Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Koo, Pua na Sikio wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Edwin Liyombo akiwaonesha waandishi wa habari kifaa cha coclea implant ambacho hupandikizwa kwa watoto waliozaliwa na tatizo la usikivu (picha na Veronica Romwald).
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)
inatarajia kufanya upasuaji wa awamu ya pili, kupandikiza vifaa vya usikivu kwa
watoto waliozaliwa na tatizo la kutokusikia (ukiziwi).
Akizungumza na mtandao huu, mwishoni mwa wiki Ofisa
Uhusiano wa hospitali hiyo, Neema Mwangomo alisema tayari watoto sita
wameandaliwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huo.
Mwangomo (pichani) alisema upasuaji huo utafanywa na
wataalamu wa Muhimbili kwa kushirikiana na wataalamu wenzao kutoka kampuni ya
MEDEL ya nchini Austria.
“Tunatarajia upasuaji huo utafanyika
Novemba, mwaka huu...hatua hii ni muendelezo Wa jitihada tunazofanya za kutoa
huduma za kibingwa na kupunguza rufaa kwa wagonjwa wanaotakiwa kwenda kutibiwa
nje ya nchi,” alisema.
Mwangomo alisema gharama za upasuaji
kwa kila mtoto anayehitaji kuwekewa kifaa cha usikivu ni milioni 36 pekee
hospitalini hapo.
“Wakati akipelekwa nje ya nchi kwa
matibabu huwa inagharimu takriban Sh milioni 80 hadi Sh milioni 100 kwa mtoto
mmoja,” alisema.
Aliongeza “Kwa hiyo kuwapo kwa
huduma hii hapa Muhimbili inasaidia kupatikana kwa gharama nafuu zaidi na hivyo
kuwezesha watoto wengi kupatiwa huduma hiyo ya matibabu.
Kifaa cha cochlea implant
Alisema hatua hiyo itachochea pia
kuwapo kwa mawasiliano kwa watoto na wazazi wao na kupata elimu anayohitaji
hivyo kupunguza mzigo kwa familia na jamii kwa ujumla.
“Huduma hii ilizinduliwa Juni 7,
mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu, kwa hatua hiyo Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hiyo
katika hospitali za umma na ya pili katika Ukanda wa Afrika Mashariki
ikitanguliwa na Kenya,” alisema.
Chapisha Maoni