Na Veronica Romwald – Dar es Salaam
KUNA mtu leo hii akiambiwa asimame, azungumze mbele ya umati
wa watu, anashindwa kabisa na iwapo atajitahidi kusimama anaweza kutokwa jasho jingi
au kutetemeka kabisa na hata kusahau baadhi ya maneno aliyokusudia
kuyazungumza.
Lakini wapo watu ambao wanao uwezo wa kusimama na kuzungumza
kwa ufasaha pasipo kuwa na shaka yoyote ile.
Kuna mtu mwingine akiona kwa mfano mdudu mdogo kama mende
ameingia ndani ya chumba chake basi yupo radhi kuhama kwa muda chumba hicho na
kutafuta watu wa kumsaidia kumtoa mende huyo.
Simulizi
ya John
John Simon mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam anasema hawezi
kabisa kusimama mbele ya umati wa watu na kuzungumza.
“Natamani mno kusimama na kuzungumza mbele za watu, lakini
sijui kwanini huwa nakosa kabisa ule ujasiri, hofu kuu huwa inaniingia ndani ya
moyo wangu,” anasema.
Simon anasema hata alipofanikiwa kuendelea na masomo yake ya
sekondari alikuwa anachelewa kufika shuleni ili asichaguliwe kuzungumza kwenye
gwaride.
“Shule niliyosoma, viranja waliweka utaratibu wa kuita
wanafunzi mbele kuzungumza jambo, hasa siku ya jumatatu, basi nilikuwa
nachelewa makusudi ili nisichaguliwe,” anasema.
Anasema hali hiyo anayo hadi leo na hajui kama anaweza
kuondokana nayo.
“Jambo ninaloshukuru mimi sina nafasi yoyote ya uongozi
kazini, nadhani wanajua nina udhaifu huu maana hawajawahi kunichagua
kuzungumza, sijui lini nitaweza kupata ule ujasiri walio nao watu wengine,”
anasema.
Wapo watu wakimuona mende 'hutimua' mbio
Mariam
Mariam
Mariam Eliud, Mkazi wa Magomeni anasema yeye akimuona mende ameingia
ndani ya nyumba yake anakosa amani kabisa.
“Yaani bora nimuone nyoka simuogopi hata kidogo, nitampiga
mwenyewe hadi nimuue lakini si mende, nikiona yupo ndani nakosa amani kabisa.
“Nyumba yangu ina vyumba viwili vya kulala, nipo radhi nihame
chumba changu kwenda kingine, nitatafuta na mtu aje kunisaidia kumuua mende
huyo kwa kutumia dawa maalumu ya kuua wadudu,” anasema.
Wazazi wanavyochangia
Msaikolojia Tiba wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi
Muhimbili (Muhas), Isack Lema anasema wengi wanakumbwa na hali hiyo ukubwani
lakini msingi wake ulianzia walipokuwa utotoni.
“Wazazi wengi hawajui, ni kosa kubwa kumtamkia maneno
yanayomvunja moyo mtoto au kumshusha thamani.
“Unakuta mtoto anajitahidi kuonesha kipaji chake lakini mzazi
anamvunja moyo na kumwambia hawezi kufika popote, au kwa mfano mwanafunzi
ananyoosha mkono darasani kujibu swali akakosea, wenzake wakamcheka.
“Mwalimu anatakiwa amsaidie mwanafunzi husika, kumjenga, ili
asiogope tena wakati mwingine kujibu, amsaidie kujenga ule ujasiri, wengi
wanaoshindwa hata kusimama mbele ya watu ukubwani, walichekwa au kukatishwa
tama walipokuwa utotoni,” anasema.
Nini
hutokea
Lema (pichani) ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya
Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anasema wasiwasi uliopitiliza ni
tatizo la akili lakini wengi hudhani ni hali ya kawaida.
“Kila mmoja anaugua ugonjwa wa wasiwasi lakini si rahisi
kuona watu wakija hospitalini kupata matibabu kwa sababu wengi hudhani ni hali
ya kawaida, kwa sababu mara nyingi huwa si rahisi kusababisha athari za moja
kwa moja, na utaona wengi huendelea kufanya shughuli zao za kila siku kama
kawaida,” anasema.
Dk. Lema anasema kawaida magonjwa ya akili huanza na vitu
ambavyo ni vya kawaida kabisa.
“Kwa mfano mtu alikuwa analala kwa saa nane inafika hatua
hawezi tena kulala analala kwa saa mbili, hali hiyo ikiendelea kwa zaidi ya
miezi mitatu tayari ni tatizo, inakuwa si hali ya kawaida tena bali ugonjwa,”
anasema.
Kila
mwanadamu ameumbwa na hofu
Daktari huyo anasema jinsi Mwenyezi Mungu alivyoumba mwili
amemuwekea kila mtu hofu ndani yake.
“Ni hali tuliyoumbwa nayo katika mfumo wa akili, hofu ni sawa
sawa na ‘alarm’ ya gari, kwa mfano
nikiigusa gari yangu vibaya ‘alarm’ itatoa mlio, kuashiria gari
haikuguswa vizuri.
“Hofu katika maisha ya binadamu ni hali ambayo ipo na
inatusaidia kuishi maisha yetu ya kila siku hasa tunapokabiliwa na hali za
hatari,” anasema.
Mwanamume akipambana na simba porini
Anaongeza “Kwa mfano tunajua kwamba simba ni mnyama hatari, ikitokea mtu akakutana naye porini, macho yake humsaidia kuona, hofu iliyopo ndani yake hutoa ishara na ubongo hupokea taarifa na kwamba kilichopo mbele yake ni kitu cha hatari.
Anaongeza “Kwa mfano tunajua kwamba simba ni mnyama hatari, ikitokea mtu akakutana naye porini, macho yake humsaidia kuona, hofu iliyopo ndani yake hutoa ishara na ubongo hupokea taarifa na kwamba kilichopo mbele yake ni kitu cha hatari.
Anasema kwa sababu hiyo, mwili nao ambao umeumbwa ukiwa na
mfumo wa kumsaidia mtu kupambana nao huanza kujiandaa kukabiliana na hatari
hiyo.
“Mwili utaachilia homoni na mhusika ataanza kukabiliana na
ile hatari, kuna njia mbili ambazo muhusika ataweza kuzitumia ama kupambana na
simba huyo au kukimbia, hofu ya namna hii ni ya kawaida kabisa,” anasema.
Kwa nini
ni kawaida
Dk. Lema anasema kwa kuwa ni hali ya hatari na macho
yamepeleka taarifa kwenye ubongo, nao utatuma taarifa kwa mwili ujiandae
kupambana, ni hali ya kawaida.
“Cha kwanza mwili utahitaji muhusika avute pumzi ya kutosha
ili kuweza kujiandaa, kisayansi mwili huvuta hewa ya oksijeni na kutoa nje hewa
ya kabonidioksaidi,” anasema.
Anasema hewa hiyo huenda hadi kwenye mapafu na ikifika huko
kuna mabadiliko ambayo hutokea katika pumzi iliyoingia ndani.
Kuna watu wanaogopa hata kupanda ndege
“Sasa mtu aliyekutana na simba, huanza kuvuta pumzi nyingi kwa nguvu, kwa kuwa anavuta kwa nguvu ile oksijeni inafika pale kwenye mapafu ambapo hata hivyo si kituo chake cha mwisho.
“Sasa mtu aliyekutana na simba, huanza kuvuta pumzi nyingi kwa nguvu, kwa kuwa anavuta kwa nguvu ile oksijeni inafika pale kwenye mapafu ambapo hata hivyo si kituo chake cha mwisho.
“Pumzi hiyo inatakiwa isafirishwe kwenda katika sehemu
mbalimbali za mwili. Kwa kuwa anavuta pumzi kwa nguvu, matokeo yake ni kwamba
mapigo ya moyo huanza kuongezeka, kuwezesha pumzi yenye oksijeni ifike sehemu
zote za mwili,” anasema.
Hofu inavyogeuka
kuwa ugonjwa
Dk. Lema anasema hofu hugeuka kuwa ugonjwa iwapo inatokea pasipo
kuwa na kisababishi chochote cha hali ya hatari.
“Yaani, inakuja katika hali ya ghafla na inakuwa nje ya uwezo
wa mtu husika kuweza kuitawala hiyo hofu na katika mazingira ambayo hakuna
sababu ya muhusika kupata hofu,” anasema.
Anatoa mfano “Ni sawa na alarm ya gari inapopiga wakati
hakuna kitu kilichoigusa gari husika. Hii inamaanisha alarm husika ina tatizo.
Hofu inapompata mtu bila kuwapo kwa kisababishi cha hatari inakuwa si hofu ya
kawaida tena (tuliyoumbwa nayo) bali ugonjwa wa wasiwasi.
Aina za
magonjwa ya wasiwasi
Daktari huyo anasema wapo watu ambao hupata wasiwasi wa
kuhamaki kitaalamu hali hiyo huitwa Panic- disorder.
“Unakuta mtu yupo mahali ghafla anapatwa na hofu, anahamaki,
anakuwa kwenye tafrani kweli kweli na hata akafikia hatua ya kukung’ang’ania
wewe uliyekaribu naye.
"Lakini ukiangalia mazingira unaona kabisa hakuna kitu
ambacho kinaweza kumfanya mtu kuingiwa na hofu namna hiyo,” anasema.
Wapo wanaoogopa kupanda au kupita kando kando ya majengo marefu au kusafiri baharini
Anasema wengine hupata wasiwasi ambao huendana na wao kuona vitu fulani fulani kwa mfano wadudu, wanyama, mabonde na vingine vingi.
Anasema wengine hupata wasiwasi ambao huendana na wao kuona vitu fulani fulani kwa mfano wadudu, wanyama, mabonde na vingine vingi.
“Kwa mfano kuna mtu akipanda lifti anapatwa na wasiwasi,
anahisi akiingia kwenye lifti atakosa pumzi, joto litakuwa kali na matokeo yake
atapoteza uhai wake, hivyo anashindwa kabisa kupanda lifti. Au mwingine
anaogopa kupanda kabisa ndege,” anasema.
Anasema mwingine akikaa juu ya ghorofa au akienda sehemu
ambapo pana mwinuko mrefu huhisi hali ya kizunguzungu .
“Wapo wengine wakiona damu wanapatwa na hali ya wasiwasi, kuna
kundi la tatu la wasiwasi wa kijamii, unakuta kuna watu wanahisi kukaa katika
kundi la watu wengi kuna kitu kinaweza kutokea.
“Hawa ndio wale ambao wakipewa nafasi ya kuzungumza mbele za
watu wanahisi huenda kuna jambo baya linaweza kutokea au watamfikiria vibaya au
atatokewa na vitu vya ajabu ajabu,” anasema.
Anasema wengine hupata wasiwasi wa kila kitu kilichopo mbele
yake.
“Yaani wanakuwa si watu wa kuwa na uhakika wa kila jambo
wanalofanya, wanahisi lazima watakosea, kwa sababu ni mambo ambayo huanza
katika hali ya kawaida ili tuseme ni tatizo lazima dalili zisiwe za siku mbili
tatu,” anasema.
Anasema lazima muhusika afanyiwe uchunguzi na wataalamu na
dalili hizo awe ameziona kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.
Mara nyingi mtu hutumia mikono yake kuficha uso pindi anaposhikwa na uwoga
Dalili za ugonjwa
Dalili za ugonjwa
Anasema wakati ni hali ya kawaida kwa mtu anayekabiliana na
hali ya hatari kuvuta na kutoa pumzi haraka haraka kwa mtu ambaye anapatwa na
hali hiyo bila kuwa na kisababishi cha hatari hali huwa tofauti.
“Yule anayekabiliana na hatari ataona anavuta hewa katika
hali ya kawaida lakini huyu ambaye hakabiliani na hatari yoyote atapata shida
mno, ataanza kujiuliza kwanini mapigo yake ya moyo yamebadilika na kwenda kasi
na anaanza kuhisi kifua kinakuwa kizito, hilo ni tatizo,” anabainisha.
Zimegawanyika
Daktari huyo anasema dalili za ugonjwa huo zimegawanyika katika makundi makuu matatu, ya
kwanza ikiwa ni dalili ya mwili ambayo wengi huanza kuipata.
“Mara
nyingi muhusika huona ile pumzi anayoivuta ni ndogo, haimtoshi, kwa hiyo
anaijitahidi kuivuta kwa nguvu na ndiyo maana anakuwa anahisi kama vile kifua
kinabana na wakati huo huo mapigo ya moyo huanza kwenda kwa kasi,” anasema.
Anasema kwa kuwa wakati hali hiyo inatokea huwa kunakuwa na
nguvu ambayo imeachiliwa ndani yake anaanza kutetemeka mwili.
“Wengine huanza kutokwa jasho jingi kiasi cha kulowanisha
nguo zao, wapo wengine huhisi kabisa kama vile kuna kipepeo kinaruka ruka ndani
ya tumbo,” anasema.
Huathiri
kibofu.
Dk. Lema anasema mara nyingi inapotokea mtu akapatwa na ugonjwa
wa wasiwasi humsababishia athari katika kibofu chake cha mkojo.
“Kibofu hulegea na ndiyo maana mtu hujihisi kwenda haja
ndogo, kila anapopatwa na hali ya wasiwasi, wapo ambao huhisi kizunguzungu,
wengine tumbo huunguruma na wapo ambao huishiwa kabisa nguvu mwilini na hata kupoteza
fahamu kabisa,” anasema.
Dalili
za kiakili
Anasema hili ni kundi la pili la dalili, kwamba mtu huwa na hofu
kuu, huhisi huenda kuna kitu kibaya ambacho kitatokea katika maisha yake.
“Unakuta anatafakari mno juu ya hayo anayodhani huenda
yatamtokea matokeo yake mapigo ya moyo yanabadilika, yaanza kwenda kasi kwa
hofu anayokuwa ameijenga ndani yake juu ya hayo anayohisi yatamtokea,” anasema.
Dalili
za kitabia
Anasema watu wanaougua ugonjwa wa wasiwasi huanza kuepuka
kukaa katika maeneo au vitu vyote ambavyo huwasababishia kukumbwa na hali hiyo.
“Kwa mfano utakuta mtu anakwepa kukaa au kusimama mbele ya kundi
la watu, kupanda lifti, kupanda gari, ndege na vitu vingine vingi
vinavyomsababishia hali ya wasiwasi,” anasema.
Anaongeza “Kuna tabia fulani tunaziita za kiusalama, kwamba
mtu anaona ili awe salama ni vema aepuke mazingira yote yanayoweza
kumsababishia kupata wasiwasi.
Si
rahisi kugundua tatizo
Anasema kwa sababu suala hilo linalohusisha mwitikio au
mabadiliko ya kimwili wengi hudhani wanakabiliwa na tatizo la pumu (athima).
“Wengine hudhani wanasumbuliwa na shinikizo la damu,
wanakwenda hospitalini lakini wakitibiwa hawaponi kwa sababu si ‘pressure’ ya
kawaida,” anasema.
Kundi linaloathirika
zaidi
Anasema ni vijana, ambao kawaida huwa wamefunzwa mambo mengi
kipindi cha utotoni na uishi kwa kuamini katika kile walichofundishwa.
“Tatizo lina vyanzo vingi, jinsi tunavyokuwa tumelelewa, kwa
mfano walizoea kukutishia tishia, unajikuta unakuwa mtu mwenye wasiwasi kila
wakati tangu ukiwa mtoto.
“Lakini wakati mwingine kuna malezi ambayo yanatuweka katika
mazingira ambayo ni ya kuogopa kila wakati, kwa mfano mtu anayeogopa mende
ukimuuliza kwanini anamuogopa mende wengi huwa hawana majibu ya kujitosheleza,”
anasema.
Tiba
Anasema wagonjwa wa wasiwasi hupewa matibabu ya kibaiolojia
ambapo hupewa dawa zinazowasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida
wanapopatwa na wasiwasi.
“Kuna tiba za kisaikolojia pia, kwa mfano mtu alipata tukio
fulani likamjengea hali ya wasiwasi, tiba hizi huwa zinatusaidia kumfanya mtu
arejee katika hali yake ya kawaida,” anasema.
*Makala haya kwa mara ya kwanza imechapishwa katika gazeti la MTANZANIA Mei 4, mwaka huu
Chapisha Maoni