Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

SERIKALI imewatoa hofu wanawake nchini juu ya uvumi wa kuwapo kwa sidiria zinazodaiwa kupandikizwa majimaji yanayosababisha saratani ya matiti.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mratibu Program ya Saratani ya Via vya Uzazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Safina Yuna alipozungumza na MTANZANIA Jumamosi katika mahojiano maalum.

Mahojiano hayo yalilenga kujua hatua mbalimbali ambazo serikali inazichukua kukabili ugonjwa huo ambao unaonekana kusababisha vifo vya wanawake wengi baada ya saratani ya kizazi na ngozi.

Akizungumza, Dk Yuna alisema hadi sasa hakuna utafiti wowote ambao umewahi kufanyika popote kuthibitisha ukweli juu ya madai hayo.

“Ni dhana potofu, jamii isiwe na hofu… kitaalamu haijagundulika nini hasa kisababishi cha saratani hii lakini kuna (risk factors) tabia hatarishi ambazo zinatajwa kuwa zinaweza kuwa kichocheo cha kumsababishia mtu kupata saratani ya matiti.

“Kwa mfano wapo ambao wanaweza kupata kwa kurithi 
yaani ikiwa kuna mtu kwenye familia au ukoo aliwahi kuwa na ugonjwa huo wapo ambao wanaweza kuja kurithi hapo baadae,” alisema.

Aliongeza “Unywaji pombe, uvutaji sigara na kitendo cha mwanamke kuchelewa kuzaa na kutonyonyesha mtoto huweza kumuweka kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu.

Alisema kwa mujibu wa takwimu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), kila mwaka tunapokea wagonjwa wapya 50,000 kati ya hao asilimia 12 huwa wanagundulika kuwa na saratani ya matiti.

“Kati ya asilimia 12 ambao hugundulika asilimia 9.7 hufariki dunia, asilimia 99 ya wanaopata saratani hii ni wanawake, wanaume huwa asilimia moja tu,” alibainisha.

Alisema hali inaonesha wagonjwa wengi hufika katika taasisi hiyo wakati ambapo ugonjwa huwa umefika katika hatua mbaya.

“Huwa unapitia hatua nne, ndiyo maana mwezi Oktoba ulipitishwa kuwa mwezi wa uhamasishaji… kuhamasisha jamii kuwahi mapema hospitalini kufanyiwa uchunguzi,” alisema.

Alisema mara nyingi dalili huwa ziwa kuongezeka ukumbwa, kubadilika rangi kuwa kama ya rangi ya chungwa, kupata uvimbe (fundo) mgumu, chuchu kutoa majibu yasiyo ya kawaida.

“Mara nyingi huwa na rangi nyekundu au usaha mzito, unaweza kupata maumivu kwenye ziwa au kwenye chuchu ukiona dalili hizo maana yake tayari una saratani, kwa hiyo unapaswa uwahi tufanye uchunguzi tujue imefika hatua gani.

“Lakini hatupendi ifike huko ni vema kujitokeza mapema kufanya uchunguzi kabla hata ya kuona dalili hizo kwani huwa tayari umepata saratani,” alifafanua.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement