Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
NOVEMBA 12, mwaka huu Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani
kuadhimisha Siku ya Nimonia Duniani.
Nimonia ni miongoni mwa magonjwa yanayotajwa kuchangia idadi kubwa
ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Unatajwa kuwa ugonjwa hatari unaoathiri mapafu ya binadamu
ukishambulia watu wa rika zote (watoto na wakubwa).
Hata hivyo, tafiti zinaonesha watoto ndiyo ambao wapo kwenye
hatari zaidi ya kupoteza maisha kuliko watu wazima.
Kaimu Meneja Program ya Afya ya Mtoto wa Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Felix Bundara anasema hiyo ni kwa sababu
kiwango chao cha kinga ya mwili kupambana na magonjwa mbalimbali huwa si kingi
kama ilivyo kwa watu wazima.
“Miili ya watoto huwa bado haina kinga ya kutosha kupambana na
magonjwa mbalimbali ukiwamo nimonia na ndiyo maana anapougua ikiwa hajapatiwa
matibabu sahihi ni rahisi kupoteza maisha,” anabainisha.
Anasema mtu hupata ugonjwa huo kutokana na maambukizi ya wadudu
(bacteria), fangasi au virusi.
Hali ilivyo
Dk. Bundara anasema tafiti zinaonesha ugonjwa huo ni tishio si tu
Tanzania bali duniani kote ukichangia idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga.
Anaongeza “Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania
wa mwaka 2015/16 (TDHS) unaonesha kati ya vifo 100 vya watoto wachanga
vinavyotokea nchini vifo 15 kati yake huwa vimetokana na ugonjwa huu wa
nimonia.
Anaongeza “Tafiti zinaonesha pia ugonjwa huo unashika nafasi ya
pili nchini kati ya magonjwa yanayosababisha idadi kubwa ya vifo vya watoto
wachanga.
Changamoto
Dk. Bundara anasema kwa mujibu wa utafiti huo wa TDS unaonesha wazazi na walezi wengi huwa hawawepeleki watoto wao hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa mapema pindi wanapopata kikohozi.
“Hali hiyo watoto kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha ikiwa
wanasumbuliwa na nimonia na wakakosa matibabu sahihi mapema,” anasema.
Anasema utafiti huo unaonesha kati ya watoto 100 waliopata kikohozi
wakati wa kipindi hicho, watoto 55 pekee ndiyo ambao walifikishwa hospitalini
kwa matibabu.
“Watoto 45 haijulikani wanaishia wapi, sasa hii ni changamoto
kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huu, jamii inapaswa kuamka na kuhakikisha
mtoto anapopata tatizo la kikohozi anafikishwa mapema hospitalini kwa
uchunguzi,” anasisitiza.
Anaongeza “Wapo pia wazazi na walezi ambao wamejenga utamaduni wa
kwenda wenyewe katika maduka ya dawa na kununua dawa za ‘antibiotics’ madukani
na kuwapatia watoto wanapopata kikohozi,” anasema.
“Si jambo sahihi, wajue kwamba si kila kikohozi ni nimonia kitendo
cha kuwapatia dawa bila ushauri wa daktari kunaweza kusababisha kutengeneza
usugu wa dawa mwilini,” anasisitiza.
Dalili
Daktari huyo anasema dalili kuu ya kwanza huwa ni kukohoa au
kupumua kwa shida au vyote viwili kwa pamoja.
“Yaani unakuta anakohoa au anapumua kwa shida, lakini nisisitize
si kila kikohozi ni nimonia, inahitaji uchunguzi wa kina ili uweze kujua kwamba
ni nimonia au la kwa sababu kuna matibabu yake yanatofautiana,” anasema.
Anafafanua “Kuna mtoto anaweza kuletwa hospitalini akiwa na tatizo
la kikohozi akichunguzwa kasi yake ya upumuaji daktari anakuta haijaongezeka na
ipo kawaida kabisa.
“Hivyo, matibabu ya mtoto wa aina hii huwa hapewi ‘antibiotics’
badala yake anapewa ‘vitulizo salama’ na kama ananyonya basi anaendelea
kunyonya maziwa ya mama yake kama kawaida.
“Hata ikiwa ameanza kula vyakula mbalimbali ataendelea kula kama
kawaida lakini atalazimika kupatiwa chai ya asali na limao kwa maelekezo maalum
ya daktari ili kutibu tatizo lake,” anabainisha.
Anaongeza “Mtoto mwingine anaweza kuletwa hospitalini na
akagundulika ana nimonia lakini si ile kali, huyu unakuta ana-kohoa na kasi
yake ya upumuaji imeongezeka.
“Lakini hii huwa inatofautiana pia, watoto wenye umri wa mwaka
sifuri hadi miezi miwili kwa kawaida ukihesabu kasi yao ya upumuaji haitakiwi
iwe 60 au zaidi, ikiwa tofauti na hapo na anakohoa daktari anajua hiyo ni
nimonia.
“Kwa watoto wenye umri wa miezi miwili hadi miezi 12 kasi yake ya
kupumua haitakiwi kuwa 50 au zaidi ukikuta ni tofauti na kiwango hicho na
anakohoa tunasema hiyo ni nimonia.
“Watoto wa miezi 12 hadi miezi 59 kasi yao ya upumuaji haitakiwi
kuwa 40 au zaidi ikiwa tofauti na kiwango hicho tunajua hiyo ni nimonia,”
anabainisha.
Daktari huyo anasema ikiwa kasi ya upumuaji imezidi viwango hivyo
moja kwa moja wanajua hiyo ni nimonia kwamba matibabu yake kwa kawaida huwa ni
kumpatia mgonjwa vidonge vya amoxilline kwa maelekezo maalum ya daktari.
“Lakini unaweza kupokea mtoto ambaye ana-kohoa na kasi yake ya
upumuaji imeongezeka kuliko kawaida, aidha, unakuta ana historia ya kutapika,
degedege, amelegea mno mwili wake au amepoteza fahamu basi moja kwa moja
tunajua hiyo ni nimonia kali,” anasema.
Dk. Bundara anasema mgonjwa mwenye dalili hizo anapaswa kuwahishwa
hospitalini ili apatiwe matibabu sahihi kuokoa maisha yake.
“Sambamba na dalili hizo, unaweza kukuta pia anapata shida ya
kubanwa kifua au katika sehemu ya chini ya kifua unakuta inaingia kwa ndani
pindi anapopumua na anapopumua unakuta anatoa sauti fulani, hizo pia ni dalili
ya nimonia kali,” anabainisha.
Mazingira hatarishi
Daktari huyo anasema wapo watu ambao huamini kwamba kitendo cha
mtu kuishi katika maeneo yenye baridi kali moja kwa moja humuweka kwenye hatari
ya kupata ugonjwa huo lakini si kweli.
“ Ingawa kuna baadhi ya tafiti (sayansi) ambazo inaonesha
mazingira ya baridi ni hatarishi kwani wale wadudu wanaweza kuzaliana kwa wingi
lakini si sababu ya msingi mno kwamba watu wanaoishi katika maeneo hayo
huathirika zaidi kuliko maeneo mengine,” anasema.
Anaongeza “Watoto wakiwekwa kwenye mazingira ya moshi, yaani unakuta
watu wanapikia ndani na kuna moshi labda unaotokana na kuni, mkaa au sigara,
moja kwa moja mtoto huwa kwenye hatari ya kupata tatizo hili.
“Lishe ni jambo la muhimu pia katika kumkinda mtoto kupata tatizo
hili hasa inayotokana na maziwa ya mama humuepusha mtoto dhidi ya ugonjwa huu,”
anabainisha.
Mafanikio ya chanjo
Anasema pamoja na changamoto iliyopo kwa baadhi ya wazazi na
walezi kutowafikisha watoto wao mapema hospitalini kupatiwa matibabu, hata
hivyo serikali imeendelea kujitahidi kuwapatia chanjo wale wanaofikishwa
hospitalini kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo.
“Matokeo ya Utafiti wa ‘Global Action Plan for Nimonia’ uliotolewa
mapema mwaka huu ambapo takriban nchi 20 tulifanyiwa ufuatiliaji, Tanzania
imeongoza kwa asilimia 90 katika utoaji chanjo dhidi ya nimonia,” anabainisha.
Anasema huduma hiyo inatolewa nchi nzima hasa katika vituo vyote
vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.
“Lakini pamoja na matokeo haya yaliyoonesha mafanikio bado
tunahitaji kuihamasisha jamii kuhakikisha watoto wanafikishwa mapema
hospitalini lengo letu tufikie kiwango cha asilimia 100.
“Ni muhimu mtoto afanyiwe uchunguzi, nasisitiza kwamba si kila
kikohozi ni nimonia inahitaji uchunguzi kujua kwa sababu matibabu yake
yanatofautiana na ikiwa atapatiwa dawa kiholela ni hatari zaidi,” anasema.
Makala haya kwa mara ya kwanza yamechapishwa Novemba 30, 2017 katika gazeti
la MTANZANIA
Chapisha Maoni