Picha na mtandao
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAKATI baadhi ya ndugu wa wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) wakilalamikia kitendo cha kulipisha faini ya Sh 50,000 pindi wanapokutwa
wamekaa juu ya vitanda vya wagonjwa.
Uongozi wa Hospitali hiyo umesema haujawahi kupokea
malalamiko yoyote kuhusu suala hilo.
Mmoja wa ndugu aliyelazwa hospitalini hapo ambaye
hakutaka jina lake litajwe gazetini alilieleza MTANZANIA kwamba kitendo hicho
kimekuwa kikifanyika katika jengo la watoto lililopo hospitalini hapo.
“Imekuwa kero kubwa, kuna wauguzi ambao ukikaa
kwenye kitanda cha mgonjwa wanakuchukua na kukudai faini ya Sh 50,000,
inatushangaza kwa sababu hakuna tangazo lolote la hospitali lililobandikwa
kutoa onyo lolote.
“Ukikaa tu unashtukizwa, unachukuliwa na kwenda
kulipishwa faini hiyo… na hakuna kiti angalau kimoja angalau mtu aweze kukaa
wakati akimuuguza ndugu yake,” alidai.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA (matukionamaisha) lilimtafuta Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha (Pichani) ambaye alionesha kushangazwa na suala hilo.
“Ni uwongo, Muhimbili hatutozi faini kwa kosa la
ndugu kukaa juu ya kitanda cha mgonjwa, jamii ielewe kwamba hospitali haina
utaratibu huo,” alisema.
Aliongeza “Lakini ‘hatu-incourage’ (hatupendelei)
ndugu wakalie vitanda vya wagonjwa kwa sababu mwisho wa siku wataondoka na
‘infections’ (maambukizi)… huku ni hospitali.
Alisema ni vigumu kuweka angalau kiti kimoja katika
wodi za wagonjwa wa jumla kama ilivyo kwa wodi za VIP kwa sababu kutaongeza
msongamano wa watu.
“Hatuwezi kwa sababu unakuta wodi ina vitanda 30
hadi 40 tukisema tuweke viti maana yake itabidi tuweke kulingana na idadi ya
vitanda tutakuwa tumeongeza msongamano mkubwa mno ndani ya wodi.
“Hivyo, naomba ndugu yeyote atakayedaiwa kutoa
kiasi hicho cha fedha ni vema aje atoe taarifa na sisi tutazifanyia kazi haraka
iwezekanavyo dhidi ya muhusika,” alitoa rai.
Habari hii imeripotiwa leo kwenye gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia pia
Chapisha Maoni