TAREHE 13- 19 NOVEMBA, 2017
- Wiki
hii Dunia inaadhimisha wiki ya kupambana na Tatizo la Usugu wa Vimelea kwa
Dawa za Antibiotiki (Antibiotics Resistance Awareness Week). Kauli mbiu ya
mwaka huu wa wiki ya uhamasishaji kuhusu antibiotiki duniani unasema: “Fuata ushauri wa wataalam wa afya kabla
ya kutumia antimicrobials”
- Dawa
za Antibiotiki ni dawa ambazo zipo kwenye kundi kubwa linalojulikana kama antimicrobials. Antimicrobials ni dawa ambazo
hutumika kuua au kuzuia ukuaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa ya
kuambukiza kwa binadamu na wanyama.
- Tafiti
za Kimataifa zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa duniani la matumizi ya
dawa za antibiotikis’. Kwa mwaka
2000-2010 matumizi ya dawa za antibiotiki yaliongezeka kwa asilimia thelathini (30%). Pia, tafiti
hizo zinaonesha kuwa kwa mwaka 2010 jumla ya tani 63,200 za antibiotiki
zilitumika kwa mifugo peke yake.
- Dawa
hizo zinatumika vibaya, ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 20- 50 ya antibiotiki zinatumika isivyo sahihi
duniani.
- Hapa
nchini Tanzania, Utafiti uliofanywa na Wizara mwaka 2014 katika mikoa ya
Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya na Mwanza ilionesha matumizi makubwa ya
dawa za antibiotiki hadi kufikia asilimia
67.7. Pia, tafiti zimebainisha kuongezeka kwa kiwango cha usugu wa antibiotikisi. Mfano, utafiti wa kitaifa
uliofanyika juu ya usugu wa dawa za kifua kikuu (MDR-TB) ilionesha usugu
wa dawa kwa wagonjwa wapya kuwa ni asilimia
1.1; na kwa wagonjwa wanaorudia dawa za TB baada ya kupona kuwa na
usugu wa asilimia 3.9. Pia,
katika kutibu ugonjwa wa malaria, usugu wa dawa za Chloroquine na
Sulfadoxine/Pyrimethamine, au “SP” ulijitokeza na kupelekea kutumika kwa
dawa ya sasa iitwayo Artemether/Lumefantrine, au “ALU”.
- Katika
tafiti ya kutibu maambukizi ya njia ya mkojo (Urinary Tract Infection, au “UTI”)
kwa kutumia dawa ya sindano ya gentamycin uliofanyika katika hospitali ya
Taifa ya Muhimbili ilionesha kuongezeka kwa usugu wa dawa hiyo kutoka
asilimia 6.9 mwaka 2003 hadi asilimia 44 mwaka 2011. Aidha, katika kutibu
ugonjwa huo, tafiti nyingine ilifanyika katika hospitali ya Rufaa ya Kanda
ya Bugando, ambapo imeripotiwa kuongezeka kwa usugu wa dawa ya sindano ya
ceftriaxone kutoka asilimia 14 mwaka 2009 hadi asilimia 29.4 mwaka 2011.
- Zipo
sababu nyingi zinazochangia uwepo wa usugu wa dawa za antimicrobials. Mojawapo ni maduka mengi ya dawa kuuza kwa
wananchi dawa za antimicrobials
bila cheti cha daktari au kutotoa dozi kamili. Ikumbukwe kuwa dawa za antimicrobials hutolewa kwa cheti
cha daktari tu.
- Wakati
mwingine dawa za binadamu hutumika kutibia wanyama kinyume na sheria za
matumizi ya dawa. Pia wapo wafanyabiashara wanaoandaa vyakula vya wanyama
ambao wamekuwa na tabia ya kuongeza antimicrobials
kwenye vyakula hivyo kwa kufikiria kuwa zinasaidia mnyama husika kukua
haraka na kutopata magonjwa.
- Madhara yanayoweza kutokea
kutokana na usugu wa dawa za antimicrobials
ni pamoja na magonjwa kushindikana
kutibiwa na dawa hizo na hata kuweza kusababisha vifo.
- Matibabu
mbadala baada ya dawa za kawaida kuwa sugu yanakuwa na gharama kubwa na ya muda mrefu.
Mfano, matibabu ya mgonjwa mpya wa Kifua Kifuu kwa dawa za kawaida
yanafanyika kwa kipindi cha miezi sita na yanagharimu takribani shilingi
laki nne (400,000/=). Ikitokea mgonjwa huyo akapata kifua kikuu sugu
matibabu hayo yanatibiwa kwa miezi 20 hadi 22 na gharama zake ni takribani
shilingi milioni kumi na saba. Kama mgonjwa huyo atapata kifuu kikuu Sugu
Zaidi matibabu yake yanakuwa ya muda mrefu zaidi na gharama kubwa takriban
shilingi milioni 64.
- Watanzania wanashauriwa
kuacha mazoea ya kununua dawa ovyo bila kupata cheti cha Daktari na ushauri wa
wataalamu wa afya. Ndugu wananchi, vile vile nasisitiza ni muhimu sana
kumaliza dozi za dawa.
- Kila mmoja wetu ana mchango mkubwa katika kuzuia
uwezekano wa vimelea kujenga usugu dhidi ya dawa za antimicrobials.
Mapambano dhidi ya usugu wa dawa za antimicrobials yatafanikiwa tu pale
ambapo mimi na wewe kwa ujumla tutashiriki katika vita hii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- AFYA
16 Novemba, 2017
Chapisha Maoni