Madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Peter Kisenge (kushoto) na Subhash Chandra (kulia) kutoka Hospitali ya BLK ya India wakifanya upasuaji wa kupandikiza pacemaker kwa mgonjwa hivi karibuni.
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
NI kifaa kidogo mno ukikitazama machoni, ambacho
hupachikwa kwa ustadi wa hali ya juu kwa njia ya upasuaji katika moyo wa
binadamu ili kumsaidia kuishi.
Licha ya udogo wake wa umbo lakini, kifaa hicho kina
uwezo mkubwa wa kusaidia kuzuia kifo cha ghafla kwa mtu anayesumbuliwa na
magonjwa ya moyo hasa shinikizo la damu.
Kwa kawaida kifaa hicho hupandikizwa kwa mtu ambaye
utendaji kazi wa moyo wake upo chini ya ya kiwango cha asilimia 50 na wale
ambao kiwango chao cha mapigo ya moyo ni chini ya 40 kwa dakika.
Wataalamu wa afya wanasema kifaa hicho kina uwezo wa
kurekebisha kiwango cha mapigo ya moyo yaliyo chini.
Wanasema mara nyingi watu wenye tatizo hilo huanguka
ghafla na kwamba hali hiyo husababishwa na kule kuziba kwa mishipa ya damu.
Wanasema kitendo cha mishipa ya damu kuziba husababisha
damu kushindwa kupita kwa wepesi kwenda katika sehemu mbalimbali za mwili.
Hivi karibuni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na Taasisi ya Madaktari Afrika ya nchini Marekani ilifanya
upasuaji na kuwapandikiza kifaa hicho jumla ya wagonjwa 12.
Jinsi unavyofanyika
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Peter
Kisenge anasema kabla ya kumfanyia mgonjwa upasuaji wa kupandikiza kifaa hicho
kwanza hufanyia uchunguzi kwa kutumia kipimo maalumu cha ECG.
Pacemaker
“Kipimo hicho ndicho ambacho hutupa mwelekeo iwapo
mgonjwa husika anapaswa kufanyiwa upasuaji kupandikizwa ICD pacemaker au la,”
anabainisha.
Anasisitiza kifaa hicho kina uwezo wa kuzuia kifo cha
ghafla hasa kwa wagonjwa ambao wana tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu.
“Wagonjwa ambao tunawapandikiza kifaa hiki ni wale
ambao utendaji kazi wa mioyo yao ulikuwa upo chini ya kiwango cha asilimia 50,
hawa mara nyingi huishiwa nguvu na kujikuta wakianguka ghafla,” anasema.
Anaongeza “Wagonjwa wengine ambao upandikizwa kifaa
hiki ni wale ambao kiwango cha mapigo yao ya moyo kilikuwa chini ya 40 kwa
dakika.
Ni
upasuaji ghali
Daktari huyo anasema nchini India upasuaji huo
hugharimu hadi Sh milioni 100 kwa kila mgonjwa mmoja kiasi ambacho ni kikubwa.
“Lakini kwa kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa
hapa JKCI, tunafanya upasuaji huo ambapo kila mgonjwa mmoja anagharimu kiasi
cha Sh. milioni 30, hivyo kwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa hao tumeokoa zaidi
ya Sh milioni 300 ambazo zingetumika kuwatibu nje ya nchi,” anasema.
Anasema pamoja na wagonjwa hao, wagonjwa wengine wawili
wamefanyiwa upasuaji wa kupandikizwa betri maalumu iitwayo kitaalamu
CRTD-pacemaker.
Anasema betri hiyo imewekwa kwa wagonjwa ambao baada ya
kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia kipimo cha ECG waligundulika mapigo yao ya moyo
yalikuwa yapo chini mno
“Unaweza kuona ICD – pacemaker na CRTD –pacemaker ni
vifaa ambavyo vinafanana lakini kila kimoja kina kazi yake na hadi tunamfanyia
upasuaji mgonjwa na kumpandikiza ni lazima tumpfanyie uchunguzi kwa kutumia
kipimo cha ECG ambacho hutusaidia kujua mgonjwa anastahili kuwekewa kifaa
kipi,” anafafanua.
