Picha kwa hisani ya mtandao
-Mapendekezo yao kuwezesha uandaaji mpango kazi wa Kitaifa, Afya kwa vijana
NA VERONICA ROMWALD –DAR ES SALAAM
MWILI wa binadamu wakati mwingine unaweza kuufananisha na
gari, mara nyingi gari linapoendeshwa
kwa muda barabarani huhitaji kufanyiwa matengenezo ya kina.
Ndiyo maana hupelekwa kwa mafundi (gereji) kwa ajili ya
matengenezo, kadhalika binadamu kuna wakati huugua na hivyo kuhitaji matibabu
dhidi ya ugonjwa unaomsumbua.
Huenda ama hospitali, zahanati au kituo chochote cha afya
ambako hukutana na wataalamu wanaoweza kumpatia matibabu sahihi dhidi ya
ugonjwa unaomsumbua.
Lakini si mara zote tunakwenda huko kwa matibabu pekee, wakati
mwingine huwa tunahitaji kwenda kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu
unaoweza kutusaidia kuishi vema ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa
mbalimbali.
Licha ya umuhimu huo, vijana wengi hawana mwamko wa kwenda
hospitalini, zahanati au vituo vya afya ama kupima afya zao au kupata ushauri.
Kwanini
Hivi karibuni MATUKIONAMAISHA
lilipata nafasi kuhudhuria Mkutano wa Kitaifa wa Vijana wa Afya na Maendeleo
uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere.
Mkutano huo ambao ni wa kwanza
kufanyika nchini uliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Save the
Children kwa kushirikiana na serikali.
Vijana wakimsikiliza kwa makini mwezeshaji wakati wa mkutano huo, picha kwa hisani ya mtandao wa Save the Children
Pamoja na mambo mengine, lengo
kuu lilikuwa kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili vijana hasa katika
sekta ya afya.
Ulihusisha washiriki zaidi ya
100 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambao walipata fursa ya kuchangia mawazo
yatakayosaidia baadae serikali kutengeneza mpango kazi wa afya kwa vijana
nchini.
Sabinius Paulo, mkazi wa
Iringa ni miongoni mwa vijana walioshiriki mkutano huo, anasema kuna vikwazo
vingi ambavyo vijana hukumbana navyo vinavyowakatisha tamaa kutafuta huduma
sahihi za matibabu na ushauri.
“Changamoto zaidi inakuja pale
kijana anapohitaji kupata taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi na ujinsia hakuna
huduma rafiki hali inayowakatisha tamaa vijana wengi,” anasema.
"Madawa ya kulevya yana madhara kiafya na hupunguza uwezo wa kufanya kazi." - Dr. Cassian
Anasema vijana wanaoathirika
zaidi na hali hiyo ni wale walioko katika maeneo ya vijijini kuliko wale
walioko katika maeneo ya mijini.
“Mijini kuna fursa nyingi
ambazo kijana anaweza kuzitumia kupata taarifa sahihi juu ya afya ya uzazi na
ujinsia, kule kijijini unaweza kukutana na kijana ambaye haelewi chochote kwa
mfano kuhusu huduma za uzazi wa mpango,” anasema.
Anasema lugha inayotumika pia
wakati mwingine huwa ni kikwazo kufikisha ujumbe unaokusudiwa kuwaelimisha
vijana walioko maeneo ya vijijini.
“Unaweza kukuta kipeperushi
kimeandikwa kwa lugha ama ya Kiswahili au ya kiingereza, kwa kule vijijini
inakuwa vizuri zaidi kutumia lugha zao ili kufikisha ujumbe kwa haraka zaidi,”
anabainisha.
Paulo anasema kutokana na idadi kubwa ya vijana kushindwa
kupata huduma rafiki za matibabu na taarifa sahihi juu ya afya ya uzazi
kumechangia ongezeko kubwa la ndoa na mimba za utotoni.
“Ni tatizo kubwa, vijana wanatamani kupata taarifa sahihi
lakini hawazipati kwa sababu hakuna huduma rafiki, nimefurahi kupata bahati
kuhudhuria mkutano huu na naamini kile nilichokiwasilisha serikali itakifanyia
kazi ili kukabiliana na hali hiyo,” anasema.
