Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
  
Picha na mtandao 

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

SCHIZOPHRENIA ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya akili. Jina hilo limetoholewa kutoka katika lugha ya kilatini ambapo asili yake ni maneno mawili ambayo ni Schizo na Phrenia.

Kwa tafsiri ya lugha ya Kiswahili rahisi humaanisha akili iliyogawanyika au iliyotawanyika, yaani huwa haziendi sawa sawa… huwa hakuna muunganiko kati ya mtu na akili yake.

Yapo magonjwa mengi ya akili ambayo kati yake yapo yanayohusisha kuchanganyikiwa akili kama huu wa Schizophrenia.

Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Said Kuganda anafafanua vema kuhusu ugonjwa huo katika makala haya aliyozungumza hivi karibuni na MTANZANIA (matukionamaisha).

“Huwa haziendi sawa sawa, yaani hakuna muunganiko kati ya mtu na akili yake, kuna magonjwa mengi ya akili ambayo kati yake yapo yanayohusisha kuchanganyikiwa akili kama huu wa Schizophrenia.

“Lakini pia yapo ambayo hayahusishi kuchanganyikiwa akili, watu wengi wanaugua magonjwa ya akili lakini huwa hawachanganyikiwi isipokuwa wapo wachache ambao wakiugua huchanganyikiwa,” anabainisha.

Dk. Kuganda anasema wale ambao huchanganyikiwa nao kuna vipindi fulani katika maisha yao huwa wanakaa sawa na kuna kipindi huonesha ile hali ya kuchanganyikiwa.

Kuchanganyikiwa akili maana yake nini?

Anafafanua “Kuna maeneo matano ambayo ni muhimu katika mwili wa binadamu ambayo huashiria akili kuchanganyikiwa.
“Eneo la kwanza ni kuwa na imani ambayo si halisi (potofu) iliyopitiliza katika ule uhalisia wake wa kawaida,” anasema.

Utajuaje?

Daktari huyo anasema ili kubaini jambo hilo ni lazima mgonjwa apimwe kwatika nyenzo zote muhimu zinazohitajika.

“Kwa mfano mila na desturi zake, tunaangalia kwao wanaamini nini kuhusu hicho anachokiamini yeye, elimu yake inamueleza nini kuhusu kitu anachokiamini na je dini yake inaeleza nini  kuhusu jambo analoliamini,” anasema.

Anaongeza “Wakati mwingine unakuta ana imani sahihi lakini huenda imepitiliza, sasa kujua iwapo imepitiliza kile kiwango au la lazima tulete vigezo muhimu na tujadiliane pamoja naye ili kujiridhisha.

“Tukibaini kuna ambavyo ameviruka tunamuuliza sababu ya kuviruka na kwenda kwenye vigezo vingine, kwa mfano mtu anaweza kusema yeye ni Mungu kwamba hiyo ndiyo imani yake na anashughulikia viumbe vyote.

“Inabidi muhojiane naye katika upande huo huo wa kuzungumzia Mungu na uwezo wake tofauti na Mungu ambaye wengine wote tunamfahamu,” anasema.
Anaongeza “Hivyo tuna-challenge ile imani yake, ikishafika kipindi kwamba hana uwezo wa kurudi nyuma katika kile anachokiamini na jamii husika na elimu na vyote vilivyobaki (background information) kwamba alipo yeye siko basi tunajua mtu huyo amechanganyikiwa.

“Na hapo anakuwa anashughulishwa na yale anayoamini, kama amesema yeye ni Mungu basi unakuta hata ametengeneza mamlaka au anashurutisha watu wafanye mambo fulani fulani.

“Matokeo yake mambo yake huwa hayafanikiwi kwa sababu anakuwa anaendeshwa na ile imani potofu aliyokuwa nayo,” anabainisha.

Daktari huyo anasema lakini yapo mambo mengine ambayo huweza kubainisha mtu kuwa na tatizo hilo la Schizophrenia.

