyombo mbalimbali
vya habari nchini walioteuliwa baada ya mchujo wa awali uliofanyika kati
ya Aprili 6 na 13, mwaka huu Bagamoyo, mkoani Pwani.
Wateule hao watachuana kuwania tuzo hizo katika vipengele 19, ikiwa ni
pamoja na tuzo ya uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha,
michezo na burudani, afya, kilimo na biashara na biashara ya kilimo,
elimu, uandishi wa habari na uchambuzi wa matukio.
Nyingine ni habari za utalii na uhifadhi, afya ya uzazi kwa vijana,
manunuzi ya umma, kodi na ukusanyaji mapato, habari za uchunguzi, data
na haki za binadamu na utawala bora, VVU na Ukimwi, jinsia, wazee na
watoto na kundi la wazi, mpiga picha bora za runinga, magazeti na mchora
katuni bora.
Alisema mwaka huu mwitikio ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na mwaka
uliopita, ambapo jumla ya waandishi 810 waliwasilisha kazi zao kutoka
568.
Alisema idadi hiyo ni dalili njema na inaonesha jinsi gani waandishi wanalipa uzito mkubwa shindano hilo.
Pamoja na kujitokeza kwa idadi kubwa ya kazi zilizowasilishwa, idadi ya
kazi zilizopitishwa imeshuka kutoka 84 mwaka jana hadi 66 mwaka huu.
Jenerali Ulimwengu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku hiyo
“Pamoja na kuwa kulikuwa na kazi nyingi zilizowasilishwa na wanahabari
wa vyombo vya kielektroniki, ubora wao haukuwa mzuri. Majaji walisema
kazi kutoka kwenye magazeti zilikuwa na ubora zaidi,” alisema Mukajanga.
Mukajanga alisema kuwa, shindano hilo ni mwelekeo mzuri kwa wanahabari
kutambua na kutathmini tuzo hizo kama kipimo cha umahiri wa uandishi wa
habari.
Aliongeza jopo la majaji waliofanya mchujo huo liliongozwa na Valerie
Msoka, Katibu alikuwa Dk. Joyce Bazira, wengine waliokuwapo ni Dk. Mzuri
Issa, Hasan Mhelela, Pili Mtambalike, Mwanzo Millinga na Nathan
Mpangala.
Mgeni rasmi katika shindano hilo litakalofanyika katika Hoteli ya Blue
Pearl iliyopo Ubungo, Dar es Salaam, anatarajiwa kuwa mshindi wa tuzo ya
mafanikio ya maisha ya uandishi wa habari mwaka 2014, Jenerali
Ulimwengu.
Tuzo za EJAT huandaliwa kila mwaka kwa ushirikiano baina ya Baraza la
Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Tasisi
ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan),
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa).
Wengine ni Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Chama cha
Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), HakiElimu, AMREF, ANSAF,
Best-Dialogue na SIKIKA.
Chapisha Maoni