Changamoto
kwa walemavu
Dorice Charles (pichani) ni miongoni mwa vijana ambao hawapo tayari
kwenda hospitalini, zahanati wala kituo cha afya kilichothibitishwa kufuata
matibabu ya kibingwa.
Akisimulia, Dorive anasema “Sikuzaliwa na ulemavu wa aina
yoyote ile, mwaka 2004 nikiwa darasa la tatu niliugua homa kali sana nikatibiwa
kwa dozi ya quinine ambayo ilinisababishia ulemavu wa kusikia.
“Hali hiyo ilinilazimu kuacha masomo kwa muda mrefu,
nilirudi shuleni mwaka 2006 wanafunzi wenzangu wakawa wananitani nimekuwa
kiziwi, uwezo wangu darasani nao ulishuka kwa kiwango kikubwa,” anasimulia.
Anasema hata hivyo aliendelea kujifunza licha ya changamoto
nyingi alizokabiliana nazo hadi akafanikiwa kumaliza darasa la saba na
kuchaguliwa kujiunga Sekondari.
“Mazingira yalikuwa magumu kwangu, miundombinu haikuwa
rafiki, walimu hawakuwa na uwezo wa kufundisha lugha ya alama, nilipohitimu
kidato cha nne nilifaulu kwa alama D somo la Kiswahili peke yake,” anasema.
Dorice anaongeza “Kuna siku nilijihisi mgonjwa, nikaenda
hospitalini lakini daktari niliyemkuta alinibagua kwa kuwa mimi ni mlemavu,
masikio yangu hayana uwezo wa kusikia (kiziwi).
Anasema siku hiyo aliwahi mapema hospitalini hapo lakini
daktari aliyemkuta alimtaka akae kwenye benchi kwanza ili awatibu wagonjwa
wengine ambao walikuwa na uwezo wa kusikia.
“Nilikaa pale kwenye benchi kwa muda mrefu sana, mwisho
muda wa kazi ulikwisha, yule daktari akatoka na kuondoka zake, mimi nikiwa
nimebaki pale pale, nikahuzunika mno, nikarudi zangu nyumbani,” anasema.
Anasema tangu wakati huo hadi sasa hayupo tayari kwenda
huko kutibiwa badala yake kila anapojihisi kuwa ni mgonjwa huenda mwenyewe
kwenye duka la dawa na kununua ile anayoona inamfaa na kujitibu nyumbani.
Mlezi
Mwanzilishi wa Kituo Maalumu cha Kusaidia Watoto wenye
Ulemavu mkoani Mara, Mwalimu Wilfred Serikali (anayezungumza pichani) anasema watoto wenye ulemavu
wengi wanakosa huduma zile wanazostahili.
“Mara nyingi jamii inawaacha peke yao, hawapewi taarifa
sahihi juu ya ukuaji wa miili yao na elimu ya afya ya uzazi kwa ujumla ili
wajitambue, wengi wamejikuta wakiishia katika mikono ya watu wasio na ni njema.
“Unakuta tayari mtoto ni mjamzito na ukimuhoji utagundua
hana taarifa yoyote kuhusu afya ya uzazi na ujinsia, wazazi au walezi
hawawaelezi ukweli watoto wao jambo ambalo linahatarisha afya na maendeleo
yao,” anabainisha.
Kundi
muhimu
RIPOTI iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) ya mwaka 2014 inaonesha idadi ya vijana
inakadiriwa kuwa watu bilioni 1.8 kati
ya watu bilioni 7.5 duniani.
Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012
iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha idadi ya vijana
inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 16.2 kati ya watu milioni 44 nchini.
Hii inaonesha wazi kwamba kundi la vijana ndilo lenye idadi
kubwa ya watu si Tanzania pekee bali duniani kote.
Vijana ni nguvu kazi ya Taifa lolote linalohitaji kupata
maendeleo na ili itumike vema katika shughuli za maendeleo ni lazima wawe na
afya njema.
Vijana wakiendelea kujadili
Ni haki ya kila raia pia (si vijana tu) kuwa na afya njema
kwani hapo mtu huweza kuutumia muda wake ipasavyo katika shughuli za kiuchumi
kwa faida yake, familia yake na Taifa kwa ujumla.
Ndiyo maana katika ajenda ya maendeleo endelevu ya
millennia (SDGs) lengo namba tatu kati ya malengo 17 yaliyopitishwa na Umoja wa
Mataifa (UN), linasisitiza juu ya kuhakikisha afya bora na kukuza maisha bora kwa
watu wote na wa rika zote.