Picha inayoonesha moyo wa binadamu
Kwanini
mishipa huziba
Inaelezwa, kwa kawaida binadamu anapofanya shughuli
yoyote ile mwili wake huhitaji kiwango fulani cha damu, mahitaji ya kiwango cha
damu huongezeka kulingana na shughuli husika anayokuwa anaifanya kwa wakati
huo.
Hata hivyo iwapo itatokea mwili wa ukahitaji kiwango
fulani cha damu lakini kikakosekana moja kwa moja mtu husika hupata matatizo
makubwa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ili damu ifike
katika sehemu mbalimbali za mwili ni
lazima ipite katika mishipa ya damu.
Wanasema kwa kawaida mishipa ya damu huwa haipaswi kuwa
na mafuta ya aina yoyote na iwapo kunakuwa na
mafuta yoyote yale, husababisha kuziba kwa uwazi unaoruhusu damu kupita.
Wanasema uwazi huo unapokuwa umezibwa kwa kiwango cha
asilimia 50 ndipo pale mtu husika huanza kupata shida mbalimbali.
Shida
zenyewe
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo anasema mara nyingi mtu ambaye
mishipa yake imeziba huanza kuhisi maumivu ya kifua.
“Maumivu hayo huwa makali mno hasa katika upande wa
kushoto na hata mtu huyo anapofanya shughuli yoyote ndogo hujikuta mwili wake
hukichoka haraka,” anabainisha.
Daktari huyo anafafanua “Kawaida mtu anapofanya
shughuli yoyote mwili wake huhitaji kiwango fulani cha damu na kwamba mahitaji
hayo hutofautina kulingana na shughuli anayoifanya kwa wakati huo.
Mtu akiugulia maumivu makali ya kifua.
“Sasa unakuta mwili unahitaji damu lakini kwa kuwa
mafuta yapo kwenye mishipa ya damu hushindwa kupita kuzunguka kwenye mwili.
“Matokeo yake kadiri muda unavyozidi kwenda mbele
mafuta yanazidi kutanda kwenye damu hasa kwenye mishipa inayopeleka damu kwenye
moyo na kuziba kabisa ule uwazi, matokeo yake mtu hupata shinikizo la damu na
wengi hufariki ghafla hasa wanapokuwa usingizini,” anabainisha.
Dk Pallangyo anasema hali hiyo hutokea pale mishipa ya damu inapokuwa imeziba kwa
kiwango cha asilimia 100.
Hali
ya ugonjwa
Anasema tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu enzi za
mababu zetu lilionekana kuwaathiri zaidi watu ambao walikuwa na umri wa kuanzia
miaka 40 na kuendelea.
Daktari huyo anasema katika miaka ya hivi karibuni,
hali ni tofauti kabisa kwani tatizo hilo linaonekana kuwakumba zaidi watu walio
na umri wa kuanzia miaka 40 kushuka chini.
Anasema tafiti zinaonesha awali tatizo hilo lilikuwa
likiwakumba zaidi watu wanaoishi katika nchi zilizoendelea lakini leo hii
linaonekana kuwapo zaidi katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.
Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi husababisha shinikizo la damu
Visababishi
Daktari huyo anasema zipo sababu nyingi ambazo
husababisha kuziba kwa mishipa ya damu lakini zimegawanyika katika makundi
makuu mawili.
“Kuna suala la lishe, tunazungumzia kuhusu suala la
ulaji mbovu hasa vyakula vyenye mafuta mengi, uzito kupindukia, kutokufanya
mazoezi, unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara,” anasema.
Anasema sababu nyingine huhusisha magonjwa mbalimbali
hasa yale ya shinikizo la damu na kisukari.
Mgonjwa
Ally Aboud (45) (si jina lake halisi), mwenyeji wa mkoa
wa Tanga ni miongoni mwa wagonjwa wanaosubiri kufanyiwa upasuaji kutibu tatizo
la kuziba kwa mishipa ya damu.
Anasema katika maisha yake alikuwa akipendelea mno
kuvuta sigara na kwamba hakuwahi kufikiria iwapo zitamfikisha katika hali
aliyonayo sasa.
“Nilipenda
kuvuta sigara, hata watu waliponishauri niache au hata nipunguze
sikuwasikiliza, niliona ni sehemu ya maisha yangu, kwa siku nilikuwa nina uwezo
hata wa kumaliza sigara 20,” anasema.
Ally anasema alianza kuvuta sigara alipofikisha umri wa
miaka 20 baada ya kushawishiwa na marafiki zake ambao alikuwa akikaa nao
kijiweni kila siku jioni.
“Walinishawishi nikaanza kuvuta kidogo kidogo kwa
kujificha nyumbani wasijue, lakini kadri muda ulivyokwenda ndivyo nilivyonogewa
na nikaanza kuitafuta mwenyewe (kununua
dukani), kumbe nimejisababishia matatizo,” anasema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Tiba ya Moyo
ya Jakaya Kikwete, Pedro Pallangyo (kulia) akizungumza na mwananchi aliyejitokeza kupima afya.
Wengi
wanaugua
Dk. Pallangyo anasema
katika taasisi hiyo kila wiki wanaona wagonjwa zaidi ya 35 wenye tatizo la
kuziba kwa mishipa ya damu.
“Iwapo ukikadiria idadi
hiyo utaona kwa mwezi tunaona wagonjwa wapatao 140, katika mwaka 2015/16
tuliwafanyia uchunguzi takribani wagonjwa 400 katika mtambo wetu maalumu wa
‘cath lab’,” anasema.
Anasema katika maonesho
ya kimataifa ya biashara (sabasaba) waliwafanyia uchunguzi watu 1,375 ambapo asilimia 31 kati yao walikutwa na
tatizo la shinikizo la juu la damu.
“Kati ya hao asilimia
39.2 walikutwa na uzito mkubwa, wagonjwa 39 tuliwapa rufaa kuja hapa JKCI, wote
walikuja na kati ya hao wagonjwa 31 tuliwakuta na shinikizo la juu la damu na
wagonjwa saba wamegundulika wana tatizo la moyo mkubwa, mmoja alikutwa na
tatizo kwenye milango ya moyo wake (valve) wameanza kupata matibabu,” anasema.
Ushauri
Dk. Pallangyo anashauri
ni vema jamii ikaepuka na kuachana na tabia hatarishi zinazosababisha tatizo
hilo.
“Viasababishi vingi
vinaepukika kwa mfano suala la kuacha kuvuta sigara, kufanya mazoezi,
kuzingatia ulaji unaofaa ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wa kila mmoja,
ukiacha zile sababu nyinginezo za ugonjwa,” anasema.
Anaongeza “Tubadilike na
kuzingatia mfumo bora wa maisha, kwa sababu gharama ya kutibu tatizo hili ni
kubwa, na mara nyingi wale wanaomudu ni wale ambao wana bima ya afya, Wale
wasio na bima hushindwa kabisa kumudu.
Kufanya mazoezi mara kwa mara kutakuepusha na hatari hii.
Huduma
kusogezwa karibu na jamii
Dk. Kisenge anasema ili kusogeza huduma ya matibabu na
afya ya moyo karibu zaidi na jamii, taasisi hiyo sasa imeanza kutoa mafunzo kwa
madaktari wa ngazi ya uzamivu.
“Madaktari hao pindi watakapomaliza masomo yao
wanatarajiwa kwenda katika Hospitali ya Mloganzila (iliyopo nje kidogo ya jiji
la Dar es Salaam na Hospitali ya Benjamini (Dodoma),” anasema.
Ushirikiano
zaidi
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya
Madaktari Afrika, Mathew Sackett anasema taasisi hiyo ipo tayari kuendelea
kushirikiana na JKCI kutoa huduma hiyo.
“Ni mara yangu ya kwanza kuwapo nchini Tanzania,
nimefurahi kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali hapa,” anasema.
Anaongeza “Madaktari Afrika tutaendelea kushirikiana na
JKCI kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu na kufanya upasuaji kuwasaidia
wagonjwa ili tuokoe maisha ya wengi zaidi.
Makala haya kwa mara ya kwanza yamechapishwa, Julai 27, mwaka huu katika gazeti la MTANZANIA.
Chapisha Maoni