Picha na mtandao
Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
Serikali imekusudia kusafirisha
dawa, chanjo na nyaraka mbalimbali kwa kutumia ndege maalumu zisizotumia rubani
kufikisha huduma haraka kwa wananchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali
kusaini mkataba na kampuni ya Zipline ya nchini Marekani.
Katibu Mkuu (Afya) wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mpoki Ulisubsya amesema hayo
Dar es Salaam wakati wa utiaji saini mkataba huo kati ya Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) na kampuni hiyo.
Dk. Mpoki amesema ndege hizo
zitatumika kusafirisha dawa katika vituo vya afya, hospitalini na zahanati
zisizofikika kwa urahisi.
“Tunatarajia kuanza rasmi mradi huu,
mwakani katika mkoa wa Dodoma katika vituo vya afya 200 mkoani humo
ambavyo havifikiki kirahisi,” amesema.
Amesema baada ya kuanza kwa
utekelezaji wa mradi huo, Taasisi ya utafiti ya ifakara itafanya utafiti kubaini
matokeo ya mradi huo na kutoa mapendekezo kama una matokeo mazuri ili kusaini
mkataba mwingine wa mikoa kumi ya hapa nchini.
"Wananchi 10,000 na vituo vya
afya 10000 katika mikoa yote itakayopita Mradi huu watanufaika, ikiwemo
mikoa ya Kanda ya Ziwa, Pwani na Nyanda za Juu kusini,” amesema.
Ameongeza “ Katika mwaka huu wa
fedha serikali iliongeza fedha katika bajeti yetu hivyo tunajipanga kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora za afya na kuweza kufikia jamii iliyopo pembezoni
mwa nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Laurean Bwanakunu amesema mradi huo pindi utakapoanza utasaidia kuokoa maisha ya watu kwani dawa zitafika kwa
wakati hata maeneo yenye miundombinu mibovu.
“Serikali kwa kushirikiana na MSD
imeweka mikakati kuhakikisha inatoa huduma kwa jamii kwa karibu ili kuweka
kuvifikia vituo vya afya zaidi ya 5,640a vilivyo chini ya mashirika ya dini na vingine vilivyoingia
mkataba na serikali kwa kutoa huduma kwa wananchi,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Zepline
Keller Rinaudo amesema ndege hizo zitakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa dawa au
nyaraka zenye kilogramu 1.8 kwa safari moja.
Amesema pia zitakuwa na uwezo wa
kusafirisha kilometa 150 kwenda na kurudi na kuahidi kampuni yake itahakikisha
inatoa ajira nchini kwa vijana wengi na kuboresha huduma hiyo ili ifanyike kwa
urahisi zaidi.
Chapisha Maoni