Na Veronica Romwald, aliyekuwa Kenya
TAFITI
za kina kubainisha kiwango cha athari za kiafya kwa bidhaa zitokanazo
na tumbaku bado zinahitajika kufanyika Barani Afrika ili kuielimisha
jamii na kuzihamasisha serikali kuanza kuchukua hatua, imeelezwa.
Hayo
yalielezwa juzi nchini Kenya na Mwanzilishi na Rais wa Shirika lisilo
la Kiserikali la Leadership Impact Dynamics, Ade Adeyami alipowasilisha
mada kwenye warsha maalum kwa waandishi wa habari hasa wajibu wao katika
kuwezesha nchi kufikia lengo namba tatu la Malengo Endelevu ya Dunia
(SDGs).
“Matokeo ya
utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya mwaka 2010
na 2011 vijana wa umri wa kati ya miaka 13 hadi 15 Barani Afrika
walionekana kuwa wameanza kutumia bidhaa hizo,” alisema.
Alisema
pamoja na utafiti huo bado kuna haja ya kufanya nyingine nyingi
zitakazosaidia kwa namna moja au nyingine kuokoa kizazi cha Afrika.
“Kama
hali ilikuwa hivyo unaweza kutafakari tupo wapi sasa na tunaelekea
wapi, jamii inahitaji kupatiwa elimu ya kutosha kuhusu athari zitokanazo
na matumizi ya bidhaa hizo, kwa hali ilivyo sasa.
“Ikiwa
juhudi hazitachukuliwa basi itakuwa vigumu kufikia lengo namba tatu la
Malengo ya Maendeleo Endelevu Duniani (SDGs) ambalo linahimiza afya bora
kwa wote,” alisema.
Alisema
takwimu zinaonesha kiwango cha matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku
duniani ni kikubwa kulinganisha na mabara mengine.
“Inakadiriwa
kufikia mwaka 2025 kutakuwa na watumiaji wa bidhaa zitokanazo na
tumbaku kufikia bilioni moja,” alibainisha Adeyemi.
Akizungumza,
Magesha Ngwiri alisema takwimu zinaonesha bara hilo kiwango cha
matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku kwa sasa kipo kwa asilimia 80.
“Takwimu
za WHO zinaonesha kila mwaka watu milioni saba hufariki dunia kutokana
na matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku na idadi hiyo inakadiriwa
kuwa itaongezeka mara dufu,” alisema.
Naye Mhadhili na Mwanachama wa Kudumu wa Taasisi ya Biashara ya Gordon, Chuo Kikuu cha Pretoria,
Dk.
Tendai Kadenhe Mhizha, alisema kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa
(UN) zilizotolewa mwaka 2012 zinaonesha vilitokea takriban vifo milioni
38 duniani.
“Asilimia 68
ya vifo hivyo vilitokana na magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza, unaweza
kwa mantiki hiyo ni muhimu wanahabari kujikita zaidi kuelimisha jamii
juu ya athari ili kushawishi serikali pia kuweza kuchukua hatua
kukabiliana na jambo hili,” alisisitiza.
Warsha
hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya Oxegene imefanyika Novemba 22, mwaka
huu nchini humo ambapo waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali
wameshiriki na kujadiliana.
Nchi
hizo ni pamoja na Tanzania, Kenya, Malawi, Zimbambwe, Uganda, Rwanda,
Zambia, Botswana, Swaziland, Lesotho, Ethiopia, Mozambique na Afrika
Kusini.
Chapisha Maoni