Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ameziagiza hospitali zote zilizopo chini ya serikali zikiwamo za
Kanda, za Mikoa, Wilaya, zahanati na vituo vya afya kote nchini kuhakikisha
zinatenga siku maalumu kwa ajili ya kufanya upimaji wa saratani ya matiti na
kizazi.
Agizo hilo amelitoa Dar es Salaam leo wakati alipozungumza wakati
alipokuwa akifunga matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa
saratani ya matiti na saratani ya shingo ya mlango wa kizazi katika viwanja vya
Taasisi ya saratani Ocean Road (ORCI).
Waziri Ummy amesema tatizo la saratani linazidi
kuongezeka ambapo kila mwaka takriban wagonjwa wapya 50,000 hugundulika.
"Inakadiriwa ifikapo 2020 idadi ya wagonjwa wa
saratani itaongezeka mara mbili ya wagonjwa wapya na kufikia wagonjwa
100,000 ikiwa hatua hazitachukuliwa, "amesema.
Amesema hali inaonesha wagonjwa wanaofika hospitalini kwa
uchunguzi ni asilimia 26 pekee na kwamba katika
wagonjwa 100 wagonjwa 74 hawajulikani wanapopata tiba na uchunguzi huku asilimia
80 ya wagonjwa hufika wakiwa katika hatua za mwisho na kusababisa matibabu
kutokuwa mazuri.
Amesema serikali imeongeza kiwango cha upatikanaji
wa dawa katika taasisi hiyo mara nne zaidi ya ilivyokuwa awali.
"Awali upatikanaji wa dawa ulikuwa kiwango cha
asilimia nne tu kwa sababu bajeti iliyokuwa ikitengwa ilikuwa ndogo walikuwa
wanapokea Sh milioni 790 lakini tumeiongeza hadi Sh bilioni saba.
Amesema serikali imekusudia kabla ya Juni 30, 2018
kununua kipimo cha kisasa cha uchunguzi wa magonjwa ya saratani cha PET/CT
Scan.
"Tumetenga Sh bilioni 14.5 kwa ajili ya
ununuzi wa kifaa hicho tutakapofunga Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika
Mashariki na Kati," amesema.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius
Mwaiselage amehimiza jamii kuwa na utamaduni wa kufanya upimaji mara kwa mara
kwani saratani ikigundulika mapema hutibika na kupona kabisa.
"Asilimia 80 ya wagonjwa wanaofika hospitalini
huwa wamechelewa, ili kuwasaidia zaidi wagonjwa tunaowapokea, kupitia matembezi
tuliyofanya miaka ya nyuma tumeweza kuboresha wodi za saratani na tumeongeza
idadi ya vitanda kutoka 40 hadi 100 katika chumba cha chemotherapy, hatua hii
imesaidia wagonjwa kupata huduma kwa wakati na kwa muda mfupi," amesema.
Chapisha Maoni