Jicho la binadamu (picha na mtandao)
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
OKTOBA 12, kila mwaka huwa ni Siku ya Macho
Duniani, Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hiyo
ambayo kwa mwaka huu ilipewa kauli mbiu isemayo ‘Afya ya Macho kwa Wote,
Thamini Uoni wa Jicho’.
Lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kuhamasisha jitihada
za kutokomeza upofu unaozuilika duniani. Maamuzi ya kuadhimisha siku hiyo yalifikiwa
na Lions Club International Foundation mnamo mwaka 1998.
Baadae yaliungwa mkono na wadau wengine likiwamo Shirika
la Afya Duniani (WHO), Muungano wa Mashirika ya Kimataifa yanayojihusisha na Huduma
za Macho (IAPB), Serikali za nchi mbalimbali, wataalamu wa afya na watu
binafsi.
Ni maadhimisho mahususi lengo likiwa kuhamasisha
utekelezaji wa Dira ya Kimataifa ya Kutokomeza Upofu unaozuilikaDuniani ifikapo
mwaka 2020 kwa kuthamini haki ya kuona kwa wote.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu anasema Serikali ya Tanzania iliridhia na kuungana na
Mataifa mengine duniani katika kutekeleza azimio hilo mnamo Mei 23, 2003.
Anasema inakadiriwa takriban watu milioni 285
duniani wana matatizo ya kutokuona na kwamba kuna ongezeko kubwa la matatizo ya
kutokuona duniani ambayo asilimia 80 ya hayo yangeweza kuzuilika.
Daktari
Asha Mweke ni Mtaalam wa Macho (Optometria) katika Taasisi
ya Letasi Eye and Optical Center iliyopo jijini hapa, anasema ni kweli kwamba
matatizo ya macho yanaweza kuzilika iwapo watu wajajenga utamaduni wa kupima
mara kwa mara.
“Tatizo tunaona kuna changamoto, wengi hawana
mwamko wa kujitokeza mapema kufanya uchunguzi wa afya ya macho, kutokana na
hali hiyo wengi huja hospitalini wakati tatizo likiwa limeshakuwa kubwa,
wamechelewa,” anabainisha.
Kundi
la wanafunzi
Mweke anasema kundi la wanafunzi ndilo ambalo
linaonekana kuathiriwa zaidi ya hali hiyo huku akitolea mfano namna walivyoweza
kuwabaini wengi baada ya kufanya upimaji bila malipo katika kituo chao.
“Tuliwaalika kituoni kwetu hivi karibuni wakati
shule zilipokuwa zimefungwa na tukawafanyia uchunguzi bila malipo, tuliwapima
wanafunzi 120 kati ya hao 90 tuliwakuta na matatizo mbalimbali hasa ya uoni
hafifu,” anabainisha.
Anaongeza “Wengi hawakuwa wanajitambua wana
matatizo ya macho, kila tuliyemuhoji alisema alijua kule kuwasha washa, wekundu
kwenye macho na au kutoka tongo tongo ni hali ya kawaida, si kweli.
“Zile ni ishara au dalili zinazokuonesha kwamba
macho yako yana tatizo kwa hiyo unapoona ishara yoyote kati ya hizo ni muhimu
ukawahi hospitalini na kuwasiliana na mtaalamu wa macho ili ufanyiwe uchunguzi
mapema,” anasema.
Undani
wa tatizo
Mtaalamu huyo anasema kitaalamu tatizo la uoni
hafifu limegawanyika katika aina kuu tatu.
“Kuna ambao wanasumbuliwa na tatizo la uono hafifu wanapokaa
kwa karibu, wapo wenye uono hafifu pindi wanapokaa kwa mbali na kuna ambao wana
huoni hafifu wa kutokuona pindi wanapokaa mbali na hata karibu,” anabainisha.
Mtaalamu wa Macho (Optometria) wa Taasisi ya Letasi Eye and Optical Center, Asha Mweke, akimuelekeza kusoma herufi katika karatasi maalumu mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Bunju A hivi karibuni wakati taasisi hiyo ilipofanya upimaji wa afya ya macho shuleni hapo.
Anaongeza “Lakini tatizo hili linatibika na mara
nyingi ni kwa kuvaa miwani, kwa wale ambao wamechelewa kupata tiba.
Anasema watu wenye tatizo la uoni hafifu kwa karibu
mara nyingi huwa wanapata maumivu makali ya kichwa na wengi hulalamika
wanapopita kwenye eneo lenye mwanga hudai unawaumiza.
“Kutokana na hali hiyo utaona mtu mwenye tatizo
anapofika kwenye mwanga mkali anakuwa anafinya macho yake kwa sababu huhisi
maumivu makali,” anabainisha.
Lishe
ni tiba mbadala
Anasema pamoja na matibabu wanayotoa ikiwamo
kutumia miwani kutibu tatizo lakini tatizo hilo pia linaweza kutibika ikiwa mtu
atapata lishe bora.
“Wapo wanafunzi ambao wanakuja hospitalini kwetu
wakilalamika macho yao yanauma, lakini tunapowafanyia vipimo tunakuta hawana
tatizo lolote, kumbe hali hiyo inawapata kutokana na kukosa lishe bora,”
anasema.
Wengi
wanapenda maharagwe
Mtaalamu huyo anasema kwa kawaida watoto wengi
hupendelea kula mboga ya maharagwe ambayo kimsingi ina protin kwa wingi.
“Maharagwe si mboga mbaya, ni nzuri kwani ina
protin kwa wingi ambayo huhitajika mwilini lakini tunahamasisha waanze kupenda
kula mboga mboga (za majani) zile zina virutubishi vingi vya Vitamin A ambavyo
ni muhimu kwani husaidia kulinda afya ya macho,” anabainisha.
Anaongeza “Mwili unapokosa virutubisho vya vitamin
A mtu huwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la uoni hafifu na matokeo
yake hujikuta akipata upofu katika maisha yake hapo baadae.
Uoni
hafifu na ufaulu duni
Juma Faustine ni mwanafunzi wa darasa la pili
katika Shule ya Msingi Bunju A anasema kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na
tatizo la macho.
“Huwa nikikaa mbali na ubaoni siwezi kuona vizuri, nilimueleza
mwalimu wangu juu ya jambo hilo akanihamishia katika dawati la mbele lakini
hata hivyo bado siwezi kuona sawa sawa,” anabainisha.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Diana Felix
anasema tatizo la uoni hafifu huchangia kwa namna moja au nyingine kushusha
kiwango cha ufaulu kwa mwanafunzi husika.
"Kwa mfano mwaka jana jumla ya wanafunzi 400
waliandikishwa kuanza darasa la kwanza, ambao tumewagawa katika madarasa manne
kila moja likichukua takriban wanafunzi 90,” anasema.
Anasema katika hali ya kawaida ikiwa mtoto
anakabiliwa na tatizo la uoni hafifu halafu akakaa umbali mrefu kutoka usawa wa
ubao ni dhahiri hataweza kuona kile ambacho mwalimu ameandika ubaoni.
“Changamoto ni kwamba si wote ambao husema, wengi
huwa waoga hivyo huamua kunakili kwa wenzao, sasa ikiwa mwenzake hajanakili
vizuri ubaoni maana yake ni kwamba wananakili makosa ya wenzao,” anabainisha.
“Pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi kwani inakuwa
vigumu mwalimu kumfikia kila mmoja na kujua iwapo ana tatizo au la,” anasema.
Ushiriki
wa wazazi kikwazo
Mwalimu huyo anasema changamoto nyingine ni
ushirikiano mdogo wa wazazi.
Anaongeza “Wengi ni wazito katika kufuatilia
maendeleo ya mtoto, hatuwaoni kuja kuuliza maendeleo ya watoto wao na hata
inapotokea mtoto mmebaini ana tatizo tunapowaita huwa hawaji, inakuwa inatupa
wakati mgumu mno.
“Hapa kuna watoto wanaishi na virusi vya Ukimwi
lakini wazazi hawapo wazi, hata kutudokeza walimu wakuu, wazazi wanasema tu
mtoto anaumwa lakini hasemi anaumwa nini lakini walimu tunaelewa tunapowaangalia
tunajua watoto wana matatizo.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Diana Felix
“Kwenye suala la afya ni changamoto nyingine, mtoto
unamuona ana afya duni, labda analalamika ana maumivu ya kichwa hata wiki nzima
lakini anakuja na kukueleza amepatiwa dawa ya kutuliza maumivu basi,
hakupelekwa hospitalini kuchunguzwa afya yake, kwa kweli ushirikiano ni mdogo
mno,” anasema.
Anasema hiyo inachangia kushusha kiwango cha
maendeleo mazuri ya mwanafunzi.
“Yupo mwanafunzi hapa (anamtaja) afya yake si nzuri
kwa sasa hata shule hawezi kuja, wenzake walienda kumtembelea hivi karibuni,
anasema ameenda hospitalini amepewa dawa ambazo anazitumia lakini hata yeye
mwenyewe hajui ni za nini zaidi ya mama yake,” anabainisha.
Mwalimu huyo anaishukuru taasisi hiyo kwa kufanya
upimaji bila malipo shuleni hapo kwani itasaidia kuwatambua wanafunzi wenye
matatizo na hivyo kupata matibabu mapema.
“Wamewafanyia upimaji wanafunzi 1,350 wa darasa la
kwanza, pili na tatu, kabla ya upimaji huu tuliwashirikisha wazazi, kwa hiyo
wale ambao watakutwa na tatizo pia tutawashirikisha wazazi ili waendelee
kufuatilia matibabu ya watoto wao,” anasema.
Hali
halisi
Waziri Ummy (Pichani) anasema idadi kubwa ya watu wenye
matatizo ya kutokuona asilimia 90 wanaishi katika nchi zinazoendelea.
Anasema asilimia 65 ya watu wasioona ni wale wenye
umri wa zaidi ya miaka 50 na kwamba kundi hilo linachangia asilimia 20 ya watu
wote duniani.
“Ongezeko la watu wenye umri mkubwa katika nchi nyingi
kunamaanisha ongezeko la watu watakaokuwa hatarini kupoteza uwezo wao wa kuona
kutokana na matatizo ya macho,” anasema.
Anaongeza “Watoto milioni 19 duniani wanakabiliwa
na matatizo hayo na kulingana na makadirio ya takwimu za WHO takriban
watanzania 573,000 hawaoni kabisa.
“Kwa ujumla watu wote wenye matatizo ya kuona kwa
viwango mbalimbali nchini wanakadiriwa kuwa mara tatu ya watu wasioona ambao ni
takriban watu milioni 1,73,000,” anabainisha.
Chapisha Maoni