Mwakilishi
wa YUNA
Mwakilishi wa Asasi za Vijana wa Umoja wa Mataifa
(YUNA-Tanzania), Rahim Nasser (pichani) anasema vijana wana nafasi kubwa ya kushiriki
katika kutekeleza malengo endelevu ya millennia (SDGs).
“Tunajitambua, tunafahamu tunachohitaji, dunia ipo katika
mikono salama ya vijana, tukipewa nafasi, tunashukuru Save the Children
wametuweka pamoja, tumechagua na kujadili kwa kina lengo namba tatu.
“Kimsingi, vijana tunahitaji kupata taarifa sahihi kuhusu
afya, kwa maendeleo yetu, Taifa na dunia kwa ujumla,” anasema.
Maandalizi
ya mpango
Mkurugenzi wa uhamasishaji na habari wa Tume ya Kudhibiti
Ukimwi, (TACAIDS), Jumanne Isango anasema kwa muda mrefu kumekuwa na pengo kubwa katika kuwahusisha vijana kwenye shughuli
ambazo zinawalenga wao moja kwa moja.
“Hasa katika suala la afya na maendeleo, mara nyingi
ushiriki wao umekuwa hautoshelezi, ndiyo maana tuliona vema tuwalete pamoja
wawakilishi kutoka mikoa yote ili tujadili na kupata mapendekezo kutoka kwao,”
anasema.
Anasema mapendekezo yaliyotolewa na vijana hao yataiwezesha
serikali kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa vijana utakaojumuisha masuala yote
yahusuyo afya.
“Kwa mfano kuhusu afya ya uzazi, elimu juu ya ugonjwa wa
Ukimwi, uzazi wa mpango kwa vijana na masuala mengine mengi. Tunakwenda
kuyapitia mapendekezo haya na tunakusudia baada ya mwezi mmoja hadi miwili tuwe
tumekamilisha kazi hiyo,” anabainisha.
Isango anaongeza “Vijana wamewasilisha mapendekezo mengi
mazuri kwa mustakabali wa Taifa letu, tunazungumza kuhusu malengo endelevu ya
dunia (SDG’s) ambayo yanasisitiza upatikanaji wa maji safi, elimu, afya na haki
nyinginezo za msingi.
“Hivyo kwa kuandaa mpango huo utatusaidia kujipima kila
mwaka kwa kufanya tathmini wapi tulipotoka, tulipo na tunakwenda kufikia
malengo hayo,” anafafanua.
Kauli
ya serikali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista
Mhagama (pichani) anasema serikali inatambua umuhimu wa kundi la vijana.
“Ipo wazi kwamba kundi hili
ndilo lenye idadi kubwa ya watu nchini kuliko makundi mengine, tunazungumzia
kuelekea uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda tunahitaji nguvu kazi hii
tuitumie ipasavyo.
“Lakini ni lazima wawe na afya
imara, tunajivunia kwamba vijana wengi wana ujuzi wa kutosha ingawa wengi
walijifunza katika mfumo usio rasmi lakini tumeanza jitihada za kuwarasimisha
shughuli zao ili tuwatambue,” anasema.
Anasema tayari serikali
imeingia makubaliano na Chuo cha Mafunzo
na Ufundi Stadi (VETA) kuwapa ujuzi rasmi na kisha kuwarasimisha vijana wenye
ujuzi ambao waliupata katika mfumo usio rasmi.
Anaongeza “Serikali ipo tayari
kuwasikiliza vijana, tupo tayari kupokea mawazo yao wakati wowote ili kwa
pamoja tuweze kufikia lengo namba tatu la malengo endelevu ya millennia.
Anasisitiza kwamba ndiyo maana ilipitisha sheria namba 12
ya mwaka 2015 juu ya uanzishwaji wa Mabaraza ya vijana ili washiriki katika
kutoa maoni yao moja kwa moja kwa serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.
“Tayari tumekamilisha uandaaji wa kanuni kwa ajili ya
uanzishwaji wa baraza, lengo ni kuwaunganisha vijana na kuwaleta pamoja na
serikali yao kwa malengo yao na Taifa kwa ujumla,” anabainisha.
Chapisha Maoni