moja

Responsive Advertisement

Mwanamke akisoma kitabu alichopewa katika mkutano huo kinachotoa elimu ya kupinga ukatili.

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

APRIL 12, mwaka huu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alikiri kwamba kuna ongezeko kubwa la watoto wa mitaani hasa katika miji mikubwa.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji ambaye alihoji serikali inachukua hatua gani kukabiliana na ongezeko la watoto wa mtaani.

Waziri Ummy alisema Utafiti uliofanywa mwaka 2012 katika mikoa kumi unaonesha jiji la Dar es Salaam linaongoza kuwa na idadi kubwa ya watoto wa mitaani kwa asilimia 28.

Alitaja mikoa mingine ni Dodoma kwa asilimia nane, Mwanza asilimia saba, Morogoro asilimia saba, Tanga asilimia sita, Iringa asilimia tano, Pwani asilimia tano, Kilimanjaro asilimia tano na Arusha asilimia nne.

Lakini kiuhalisia mitaa huwa haizai watoto, binadamu ndiye anayezaa hivyo inaaminika kwamba watoto hao wametoka katika familia zao kutokana na sababu moja au nyingine huku sababu kubwa ikitajwa umasikini.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Charambe, Fikiri Mtenukila (pichani) anasema sababu nyingine ambayo anaona inachangia ongezeko hilo ni wanamume kutelekeza familia zao.

“Wapo baadhi ya wanamume wana tabia ya kuzalisha wanawake na kuwatelekeza, unakuta mama ameachiwa watoto watatu au wanne, anashindwa kuwahudumia vema, wanakosa malezi ya baba, wanashindwa kupata mlo kamili na kukosa fursa ya kusoma,” anasema.

Anasema tabia hiyo ni mbaya na kwamba wanamume wanapaswa kujitambua na kuachana nayo kwani inatesa familia hasa watoto wengi wamekuwa wakikosa haki zao za msingi na kukimbilia kuishi maisha ya mtaani.

“Inasikitisha mno, binafsi kitendo hiki nakichukulia kuwa sawa na ukatili wa kijinsia, wanawatesa wakina mama na watoto ambao wanawaacha katika mazingira magumu, kweli unaweza kukuta maisha ni magumu lakini hiyo isiwe sababu ya wao kuzikimbia familia zao, wavumilie, wasaidiane kulea familia,” anasema.

Anasema katika Kata hiyo amekuwa akipokea kesi zipatazo mbili hadi tatu za ukatili wa kijinsia pamoja na hizo za wanamume kutelekeza familia zao.

“Mara nyingi mwisho wa kesi wanamume hao huwa tunalazimika kuwapeleka polisi na ustawi wa jamii ambako huko huwa wanatakiwa kutunza familia zao kwa mujibu wa sheria, lakini kwa nini iwe hivyo, nawashauri wanamume wasikimbie majukumu yao, wakae walee familia zao ili watoto wapate haki zao za msingi,” anashauri.

Mtenukila anasema Kata hiyo imejipanga madhubuti kupambana na vitendo hivyo kwa kushirikisha moja kwa moja wenyeviti wa serikali za mitaa, wajumbe wao na kamati za maendeleo zilizoundwa.

“Tuna mikakati madhubuti ambayo tunashirikiana nao kuelimisha jamii, suala la kupinga ukatili wa kijinsia ni kipaumbele chetu, tunahakikisha jamii inapewa elimu ya kutosha juu ya madhara yatokanayo na ukatili wa kijinsia,” anabainisha.

Hidaya Nanjundu (anayehojiwa juu na mwandishi) ni mjane anayeishi katika kata hiyo ambaye ameathirika na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Anasema enzi za uhai wa mume wake walijaliwa kupata mali nyingi na watoto wanane lakini maisha yao yalibadilika baada ya kifo chake.

“Ndugu walikuja wakachukua mali zote, wakaniachia watoto pekee niwalee, ilikuwa ni maisha magumu kwangu, sikuwa na namna nyingine, nilikesha nikilia peke yangu, sikujua wapi pa kupata msaada,” anasema.

Anasema alipata wazo la kufanya biashara ndogo ndogo ili kupata fedha za kumuwezesha kuishi yeye na watoto wake katika maisha yao hayo mapya.

“Huu ni mwaka wa 30 tangu mume wangu afariki dunia, kwa kweli wajane tunaumizwa mno na vitendo vya ukatili wa kijinsia, tunashindwa kutatua matatizo tuliyonayo kwa sababu hatujapata watu wa kutushika mkono kutuongoza.

“Wengi tunaathirika kisaikolojia, tunakata tama, tupo kwenye wakati mgumu, hatupati haki zetu, binafsi niliamua kuanzisha kikundi hiki kwa uchungu mkubwa, pamoja na kusaidiana kiuchumi lakini tunatafuta pia msaada wa kisheria tupate haki zetu,” anasema.

Mjane huyo ambaye sasa ameanzisha kikundi kiitwacho wajane group huko Mbagala, anapewa mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia na msaada wa kisheria katika Shirika la Maendeleo ya Vijana (TYDC) ambalo linashirikiana kwa ukaribu na WILAC.

Mwenyekiti wa Shirika hilo, James Isdore (pichani) anasema lilianzishwa mwaka 2009 na kwamba hadi sasa wameweza kuwafikia watu zaidi ya 500 kufikisha elimu hiyo.

Anasema huwa wanatumia njia mbalimbali kuwafikia kwa kushirikiana na serikali hasa za mitaa na kuwaeleza madhara yatokanayo ya ukatili wa kijinsia.

“Huwa tunawaelimisha wananchi mahali wanapoweza kupata msaada pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, lakini pia tunakutana na kuzungumza na wadau mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani,” anasema.

Anasema huwa pia wanawajengea uwezo wananchi ambao tayari wameathirika na vitendo hivyo, wapo ambao huwasaidia kwa namna moja au nyingine kujikwamua na wengine huwapeleka mbele zaidi na kuwapatia msaada wa kisheria ili wapate haki zao.

“Changamoto kubwa ambayo tunaiona ni kitendo cha baadhi ya watumishi wa serikali hasa askari wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakijihusisha na usuluhishi katika kesi mbalimbali na kuzikwamisha.

“Yaani, kwa mfano, mjomba amebaka mtoto wa dada yake, unakuta askari anasuluhisha matokeo yake, kesi ya jinai inageuka kuwa ya kijamii, mwisho anaachiwa huru,” anasema.

Anaongeza “Wengi hurudi uraiani jambo ambalo wengine huona kumbe inawezekana kufanya kitendo cha ukatili na ukaachiwa huru kwa njia ya usuluhishi, ndiyo maana vitendo hivi vinazidi kutokea.

Makala haya kwa mara ya kwanza yalitoka katika gazeti la MTANZANIA

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement