Taka zikiwa zimetupwa na kutelekezwa mtaani (picha na mtandao)NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KILIO cha ukosefu wa ajira sit u cha Tanzania bali
dunia nzima, kundi kubwa linaloathirika likiwa ni la vijana.
Tunashuhudia wengi wakikata tamaa huku baadhi yao
wakiamua kujiingiza katika shughuli ambazo si halali.
Wengine kutokana na hali hiyo wamekuwa wakitumbukia
katika matumizi ya dawa za kulevya na hili ni janga la Taifa.
Vijana ni nguvu kazi muhimu inayohitajika kutumika kwa
Taifa lolote duniani katika shughuli za uzalishaji kukuza uchumi wake.
Kila kukicha kilio cha ukosefu wa ajira kinazidi
kuongezeka huku serikali katika kila nchi zikijitahidi kutafuta mbinu za
kukimaliza.
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John
Magufuli imedhamiria kufufua viwanda kupitia kauli mbiu yake ya Tanzania ya
viwanda ili kukabiliana na hali hiyo.
Jambo hilo, linaungwa mkono na wadau wengi hasa vijana
wenyewe lakini bado kuna changamoto nyingi kufikia lengo hilo hasa sera nzuri
za kuhamasisha uwekezaji wa kutosha nchini.
Miaka ya nyuma vijana wengi walisoma wakitarajia
kuajiriwa pindi watakapomaliza masomo yao, lakini si wote waliokuwa wakiajiriwa
na hivyo kujikuta wengi wakiishia mitaani huku wakiwa hawana ajira ya
kuwaingizia kipato.
Leo hii ingawa bado wapo ambao wamebaki na mawazo
mgando (wanasubiri kuajiriwa) wengi wameamka na kuamua kujiajiri wenyewe na
sasa wanafurahia matunda ya maamuzi yao.
Sabore Mussa (pichani) ni Meneja wa kampuni ya Africraft anasema yeye
na wenzake zaidi ya 10 waliamua kutumia mikono yao kujitengenezea ajira.
“Tulitafakari namna gani tunaweza kukabiliana na
changamoto ya ukosefu wa ajira tukaona ni vema tutumie ufahamu tulionao kubuni
bidhaa mbalimbali na kutumia mikono yetu kuzitengeneza bidhaa hizo,” anasema.
Mussa anasema walianzisha kampuni yao mwaka 2006 na
kwamba huwa wanatengeneza bidhaa zao kwa kutumia malighafi ambazo wengi
huzitupa baada ya kumalizika muda wake.
“Wazo letu ni la tofauti kidogo na wengi wanavyodhani, tunatumia makopo yaliyokwisha tumika hasa yale
ya soda za kopo, vifuu, chupa, mifuko ya plastiki, viroba vya unga wa ngano na
sembe na ile ya saruji.
“Utaona malighafi hizi wengi huzitupa baada ya
kuzitumia na kutokana na hali hiyo, taka hizo zimekuwa zikichangia mno
uharibifu wa mazingira yetu,” anasema.
Anasema tangu wakati huo hadi sasa kampuni yao imekuwa
na wameweza kufundisha vijana wenzao ambao wamejiajiri kwa kazi hiyo.
“Sasa hivi tupo vijana zaidi ya 30 ambao tumejiajiri
kwa kazi hii, tumesambaa katika maeneo mbalimbali nchini,” anasema.
Kuhusu soko
Anasema wamefanikiwa kupata soko kubwa la bidhaa zao
wanazotengeneza hasa nchini Ujerumani na Marekani.
“Soko la ndani (Tanzania) si kubwa sana kama tunavyoona
Ujerumani na Marekani, kwa mfano kuna bidhaa ambayo katika soko la ndani
tutauza kwa Sh 2,000, bidhaa hiyo hiyo tukiipeleka nje hasa nchi hizi mbili
tunaweza kuiuza kuanzia Sh 1,0000 na kuendelea,” anasema.
Mussa anasema hiyo ni kwa sababu mwamko wa watanzania
kupenda bidhaa zinazotengenezwa ndani kwa malighafi za kitanzania ni mdogo.
“Wengi wanapenda kutumia bidhaa zinazotoka nje ya nchi
lakini illi tukuze uchumi wetu wakati umefika sasa tuanze kupenda bidhaa zetu
za ndani zilizotengenezwa na watanzania wazalendo,” anasema.
Anasema serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri kwa
wabunifu, wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani ili vijana wengi zaidi
wavutiwe kujiajiri.
Amabilis Batamula ni Mkurugenzi wa Habari wa Jarida la
Fema anasema vijana wengi bado hawajui kwamba wanaweza kujipatia mamilioni ya
fedha katika taka.
“Vijana hawana elimu ya kutosha kwamba taka wanazoziona
zikizagaa huko mitaani wanaweza kuzitumia kujipatia fedha na kuondokana na
tatizo la ukosefu wa ajira, zinabaki na kuchafua mazingira,” anasema.
Anasema leo hii dunia inashuhudia mabadiliko ya hali ya
nchi ambayo yamechochewa zaidi na uharibifu wa mazingira.
Anasema Juni 5, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku
ya Mazingira Duniani, waliungana na wadau mbalimbali kusherehekea siku hiyo kwa
njia ya kipekee.
“Tulikutana na vijana na kuwapa elimu namna wanavyoweza
kutumia taka kupata fedha, tunaamini watatumia elimu hiyo kujiajiri, tunahimiza
wajiajiri na walinde mazingira, kwa sababu dunia inatuhitaji tuitunze,
tusipoitunza na yenyewe itashindwa kututunza,” anasisitiza Batamula.
Anaongeza “Utaona matairi ambayo yamekwisha tumika
kwenye magari mengi hutupwa, kandambili hutupwa pia, lakini zipo ambazo vijana
wamefanya usafi huko baharini zikizagaa zimetumika kutengeneza mapambo mazuri
mno, utashangaa.
“Kwa hiyo wamesafisha kulinda mazalia ya samaki lakini
pia wamejipatia fedha, ndiyo maana tumeamua kuhamasisha vijana watumie fursa
hii kwani licha ya kupata kipato tutalinda mazingira yetu ikiwamo kuzuia
mmonyoko wa udongo,” anasema.
Mhifadhi Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Alhaji
Seleman Kisimbo anasema ili kuendana pia na dhamira ya serikali ya Tanzania ya viwanda
ni wakati mwafaka watanzania kutumia elimu hiyo.
“Elimu ya kubadili taka kuwa bidhaa imekuja wakati mwafaka,
nawasihi vijana watumie fursa hii na watafute taarifa zaidi ili kwa pamoja
tufikie lengo kufikia Tanzania ya viwanda lakini pia kulinda mazingira jambo
ambalo ni wajibu wa kila mmoja wetu,” anasema.
Makala haya kwa mara ya kwanza yalitoka kwenye gazeti la MTANZANIA
Makala haya kwa mara ya kwanza yalitoka kwenye gazeti la MTANZANIA
Chapisha Maoni