“Kwa mfano katika hali ya uhalisia mtu anaweza kulalamika kuna watu nje ya nyumba yake wanamsubiri huku wamebeba silaha wakitaka kumdhuru.

“Sasa unakuta mtu analalamika kuna watu wanamfuatilia wamdhuru nje ya nyumba yake lakini mkifuatilia kwa kina hata kwa kukaa nje ya nyumba yake hamuwaoni watu hao lakini yeye anang’ang’ania kwamba wapo, hiyo inakuwa ni imani ambayo si ya kweli,” anasema.

Dk. Kuganda anasema hali hiyo huweza kumsababishia muhusika kuogopa kabisa kutoka nje ya nyumba yake akiamini kuna maadui wanamsubiri.

“Kama ni mfanyakazi moja kwa moja hali hiyo huathiri ule utendaji kazi wake wa kila siku, anaweza kuamua asiende kazini kabisa na akajikuta akifukuzwa kazi lakini wakati huo ofisi yake huenda haijui kabisa kama anakabiliwa na tatizo la akili,” anasema.

Anaongeza “Eneo jingine ambalo linaashiria akili kuchanganyikiwa ni kuwa na hisia ambazo ni potofu, kwa kawaida binadamu ana hisia tano muhimu za kawaida.

Anazitaja hisia hizo kuwa ni za kuona, kugusa, kuonja, kusikia na kunusa.

“Lakini mtu aliyechanganyikiwa anaweza kutumia nyenzo hizo hizo kuona, kuhisi, kunusa, kugusa au kusikia vitu ambavyo wengine hatuoni, hatuhisi, wala kusikia,” anabainisha.

Dk. Kuganda pichani anatoa mfano kwamba “Muhusika anaweza kusema anaona nyoka anapita eneo ambalo mmekaa naye pamoja lakini nyie msimuone au anasikia sauti na watu wanazungumza habari zake, wanamshurutisha au wanamtisha lakini nyie hamuoni wala hamsikii chochote.

Anaongeza “Wakati mwingine anaweza kudai kwamba anasikia sauti yake mwenyewe,… kwamba yale anayowaza na kutafakari anasikia kikizungumzwa huko redioni.

“Wakati mwingine anaweza kuhisi kuna vitu ambavyo vinatambaa mwilini mwake (hii ni hisia ya kugusa)  lakini kila anacholalamika kwamba kinamsumbua unakuta nyie wengine hamkioni ila yeye kinakuwa kweli kinamsumbua na mambo yake unakuta hayaendi sawa sawa,” anasema.

Anasema wakati mwingine mnaweza kula naye chakula aina moja lakini yeye akalalamika kupata ladha tofauti na ile mnayoipata nyie.

“Anaweza hata akadai chakula chake kimetiwa sumu lakini si kweli, au wakati mwingine akanusa harufu ambazo hazipo,” anasema.

Anasema ingawa hayo wakati mwingine huwa ni mambo ya kawaida hata hivyo yakipitiliza huashiria kuwapo kwa tatizo hasa la kuchanganyikiwa kwa akili ya muhusika.

Anasema hali hiyo husababisha tabia za muhusika kubadilika na hata mienendo yake kwa ujumla.

“Mnaweza kumbaini pia kwa maneno yake, anaweza kuongea vitu vingi ambavyo havina muunganiko kutoka stori ya kwanza kwenda ya pili.

“Kwa mfano akaanza kuwasimulia amezaliwa lini, kisha hapo hapo akahamia stori nyingine labda kuhusu mambo ya barabarani mara akaanza tena kuwasilimulia kuhusu mambo ya Marekani.

“Tunasema anaongea ovyo ovyo kwa hiyo kule kuongea ovyo ovyo kunaonesha wazi dalili ya kuchanganyikiwa hata kama hajawaambia anaumwa,” anasema.

Rahisi kumtambua

Dk. Said anasema ni rahisi kumuangalia hata kwa matendo yake.

