Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Picha na mtandao

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

TANGU siku sifuri hadi miezi tisa ya ujauzito, mtoto hutegemea kupokea vitu vyote muhimu kwa ajili ya ukuaji wake kuanzia chakula (virutubisho), hewa, maji na vinginevyo kutoka kwa mama yake kupitia kondo la nyuma.

Kisayansi  kondo la nyuma ndiyo kiunganishi pekee kinachowaunganisha mama na mtoto katika kipindi chote cha ujauzito.

Wataalamu wa afya wanasema ni muhimu mno kwa mjamzito kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito wake.

Kliniki ndipo sehemu pekee ambako mjamzito  hufanyiwa uchunguzi wa kina na wataalamu wa afya kufuatilia maendeleo ya mtoto wake aliyepo tumboni mwake.

Aidha, huko hupatiwa matibabu na ushauri sahihi inapobidi ili kumuwezesha kujifungua mtoto mwenye afya njema na uzito unaostahili.

Mara kadhaa imepata kutokea katika baadhi ya maeneo, watoto kuzaliwa na kugundulika kuwa na maambukizi ya malaria kali, hali inayowashangaza wengi.

Daktari Sigsbert Mkude ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi na Matibabu, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria nchini, na hapa anafafanua kuhusu suala hilo katika makala haya (karibu, soma uelimike).

“Kisayansi mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na ugonjwa wa malaria kitaalamu inaitwa ‘congenital malaria’, lakini jambo hilo huwa ni nadra sana kutokea,” anabainisha

Anasema ni nadra kutokea kwa sababu katika kondo la nyuma la mama kuna njia mbalimbali za kinga za asili ambazo humkinga mtoto aliyepo tumboni kupata ugonjwa huo.

“Mama anapokuwa na maambukizi kwenye kondo la nyuma, vimelea vya malaria hutumia mwanya huo kwa kusafiri kupitia kondo la nyuma kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” anabainisha.

Anasema inapotokea hali hiyo ndipo pale mtoto huzaliwa akiwa tayari ameambukizwa malaria kali.

“Ndiyo maana tunahamasisha kina mama wafike kliniki, hata kama hana dalili tukimpima kwa kipimo cha MRDT tukakuta ana vimelea vya malaria tunampatia dawa mapema ili kuzuia asimuambukize mtoto wake aliye tumboni,” anafafanua.

Dk. Mkude (pichani) anasisitiza mjamzito anapowahi mapema kliniki tunampatia chandarua chenye dawa ili kumkinga dhidi ya mbu waenezao malaria na anapogundulika kuwa na malaria tunampa dawa ili kuangamiza vimelea vya malaria.

Baada ya kuzaliwa

Anaongeza “Tunasisitiza mjamzito kuhudhuria kliniki kwa matibabu kwa sababu katika kipindi cha mwezi wa kwanza tangu mtoto kuzaliwa mara nyingi magonjwa anayoyapata huwa ni ya maambukizi na hupitia kwenye kitovu.

“Katika ule mwezi wa kwanza ikitokea kwa bahati mbaya kitovu chake kikachafua, kama kitovu hakijafunga vizuri  kunakuwa na uhusiano mkubwa wa kitovu na mishipa yake ya damu ikiwa atapata ugonjwa huugua mno,” anasema.

Anasema hata hivyo mara nyingi watoto wadogo huwa hawaoneshi dalili ya homa na kwamba wakati mwingine huwa wanakuwa baridi au hushindwa kunyonya.

“Akipata maambukizi kupitia kitovu mara nyingi wengine hutokwa vipele katika eneo la shingoni, hivyo ni muhimu mama kuhudhuria kliniki,” anasema.

Hali ipoje nchini

Dk. Mkude anasema tafiti zinazoendelea kufanyika nchini tangu mwaka 2000 hadi sasa zinaonesha kiwango cha maambukizi ya malaria kinazidi kupungua.

