WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE
NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU USAMBAZAJI WA KONDOM KWA UMMA.
Kumekuwa na taarifa mbalimbali, hamaki na kejeli zinazoenea katika
mitandao ya kijamii kuhusiana na taarifa iliyotolewa tarehe 27 Novemba
2017, Mnazi Mmoja kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kondom kuhusu
mpango wa Serikali kununua na kusambaza kondom 500,000,000 katika kipindi
cha miaka mitatu 2018 hadi 2020.
Tunapenda kuukumbusha umma wa Watanzania kwamba maambukizi ya VVU
na UKIMWI bado ni tatizo katika nchi yetu. Takriban watu 1,400,000 wanakadiriwa
kuwa na VVU.
Hivyo katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI Serikali inaendeleza
afua mbalimbali ili kuzuia maambukizi mapya. Asilimia 40% ya maambukizi
mapya yanatokea miongoni mwa vijana wenye umiri wa miaka 15-24.
Aidha
makundi maalum kama vile wanaojidunga madawa ya kulevya, wanaofanya
biashara ya ngono na wale wanaoamiiana wa jinsia moja wako katika hatari
kubwa ya kupata maambukizi. Makundi mengine ya walio katika hatari
ni waendesha magari ya masafa marefu, wavuvi na wananchi wa kwenye migodi.
Wizara inatekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha
na kupima uwepo wa VVU, na kisha kuanza tiba na matunzo, pamoja na kutoa
dawa za kufubaza kwa watakao kuwa na maambuzi ya VVU.
Kuna afua pia
za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto, kutoa elimu ya VVU/UKIMWI
na afya uzazi kwa vijana, elimu kuhusu VVU/UKIMWI kwa jamii na tohara
kwa wanaume. Matumizi ya kondom ni moja wapo ya afua katika kuzuia maambukizi
mapya.
Hata hivyo utafiti wa viashiria vya Malaria na UKIMWI wa mwaka
2011/12 umebaini kuwa kuna matumizi duni ya kondom, kwani ni asilimia
27 tu ya watu wenye wenza zaidi ya mmoja waliokiri kutumia kondom mara
ya mwisho walipofanya ngono.
Hivyo Serikali itaendelea kununua na kusambaza
kondom kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na mimba
zisizo tarajiwa ikiwa ni mojawapo ya afua hizo za kudhibiti maambukizi
ya VVU.
Tunasisitiza kuwa Wizara na wadau wake inaendelea kutoa elimu ya kondom
sambamba na elimu ya kusubiri kufanya ngono kwa wale ambao hawajaanza
na wale ambao wameanza lakini wanapaswa kusubiri (Abstinence) na elimu ya
kuwa waaminifu kwa mwenza mmoja aliye mwaminifu na anaejua hali yake
ya maambukizi ya VVU (Be faithfull). .
Hivi sasa nchini kuna vyanzo vya upatikanaji wa kondom vya aina tatu.
Kwanza ni kondom zinazopatikana kupitia sekta ya umma ambazo husambazwa
na Serikali kwa wananchi bila malipo.
Pili, kuna kondom zinazosambazwa
na wadau ambazo zinauzwa kwa bei ya chini kwa kuwa wadau wamechangia.
Mfano kondom za Salama na Dume, na chanzo cha tatu ni kondom za kibiashara
ambazo zinauzwa kwa bei ya kati na ya juu.
Kondom za sekta ya umma husambazwa kupitia vituo vya kutolea huduma
za afya na huduma za mkoba ngazi ya jamii, Kondom za wadau na zile za
biashara husambazwa katika maduka ya dawa, maduka ya bidhaa mbambali,
baa na nyumba za wageni.
Kwa mwaka 2016/17 Serikali iliboresha kondom zinazopatikana kupitia
ya sekta ya umma kwa kuipa kifungashio kipya na jina la ZANA, ambapo
kondom 36,916,911 zilisambazwa.
Kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2018 hadi 2020 Serikali kwa kushirikiana
na Mfuko wa Dunia wa kudhibiti malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu inatarajia kununua kondom za kiume takribani 500,000,000.
Kondom hizi zitasambazwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na
katika maeneo hatarishi yanayoaminika kuwa na watumiaji wengi. Aidha,
kwa vile imebainika kuwa watu ambao hawaumwi hawaendi vituo vya afya
kwa ajili ya kuchukua kondom tu na hivyo kupelekea kutofikia
walengwa, usambazaji na ugawaji huu utalenga maeneo ambayo kuna matukio ambayo yanaendana na ngono na yana walengwa wa afua za
kondom. Maeneo haya ni kama baa, nyumba za kulala wageni, maeneo yenye
mikusanyiko ya magari ya masafa marefu, maeneo ya uvuvi na migodini.
Aidha ikumbukwe kwamba nchi yetu ina sera sheria, mila, desturi na
maadili yetu kama watanzania, Hivyo kondom zote haziruhusiwi kusambazwa
bila kufuata miongozo ya Wizara, ili kulinda zisifike kwa wasiolengwa.
Hivyo basi, iwapo tunataka kuzuia na kumaliza maambukizi ya VVU na
UKIMWI ifikapo 2030 tunapaswa kama nchi kuwekeza katika kuzuia maambukizi
mapya. Matumizi ya kondom, ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi, dawa
za ARV na za magonjwa nyemelezi ni afua muhimu.
Tunaomba wanahabari
na wananchi waunge mkono juhudi hizi kwa kuwa tunahitaji watanzania
wenye afya bora na uwezo wa kuzalisha ili kuijenga Tanzania ya Viwanda.
Imetolewa na:
KATIBU MKUU - AFYA
Chapisha Maoni