“Kuna kuchanganyikiwa kwa matendo yake kwa mfano wale wanaotembea barabarani utaona wanaanza kubeba mizigo mikubwa, wanavaa nguo zaidi ya moja wakati mwingine hadi nane, hiyo huashiria kwamba kile kiwango cha kuchanganyikiwa kimekuwa kikubwa mno,” anabainisha.

Anaongeza “Yaani hata kama hujaambiwa kitu ukimtazama tu unajua kwamba mtu huyo amechanganyikiwa.

“Unaweza pia kubaini, wakati mwingine wagonjwa wa aina hii hujitenga na jamii, hujitengenezea ulimwengu wa peke yao, unakuta mtu anatabasamu mwenyewe, anaongea mwenyewe na mambo mengine kama hayo.

“Huwa hawahitaji kuingiliwa au kuwaingilia wengine ndiyo maana hujitenga, hapo huonesha wazi viashiria vya kuchanganyikiwa,” anasema.

Anasema mgonjwa huweza kuonesha mambo mawili au matatu na wakati mwingine yote matano kati ya hayo aliyoeleza hapo juu.

“Ni ugonjwa ambao hukaa muda mrefu kuanza kuonesha dalili hadi kipindi cha miezi sita lakini wakati mwingine hali hiyo huweza kutokea ghafla,” anasema.

Idadi ya wanaougua

“Katika magonjwa yote ya akili tunayoyafahamu huu ni ugonjwa ambao katika ‘population’ watu chini ya asilimia moja huugua ugonjwa huu,” anasema.

Anaongeza “Kiwango cha kuathirika kipo sawa kwa jinsi zote ( wanaume na wanawake) lakini kuna vitu ambavyo huchangia mtu kupata ugonjwa huu.
Idara hii hupokea wagonjwa wote wa dharura ikiwamo wanaofikishwa wakisumbuliwa na magonjwa ya akili

Visababishi

Anasema ugonjwa huo hurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“Ikiwa katika kizazi chenu kuna mtu amewahi kuugua ugonjwa huo basi kuna uwezekano wa mmoja wenu kurithi kwa sababu shida ipo katika akili,” anasema.

Anasema mambo mengine ambacho huchangia mtu kupata ugonjwa huo ni changamoto za kimaisha.

“Hali ya umaskini, kutokuwa na kazi na ikiwa mtu aliwahi kupata majanga mbalimbali wakati wa makuzi yake anauwezekano wa kupata ugonjwa huu katika maisha yake,” anasema.

Anaongeza “Ingawa si visababishi vya moja kwa moja lakini mara nyingi humuwekwa mtu kwenye hatari ya kuja kupata ugonjwa huu.

Wenye akili nyingi

Yapo madai kwamba baadhi ya watu huzaliwa wakiwa na akili nyingi kuliko wengine na hali hiyo hupelekea kuchanganyikiwa akili katika maisha yao, Dk. Kuganda anafafanua madai hayo.

“Si kweli, hakuna uhusiano wowote kati ya mtu kuzaliwa akiwa na akili nyingi na kuchanganyikiwa,” anasema Dk Kuganda.

Anaongeza “Isipokuwa kuna ugonjwa mwingine ambao si Schizophrenia. Huo mtu akiugua akili zake huwa zina-charge vizuri lakini akipona akili yake hurejea katika hali yake ya kawaida.

“Lakini huu wa Schizophrenia hauhusiani kabisa na akili ya mtu kwamba aliyesoma sana anaweza kuugua ugonjwa huu lakini wale ambao hawajasoma huwa kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu,” anasema.

Anafafanua “Usiposoma kabisa maana yake hujaelimika na labda huna kazi, hapo vitu vingi hujipanga na vingi huwa ni changamoto hali hiyo hupelekea akili kuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kulipuka.

“Tunasema kuchanganyikiwa ni mlipuko wa akili hata wale ambao wapo barabarani jamii huwatenga bila kujua kwamba ile hali hujitokeza tu na wakipata matibabu sahihi akili hurejea katika hali yake ya kawaida,” anasema.

