Picha na mtandao
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
HAIKUWA rahisi kwa Mariam Mussa Mkazi wa Temeke
kumshawishi mumewe (jina tunahifadhi) kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango
kupanga uzazi.
“Nilikutana na mume wangu huko Tandika mwaka 2010
wakati huo nilikuwa nikifanya biashara ndogondogo katika soko la Tandika, wote
tulikuwa wafanyabiashara sokoni hapo, tulipendana na kukubaliana kuishi,”
anasema.
Anasema mwaka uliofuata alihisi kuwa ni mjamzito
akaamua kwenda katika kituo cha afya ambapo alifanyiwa vipimo vilivyothibitisha
kweli ni mjamzito.
“Tulibahatika kupata mtoto wetu wa kwanza wa kiume,
nilijifungua katika hospitali ya binafsi ambako huko walinishauri nianze
kutumia njia za uzazi wa mpango,” anasema.
Anasema alirudi nyumbani kwake na kumjulisha mumewe
taarifa hizo ambazo hata hivyo alionesha wazi kutokubaliana na suala hilo.
“Hakuonesha furaha yake niliyoizoea kuiona kila
nilipomueleza jambo ambalo lilimpendeza, aliniangalia kwa hasira mno basi
nikanyamaza kimya na kuacha kabisa kulizungumzia suala hilo,” anasema.
Mariam anasema pamoja na kukaa kimya huko aliamua kufanya
jambo hilo mwenyewe kwa siri pasipo kumshirikisha mumewe.
“Nilianza kutumia njia ya sindano ambapo haikuwa rahisi
kwake kubaini kwani nilikuwa nikienda kuchoma kule hospitalini, nilipoona
mwanangu amefikia umri wa miaka miwili niliacha kuchoma nikabeba ujauzito wa
pili,” anasema.
Anasema ilimlazimu kuacha matumizi ya uzazi wa mpango
kila baada ya miaka miwili ili mumewe huyo asishitukie juu ya jambo hilo
aliloamua kulifanya mwenyewe.
“Sasa hivi tuna watoto watatu, bado sijamueleza kwamba
niliamua mwenyewe kutumia njia ya uzazi wa mpango kwani nina wasiwasi kwamba
huenda ataniacha jambo ambalo sipo tayari kuona likitokea,” anasema.
Si Mariam pekee anayekumbana na hali hiyo, jamii nyingi
zilizopo katika bara la Afrika hasa Tanzania zinaamini kwamba suala la kupanga
uzazi ni la mwanamke pekee na wala halimuhusu kabisa mwanamume.
Frank Eugene (38) anasema haoni sababu ya mwanamume
kupanga uzazi na wala si jukumu lao kabisa.
“Hakuna sababu ya kumlazimisha mwanamume atumie njia za
uzazi wa mpango au kumshawishi mwanamke kutumian njia ya uzazi wa mpango,
wakati hata vitabu vya dini vinatueleza tuliletwa duniani ili tuzae tuijaze
nchi,” anasema.
Msimamo huo wa Eugene ndiyo walio nao wanamume wengi
ambao Ofisa Mawasiliano na Utetezi wa Chama cha Malezi Tanzania (UMATI), Josephine
Mugishangwe anasema si mtizamo sahihi.
“Ni kweli Mwenyezi Mungu amesema tuzae lakini ni lazima
kuangalia na kupanga idadi ya watoto ambao mtu anao uwezo wa kuwahudumia na
kuwapa malezi bora na elimu bora itakayomsaidia katika maisha yake ya baadae,”
anasema.
Muuguzi wa Hospitali ya Temeke, Framan Swai
akiwafafanulia jambo kuhusu masuala ya uzazi wa mpango wanawake ambao
waliohudhuria jana katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani
Hali
halisi
Takwimu zinaonesha kwamba kasi ya kuzaliana nchini kwa
sasa ni kubwa hali ambayo inasababisha kuwapo kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini.
Kulingana na sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 1967 idadi
ya watu iliongezeka kutoka milioni tisa ilivyokuwa mwaka 1961 hadi kufikia watu
milioni 12.3.
Aidha, katika sensa ya mwaka 2012 idadi hiyo
iliongezeka hadi kufikia watu milioni 45.
