Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
WATUMISHI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwamo
madaktari, wauguzi na wale wa kada nyinginezo wameanza upya kuhakikiwa taarifa
zao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema uhakiki
huo unafanyika kufuatia agizo walilopokea kutoka serikalini.
“Ni kweli tulifanyiwa uhakiki, lakini tumepokea barua
inayotaka tuhakiki tena watumishi na tayari tangazo limebandikwa katika mbao za
matangazo na uhakiki umeanza,” alisema.
Aligaesha alisema baada ya kukamilika kwa uhakiki huo,
taarifa za watumishi hao zitatumwa katika ngazi husika serikalini.
MTANZANIA lilipita katika moja ya mbao za matangazo iliyopo
katika jengo la utawala na kuona tangazo hilo ambalo limesainiwa na Mkurugenzi
wa Utumishi, Makwaia Makani.
Kupitia tangazo hilo, Makani alisema uhakiki huo utafanyika
kwa watumishi wote kupitia taarifa za kitambulisho cha Taifa (NIDA) na taarifa
zilizopo katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).
Alisema uhakiki huo utaanza rasmi Julai 18, mwaka huu hadi
Agosti 15, mwaka huu.
“Muhimbili itaendesha zoezi la uhakiki wa wafanyakazi wake
wote kwa kutumia taarifa zilizopo katika kitambulisho cha Taifa pamoja na
taarifa zilizopo katika mfumo wa LAWSON, ikiwa ni kutekeleza agizo la
serikali,” alisisitiza.
Aliongeza “Uhakiki huo utafanyika katika darasa la komputa
lililopo katika jengo la utawala. Katika kuhakikisha uhakiki huo unafanikiwa
wafanyakazi wote wanatakiwa kuzingatia yafuatayo: kila mmoja awe na
kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho chake.
“Kila mfanyakazi awe na kitambulisho cha kazi, wafanyakazi
wote waliopo likizo yoyote ndani ya nchi wahakikishe wanafika na kuhakikiwa taarifa
zao,” alisema.
Makani alisisitiza ni lazima watumishi wazingatie suala la
nidhamu katika kipindi chote cha uhakiki huo.
“Aidha, wakurugenzi wakuu wa idara, vitengo, wakuu wa
majengo na wodi zote, wanatakiwa kuhakikisha wafanyakazi wote walio chini yao
wanahakikiwa bila kukosa,” alisisitiza.
Uhakiki huo unafanyika ikiwa ni siku chache tangu
Muhimbili, kupitia Ofisa Uhusiano wake, Neema Mwangomo kueleza kuwa watumishi
saba wa hospitali hiyo ambao awali walitajwa kuwa miongoni mwa watumishi
waliokutwa na vyeti feki kushinda rufaa zao.
Katika uhakiki wa awali, jumla ya watumishi 134 walibainika
kuwa na vyeti feki vya kitaaluma ambao walitakiwa kujiondoa wenyewe kazini
kabla ya Mei 15, mwaka huu.
Chapisha Maoni