Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Serikali na Afya tawi la
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TUGHE-TIC) wakiapa mbele ya Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. Hafla hiyo ilifanyika katika
ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
SEKTA ya viwanda imepewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli.
Mpango wa serikali ni kufikia Tanzania ya viwanda,
hivi sasa mikakati mbalimbali imepangwa na inatekelezwa kufanikisha lengo hilo.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage anasema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ni miongoni mwa taasisi muhimu
mno katika kufanikisha suala hilo.
Desemba 15, mwaka huu Waziri Mwijage alizindua
rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tawi la TIC (TUGHE-TIC).
Akizindua Baraza hilo, anasema litasaidia kuongeza
chachu ya ushiriki wa wafanyakazi moja kwa moja katika uandaaji wa mipango
mbalimbali na utekelezaji wake.
“Ili tuweze kupata matokeo mazuri, nimepewa kazi ya
kujenga viwanda, TIC ni jicho na masikio yangu katika kulitimiza jambo hilo,”
anasema.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akimkabidhi
mkataba wa uundwaji wa Baraza la Wafanyakazi wa Serikali na Afya tawi la Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TUGHE-TIC), Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe mara
baada ya kuzindua Baraza hilo
Anaongeza “Bado TIC hamjafanya kazi kiasi cha
kunifurahisha, nataka mfanye kazi kama vile waganga wa kienyeji wanavyofanya
kazi zao.
“Mganga wa kienyeji huwa hakosi majibu ya maswali
aliyonayo mteja wake yeyote anayempokea katika kibanda chake.
“Nataka mtu akija kwenu kutaka kuwekeza au
nikimuelekeza mtu kwenu basi apate majibu ya mahitaji yake na ikiwa hamna
nendeni pembeni mnipigie simu moja kwa moja ili niwape maelekezo,” anasisitiza.
Mgongano
wa kisheria
Waziri huyo anawataka TIC kufanya kazi kwa weledi
na kwamba pale ambapo kunatokea mgongano wa kisheria wamjulishe mapema.
“Ili kufikia Tanzania ya viwanda inahitajika
mabadiliko ya kifkira, penye mgongano wa kisheria nijulisheni ili tuipitie na
kuifanyia maboresho au marekebisho pale inapobidi, tunaongozwa na sheria ambazo
si msahafu wala biblia,” anasema.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akimkabidhi mkataba
wa uundwaji wa Baraza la Wafanyakazi wa Serikali na Afya tawi la Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TUGHE-TIC), Mwenyekiti wa Baraza hilo, Brandon Maro mara
baada ya uzinduzi huo
Hali
ya uwekezaji
Akizungumzia hali ya uwekezaji kwa sasa nchini,
Waziri Mwijage anasema ni nzuri ikilinganishwa na hapo awali.
“Nimesema awali, TIC ndiyo jicho na sikio letu
katika kufikia Tanzania ya viwanda, ninyi ndiyo receptionalist (mapokezi) yetu.
“Kimsingi watu wote wanaohitaji kuwekeza nchini lazima
waanzie TIC na anayepaswa kuelekeza na kufundisha kuhusu uwekezaji ni TIC
wapokeeni watu na muwaelekeze inavyopaswa,” anasema.
Anasema katika kipindi cha miaka miwili tayari kuna
jumla ya viwanda 3,306 vyenye uwezo wa kuajiri kuanzia wafanyakazi 10 na
kuendelea.
“Viwanda vikubwa vipo 580 na nina matumaini ya
viwanda vikubwa zaidi, tunaelekeza kwenye sekta tatu viwanda vinavyotoa ajira
kwa watu wengi, vinavyochakata malighafi kutoka nchini na viwanda
vinavyozalisha bidhaa zinazotumika kwa wingi,” anabainisha
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akifafanua
jambo mara baada ya kuwakabidhi wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Serikali na
Afya, Tawi la Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TUGHE-TIC)
Waziri Mwijage anasema leo hii Tanzania ina uwezo
wa kuzalisha saruji kuliko uhitaji wan chi, kuna uwezo wa tani milioni 10.8 na
mahitaji ni tani milioni 4.87.
“Kuna viwanda viwili vinakuja cha Mamba na Nyati
vyote vitakuwa Chalinze na kingine kitaenda Tanga, kuna vya kuchakata matunda.
“Dabaga naye anatengeneza tomato saurce nchini na
Sayona anazindua kiwanda Januari mwakani cha kuchakata matunda, hivyo
tunakwenda vizuri,” anasema.
Anaongeza “Ndiyo maana nikasema Baraza hili ni
muhimu, kwa sababu wafanyakazi wakishaelewa tunategemea watawakaribisha vizuri
watanzania na wageni wanaohitaji kuwekeza nchini.
Vipimo
vya WB
Anasema vipimo vya Benki ya Dunia (WB)
vilivyotolewa hivi karibuni kuhusu wepesi wa kuwekeza duniani Tanzania ina
namba mbaya ya uwekezaji.
“Lakini mimi hiyo hainibabaishi kwa sababu vitu
vingine vinahitaji ukombozi wa kifkra kuna mambo ambayo lazima tuondokane nayo
ili twende kwenye nafasi tunayostahili.
“Tunataka mtu akiwekeza hapa afurahie kuwekeza
Tanzania, kiujumla hali ya uwekezaji ni nzuri na hiyo misukosuko mnayoisikia ni
kwa sababu ya kutaka malengo makubwa.
“Ni kama vile mgumba akiolewa miaka 30 anataka
apate mtoto na amtume dukani hapo hapo, tumeahidi viwanda lazima tufikie
lengo,” anasema.
Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe anasema Baraza
hilo lina jumla ya wajumbe 35 na kwamba kati yake wapo wawakilishi wa kuteuliwa
kutoka nje ya kituo ambao wanaingia kwa mujibu wa sheria na kanuni.
“Baraza hili ni la muhimu mno katika kuboresha
ufanisi na utendaji kazi wa kituo ikiwamo utekelezaji wa maagizo na maelekezo
ya Rais John Magufuli,” anasema.
Chapisha Maoni