Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Macho ya mtoto wako yanapobadilika na kupata kengeza jambo
unalotakiwa kufanya ni kumuwahisha hospitalini afanyiwe uchunguzi na kupatiwa
matibabu sahihi.
Makengeza yametajwa kuwa ni miongoni mwa dalili za saratani
ya jicho ambayo inaonekana kuwatesa watoto wengi katika miaka ya hivi karibuni.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Judith Mwende alisema hayo hivi karibuni alipozungumza na
MTANZANIA kwenye mahoajiano maalumu.
Mahojiano hayo yalijikita kuzungumzia tatizo la saratani ya
jicho kwa watoto, ambapo alisema kila mwaka wanapokea watoto kati ya 100 hadi
150 wanaougua ugonjwa huo.
“Asilimia 70 hadi 90 ya watoto tunaowapokea wanaletwa
wakati ugonjwa ukiwa upo katika hatua za tatu na nne, katika hatua hizi ugonjwa
unakuwa umesambaa kwa sehemu kubwa,” alisema.
Dk. Mwende alisema wazazi wengi wanapohojiwa wanaeleza
kwamba waliona mabadiliko mbalimbali katika macho ya watoto wao lakini
walidhani ni ya kawaida.
“Wapo ambao wanatueleza walianza kuona macho yamepata
kengeza, ingawa si mara zote, lakini mara nyingi kengeza ni miongoni mwa dalili
za saratani ya jicho kwa watoto,” alisema.
Daktari huyo alitaja dalili zingine za awali za tatizo hilo
ni weupe kwenye mboni ya jicho, jicho kuvilia damu, jicho kuwa jekundu na
kupata maumivu.
“Dalili nyingine ni mtoto wa jicho, jicho kuwaka kama paka
usiku au mwanga mweupe pindi unapopiga picha na ‘flash’ na dalili zingine
hutokea kadiri ugonjwa unavyozidi kukomaa kwa mfano jicho kuvimba na kuwa
kubwa,” alisema.
Aliongeza “Hivyo ni vema wazazi wanapoona mabadiliko haya na
mengineyo wasipuuze na kukaa nao nyumbani wakiwatibu wenyewe kwa kununulia dawa
bila ushauri wa daktari, wawalete hospitalini wapate tiba stahiki.
“Ingawa dawa zote ni halali kwa matumizi na salama lakini ni
hatari hasa zinapotumika bila kufuata maelekezo maalumu ya wataalamu wa afya,
zinaweza kusababisha upofu,” alifafanua.
Habari hii imetoka leo kwenye gazeti la MTANZANIA leo
Chapisha Maoni