Anasema hata hivyo pindi wanapochelewa kupatiwa matibabu sahihi ingawa hupona wakitibiwa hata hivyo matibabu huchukua muda mrefu.

“Magonjwa mengi ya akili huja na kuondoa ndiyo maana tunasema mlipuko tu ule yakitibiwa huondoka na mtu hupona,” anasisitiza.

Jinsi wanavyotibu

Anasema hwua wanatumia njia tatu kuwatibu wagonjwa wa akili ambazo ni za kibaiolojia, kisaikolojia na

“Kibaiolojia huwa tunawapatia dawa mbalimbali za kuondoa zile dalili lakini yapo ambayo huwa hayahitaji kutibiwa kwamba dawa bali kwa mazungumzo maalum (kisaikolojia) na matibabu ya kijamii.

“Huwa tunazungumza kitaalamu na mgonjwa namna ya kupunguza msongamano wa mawazo kwenye ubongo wake, ule msongamano ukipunguabasi mtu huweza kutafakari vizuri na kufanya maamuzi sahihi,” anasema.

Anasema kwa upande wa matibabu ya kijamii huwa wanakaa na kuzungumza na watu wanaomzunguka mgonjwa husika.

“Kwa sababu unaweza kukuta shida haipo kwa mgonjwa bali kwa jamii inayomzunguika, wakati mwingine matibabu huhitaji kufanya kazi basi hapo huwa tunamtibu mgonjwa kitaalamu kwani si kila kazi anapaswa kufanya kutibu akili yake,” anabainisha.

Anaongeza “Lakini kuna wakati mwingine huwa tunalazimika kuchanganya matibabu yote haya kwa wakati mmoja ili kupata matokeo mazuri zaidi kwa mgonjwa.

Vijana hatarini

Anasema mara nyingi tatizo la Schizophrenia hutokea mtu anapokuwa katika hatua ya ujana hasa kuanzia kipindi cha miaka 18 hadi 25.

“Hiyo ni kwa sababu huo ndiyo umri wenye changamoto nyingi kuliko makundi mengine, mtu anaweza kurithi lakini mlipuko wa kwanza wa akili ukatokea akiwa na umri wa miaka 25.

“Kwa sababu katika kipindi hicho mtu hukutana na changamoto nyingi za kimaisha kuliko kipindi kingine katika maisha yake,” anabainisha.

Uelewa duni

Daktari huyo anasema bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa hayo kwamba pindi mtu anapougua anapaswa kuwahishwa hospitalini kupatiwa matibabu na si vinginevyo.

“Unakuta wengi wanawafungia majumbani au wanasukumia huko mitaani au wanawapeleka kwenye nyumba za ibada au kwa waganga wa kienyeji wakiamini wamerogwa jambo ambalo si sahihi,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo wengi hufikishwa hospitalini miaka miwili hadi mitatu tangu walipoanza kuugua.

“Wale ambao huwahishwa hospitalini mara nyingi unakuta hali ya kuchanganyikiwa huhusisha kufanya vurugu na wapo ambao tunapoanza kuwatibu wakitulia tu ndugu zao huwachukua na kuondoka nao huku wakiwa hawajapona vema,” anasema.

Rai kwa jamii

“Ni vema ukipata ndugfu yako ameugua ugonjwa wa akili mumuwahishe hospitalini apate matibabu sahihi kwani karibu magonjwa yote ya akili yanatibika na watu huendelea kuishi kwa amani na furaha kama awali.

“Kuliko kumfungia mgonjwa ndani si jambo zuri, kunyanyapaa pia si vizuri jaribu kufikiri jinsi unavyomsukumia mtaani ingekuwa wewe ungejisiaje, kusema ule ukweli kwamba wagonjwa wengi wa akili huwa hawapendi na hawajisikii vizuri kuendelea kukaa huko mitaani,” anasema.

Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka Desemba 28, 2017 katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement