NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kingwangalla amesema
watu wanaohusika na ukusanyaji wa taarifa za kihistoria watakwenda kumfanyia
mahojiano Francis Maige (86).
Dk. Kingwangalla alisema
hayo juzi wakati alipokwenda kumjulia hali Maige ambaye maarufu kwa jina la
Ngosha ndiye aliyebuni Nembo ya Taifa (bibi na bwana) katika Hospitali ya Amana
ambako alikuwa amelazwa kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa matibabu zaidi.
“Inawezekana kuna vitu vingi
bado hatuvijui kuhusu nembo hii, watakuja watu wa kukusanya historia kumuhoji
mzee Maige naamini kuna mambo mengi atawaeleza,” alisema.
Dk. Kingwangalla akimjulia hali Mzee Maige
Akizungumza, Mzee huyo
alisema nembo hiyo aliibuni na kuichora mnamo mwaka 1957 pamoja na mwezake Ali
Panga mwenyeji wa Tanga ambaye hata hivyo kwa sasa ni marehemu.
“Tulichora nembo hiyo mwaka
1957 baada ya kupewa tenda, tuliambiwa kwamba itatumika pindi Mwenyezi Mungu
atakapotujalia kupata uhuru na kweli tulipata,” alisema.
Pamoja na hayo, Ngosha
alisema anampango wa kumpatia Rais John Magufuli zawadi ya picha tatu ambazo
amezichora.
“Ninazo picha tatu, ya
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais Mstaafu Jakaya
Kikwete na ya kwake mwenyewe (Rais Magufuli ambazo nimepanga kumpatia zawadi,”
alisema.
Chapisha Maoni