Inakadiriwa kila mwaka watanzania milioni 1.5
wanazaliwa na hivyo huenda idadi hiyo imefikia zaidi ya milioni 50 tangu
kufanyika kwa sensa hiyo ya mwaka 2012.
Ofisa Habari wa Tume ya Mipango Tanzania, Adili Mhina
anasema kasi ya ongezeko hilo imesababisha kuwapo kwa changamoto kubwa ya upungufu
wa miundombinu na huduma za kutosheleza mahitaji.
“Mahitaji yameongezeka kwa sababu kuna shinikizo la
ongezeko la idadi ya watu, kila mwaka vijana milioni 1.2 wanafikia umri wa
kuingia katika soko la ajira lakini vijana 300,000 pekee ndiyo wanaobahatika
kuajiriwa.
Athari
zake
Mhina anasema kutokana na hali hiyo leo hii
kunashuhudiwa wimbi kubwa la watu hasa vijana wakihama katika maeneo ya mijini
kutafuta ajira.
“Ndipo pale tunashuhudia uanzishwaji wa maeneo ya
biashara zisizo rasmi yasiyoendana na taratibu za ustawi wa jamii pamoja na
ujenzi wa makazi holela,” anasema.
Athari
zaidi
Meneja Utetezi wa Shirika la Advance Family Planning
(AFP), James Mlali anasema ongezeko hilo ni hatari kwani linaweza kuja kuathiri
uchumi wa nchi hapo baadae.
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya suala la uzazi wa mpango
na maendeleo, leo hii tunashuhudia idadi ya watoto wanaoanza elimu ya msingi
haiendani na idadi ya miundombinu iliyopo.
“Yaani mahala pengine majengo hayatoshelezi, vifaa
havitoshelezi, walimu hawatoshelezi, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya
navyo siku hizi havitoshelezi,” anasema.
Anaongeza “Tafiti zinaonesha kama tutazidi kuongezeka
miaka 25 ijayo tutahitaji kuwa na vituo vya afya mara tatu ya hivi vilivyopo
sasa, yaani kama tuna vituo 7,000 basi tutahitaji kuwa na vituo 21,000, kama
tuna shule za msingi 10,000 tutahitaji kuwa na shule 30,000.
“Aidha, tutashuhudia pia ongezeko kubwa la ukosefu wa
ajira, upungufu wa wataalamu, ongezeko la watu wanaohamia katika maeneo ya
mijini, ni hatari kwa maendeleo ya nchi,” anabainisha.
Nini
kifanyike
Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA-Tanzania), Dk. Hashina Begum
anasema ni muhimu kupanga uzazi.
Anasema afya ya uzazi iliyo nzuri inayoambatana na njia
za uzazi wa mpango inaweza kukuza uchumi na kuchangia maendeleo endelevu kwani
wanawake hupata fursa ya kumaliza eluimu na kuwa sehemu ya nguvu kazi kuchangia
pato la taifa na familia zao.
Anaongeza “Kwa hiyo afya ya uzazi wa mpango ni muhimu
katika kufikia lengo namba moja la Maendeleo Endelevu (SDG’s) ambalo ni
kutokomeza umaskini, njaa na mengineyo.
Muelimishaji Rika wa Chama cha Uzazi na Malezi Tanzania (UMATI), Neema Gaitana akimuelimisha matumizi sahihi ya kondomu kwa kutumia kifaa maalumu wakati wa maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani hivi karibuni katika viwanja vya Temeke Mwembe Yanga.
Anasema hata hivyo hali inaonesha kila siku wanawake walio katika mazingira hatarishi hasa walio masikini na wakimbizi wanakumbana na changamoto za kijamii, kiuchumi na kijiografia zinazowakosesha kupata huduma za uzazi wa mpango.
“Pamoja na hatua kubwa zilizofanywa lakini changamoto
bado zipo, wanawake milioni 214 katika nchi zinazoendelea wanakosa taarifa za
uzazi wa mpango na wengi wao wanaishi katika mataifa 69 yaliyo maskini
duniani,” anasema.
Dk. Begum anasema shirika hilo limejipanga kuhakikisha
linakabili changamoto za kukosekana kwa huduma za uzazi wa mpango nchini
ifikapo mwaka 2030 hata hivyo ili kufikia lengo hilo ni lazima pawepo na
ushirikiano wa dhati kati ya serikali na wadau wengine wa maendeleo.
“Serikali ya Tanzania inajitahidi mno kuwekeza katika
suala la uzazi wa mpango lakini jambo tunaloliona ni kwamba elimu zaidi
inahitajika kuwafikia jamii, iwapo jamii itapata elimu hiyo na kuitumia vizuri,
serikali itaweza kuokoa kiasi cha Dola moja hadi sita inazowekeza huko na
kuzitumia katika shughulki zingine za maendeleo,” anabainisha.
Faida
yake
Mratibu wa Dawa za Uzazi wa Mpango wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Cosmas Swai anasema kuna faida
nyingi iwapo wenza wataamua kupanga uzazi.
“Uzazi wa mpango ndiyo njia pekee itakayotuwezesha
kukabili ongezeko la kubwa la idadi ya watu lililopo sasa,” anasema.
Dk. Swai anasema matumizi ya njia za uzazi wa mpango
husaidia kuzuia vifo vya uzazi kwa kina mama kwa kiwango cha asilimia 30 hadi
50.
Anasema pia husaidia kupunguza ongezeko la idadi ya
watu na hupunguza uwezekano wa kuharibika kwa mimba.
“Hatua hiyo pia inasaidia kupunguza idadi ya vifo vya
watoto wachanga, ikiwa tutachagua njia za uzazi wa mpango kupanga uzazi
itatuwezesha pia kuwa na Taaifa bora,” anasema.
Anaongeza “Wakina mama nao wataweza kushiriki katika
shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hivyo watakuza uchumi wa familia zao
na Taifa kwa ujumla.
Ushauri
Dk. Swai anawatoa hofu wanawake juu ya matumizi ya njia
za uzazi wa mpango na kusisitiza kuwa njia hizo hazina madhara yoyote kwa
mtumiaji.
“Isipokuwa wanaweza kupata maudhi madogo madogo lakini
si wote, inaweza kweli kutokea mwingine akanenepa sana au akapungua sana,
lakini kama mwanamke ameanza kutumia njia moja wapo ya uzazi wa mpango na
ikamsumbua ni vema arudi kwa wataalamu wa afya wamsaidie,” anashauri.
Anasema upo mtazamo kwenye jamii kwamba njia za uzazi
wa mpango husabisha saratani hata hivyo si kweli kwani husaidia kupunguza
uwezekano wa mtu kupata maradhi hayo.
Serikali
imejipangaje
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dk. Neema Rusibayamila anasema serikali imekusudia kuongeza kiasi cha
fedha kutoka Sh. bilioni 14 hadi Sh bilioni 17 ifikapo 2020 zitakazotumika
kuboresha huduma za uzazi wa mpango nchini.
Dk. Neema ndiye ambaye aliiwakilisha Tanzania katika
mkutano wa kimataifa kuhusu
masuala ya uzazi wa mpango uliosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshugulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).
Anasema hatua hiyo imelenga kuhakikisha huduma za
kisasa za uzazi wa mpango zinapatikana kwa kiwango cha asilimia 100 ifikapo
2020 kutoka kiwango cha asilimia 94 kilichopo sasa.
“Tumekusudia pia kuongeza idadi
ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za afya ya uzazi kwa vijana kutoka asilimia
30 mwaka huu hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2020,” anasema.
Anaongeza “Dhamira
yetu (Tanzania), ni kufikia maelfu ya wanawake na wasichana na kuwapa elimu
kuhusu afya ya uzazi na huduma za kisasa za uzazi wa mpango, tumekusudia
kuwafikia wasichana 345,000 kufikia mwaka huo.
Naibu Katibu wa Tume ya Mipango, Ibrahim Kalengo anasema
ili kukabili hali hiyo mwaka 1992 serikali ilipitisha sera ya Taifa ya Idadi ya
Watu.
“Mwaka 2006 serikali iliandaa sera mpya ambayo kwa sasa
nayo inafanyiwa mapitio ili kuendana na mahitaji ya wakati wa sasa kutokana na
maendeleo na mabadiliko mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,” anasema.
Kwa mara ya kwanza makala haya yalichapishwa katika gazeti la MTANZANIA Julai 20, mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza makala haya yalichapishwa katika gazeti la MTANZANIA Julai 20, mwaka huu.
Chapisha Maoni