“Tangu mwaka 2000 hadi sasa kiwango cha maambukizi ya malaria kimepungua hadi asilimia 30, na idadi ya vifo imepungua kwa kiwango cha asilimia 33 na 34 katika kipindi hicho,” anasema.

Anasema mahudhuria ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa mwaka ni kati ya wagonjwa milioni 10 hadi 12.

“Hawa ni wale ambao hufika kutibiwa na kuondoka nyumbani, malaria husababisha vifo vya takriban watu 5,000 kila mwaka nchini sawa na asilimia 30,” anabainisha.

Kundi lililopo hatarini

Anasema tafiti zinaonesha wananchi wenye kipato cha chini ndio ambao wengi hupata maambukizi ya ugonjwa huo kuliko wale ambao wana kipato kizuri.

“Zaidi ya asilimia 90 wanaishi kwenye maeneo yenye maambukizi ya malaria, ukitazama hali ya maambukizi ya ugonjwa huu kwa mfano kwenye eneo kama Mikocheni unaweza kukuta mtoto mmoja kati ya watoto 100 anaugua malaria lakini Vingunguti na Buguruni hali inakuwa kinyume chake,” anasema.

Anasema katika miaka ya hivi karibu takwimu zinaonesha idadi ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kutokana na ugonjwa huo zinaonekana kupungua.

“Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010 malaria ndiyo ugonjwa ambao ulikuwa unaongoza kwa vifo lakini tangu mwaka 2010 hadi sasa kuna magonjwa mengine yameibuka kwa mfano magonjwa ya njia ya hewa tunaona yamepiku ugonjwa wa malaria.

“Mwaka 2015 NIMR walifanya utafiti ambao ulionesha kwamba idadi ya vifo vitokanavyo na malaria vinapungua  lakini bado ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vya watu wengi,” anasema.

Mbu anayeeneza malaria

Idadi ya maambukizi kimkoa

Dk. Mkude anaitaja mikoa yenye kiwango kikubwa cha Katavi, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Simiyu.

“Lakini kwa miaka 15 sasa kiwango vya maambukizi kimepungua kwa asilimia zaidi ya 50 ingawa mikoa yenye maambukizi ya malaria inaonekana kuongezeka,” anasema.

Anasema takwimu za mwaka 2016 zinaonesha asilimia 6.0 ya watu maskini wapo katika maambukizi kuliko wenye uwezo mkubwa kifedha ambao kiwango cha maambukizi ni asilimia 1.0.

“Hii inamaanisha kwamba makazi bora yaliyojengwa katika mpangilio mzuri hasa katika miji mikubwa inasaidia kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria kuliko maeneo yenye makazi duni,” anabainisha.

Anataja mikoa yenye kiwango kidogo cha maambukizi ni Dar es Salaam, Iringa, Pwani, Kilimanjaro, Njombe, Songwe na Ruvuma.

Changamoto

Mkurugenzi wa Kitengo cha Udhibiti Mbu Waenezao Malaria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Charles Mwalimu anasema ingawa chandarua ni njia rahisi na bora kujikinga dhidi ya mbu waenezao malaria hata hivyo wapo watu kwenye jamii huogopa kuvitumia.

“Kuna imani potofu ambazo zimejengeka huko kwenye jamii, baadhi ya wanaume wamekuwa wakikataa kulala kwenye vyandarua eti watapata tatizo la upungufu wa nguvu za kiume,” anasema.

Anaongeza “Wengine wanaogopa kulala kwenye chandarua eti wakilala wanaona ni kama wapo kwenye jeneza au wengine wakivihusisha na imani za freemason, jambo ambalo halina uhusiano 
hata kidogo.

“Hakuna utafiti wowote uliowahi kufanyika kuthibitisha kwamba chandarua kinasababisha upungufu wa nguvu za kiume, kilichothibitishwa ni kwamba humpatia mtu usingizi mnono kwa sababu mbu huwa hawamfikii na kumsabishia usumbufu wa aina yoyote,” anabainisha.

Anasema vyandarua vinavyogawiwa kwa wananchi vimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na na Taasisi ya Usajili wa Viuatilifu katika Kanda za Joto (TPRI) kuwa ni salama.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha inalinda afya za wananchi wake na si kuwaangamiza,” anasisitiza.

Mtaalamu akipuliza dawa ukoko ndani ya nyumba (picha na mtandao)

Mkakati maalumu

“Wizara tumejipanga kufanya kampeni nyingine kubwa ya kusambaza vyandarua mapema mwakani katika mikoa yote 26 ili kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria,” anasema.

Anaongeza “Tumeshapokea fedha kutoka, Mfuko wa Dunia wa kukabiliana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu,  tutaanza na mikoa mikoa 11 ambako tutagawa vyandarua takriban milioni 15.

“Lengo letu ni kuhakikisha kila chandarua kimoja kinatumika na angalau watu wawili ndani ya familia, tunawasihi wananchi tutakapokuwa tunakwenda wawe tayari kuvipokea vyandarua hivyo na kuvitumia ili kwa pamoja tuweze kutokomeza malaria nchini,” anatoa rai.

Unayopaswa kufahamu

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea viitwavyo Plasmodia ambavyo hungia katika mfumo wa damu mwilini baada ya mtu kuumwa na mbu jike aitwaye Anopheles anayekuwa amebeba vimelea hivyo.

Wataalamu wa afya wanaeleza kwamba vimelea hivyo vinapoingia mwilini, vimelea hivyo huenda katika chembe za ini la binadamu na kuanza kuzaliana, wakati chembe za ini zinapopasuka, huruhusu vimelea hivyo ambavyo huenda kushambulia chembe nyekundu za damu yake.

Wanasema huko vimelea hivyo huzidi kuongezeka na wakati chembe nyekundu za damu zinapopasuka huruhusu vimelea ambavyo huenda hushambulia kwa wingi zaidi chembe nyekundu za damu.

Wanasema mzunguko wa chembe nyekundu za damu unapovamiwa na mipasuko hiyo huendelea hatimaye mtu huanza kuonesha dalili za malaria kila baada ya chembe hizo kupasuka.

Kwa mujibu wa wataalamu, mtu huuanza kuhisi homa, baridi, kutokwa jasho jingi, maumivu ya kichwa na mwili, kichefuchefu na hata kutapika, dalili hizo huanza kuonekana baada ya saa 48 hadi 72, 

ikitegemea aina ya vimelea na muda ambao mtu amekuwa na ugonjwa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2013 lilikadiria zaidi ya watu milioni 198, waliambukizwa malaria na kwamba watu 584,000 walifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

WHO ilieleza karibu watu wanne hadi watano waliofariki dunia ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ugonjwa huo unatishia mamia ya nchi na maeneo mbalimbali ulimwenguni kwani watu bilioni 3.2 wanakabili hatari ya kuambukizwa.

Jinsi ya kujikinga

Kwa kuhakikisha unatumia chandarua kilichowekwa dawa ya kuua mbu hao waenezao malaria, ambacho hakijatoboka na unapaswa kukichomeka vizuri kwenye godoro lako.

Ni vema ukapuliza dawa ya kuua wadudu ndani ya nyumba yako mara kwa mara kabla ya kulala na ikiwezekana weka wavu wa kuzuia wadudu katika madirisha na milango yako ili kudhibiti mbu kuingia ndani ya nyumba yako.

Vaa nguo zinazofunika vema mwili wako hasa nyakati za jioni na usiku ambapo mbu huzunguka zunguka na inapowezekana epuka kuwa katika maeneo yenye mbu wengi kwa mfano mabwawa, maji yaliyotuama au mahala ambapo mbu huzaliana.

Ikiwa umeanza kuona dalili za malaria wahi mapema hospitalini kupata matibabu haraka.

Makala haya kwa mara ya kwanza yalitoka Septemba 21, mwaka huu kwenye gazeti la MTANZANIA

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement