Picha inaonesha mfumo wa chakula
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MWAKA 2015, Mariam John alijifungua salama mtoto wake wa
pili Elizabeth Peter (si majina yao halisi), huko mkoani Kigoma ambako ndipo yalipo
makazi yao.
Maendeleo ya afya ya Elizabeth yalikuwa yanaridhisha kila
walipohudhuria kliniki lakini miaka miwili baada ya kuzaliwa hali ilianza
kubadilika ghafla.
Mariam anasema siku moja alipokuwa akimnawisha sehemu ya
haja kubwa mtoto wake huyo, baada ya kumaliza kujisaidia alishangaa kugusa
kinyama ambacho kilijitokeza kwa nje.
“Awali sikutilia maanani suala hilo, nikadhani kwamba labda
kimejitokeza na kitarudi baada ya muda fulani lakini kadri muda ulivyosonga
mbele hali ilizidi kuwa mbaya,” anasema.
Anasema kinyama hicho kiliendelea kuongezeka urefu kutoka
nje hali ambayo ilimfanya awe na wasiwasi mkubwa juu ya afya ya mtoto wake
huyo.
Anasema aliamua kumjulisha mumewe na ndugu zake wa karibu
juu ya hali hiyo iliyomtokea mwanawe.
“Kinyama hicho kilikuwa kikijitokeza kila alipokuwa
akijisaidia haja kubwa, ikafika hatua…. Siku moja nikaona utumbo umetoka nje
kabisa katika sehemu hiyo,” anasema.
Anasema wapo watu ambao walimshauri kumpeleka hospitalini
mtoto wake ili akapewe matibabu lakini wengine walimshauri ampeleke kwa waganga
wa kienyeji.
“Walionishauri nimpeleke kwa mganga wa kienyeji walikuwa
wengi, walinieleza kwamba hali hiyo si ya kawaida na kwamba mwanangu amerogwa,
na iwapo nitaendelea kukaa naye bila kumpeleka huko atapoteza maisha wakati
wowote,” anasema.
Anasema hata hivyo, baadhi ya ndugu zake walimueleza kwamba
ampeleke mapema hospitalini ili afanyiwe uchunguzi wa kina kujua anasumbuliwa
na ugonjwa gani.
Safari
ya matibabu.
Mariam anasema alimpeleka katika zahanati moja iliyopo
mkoani humo ambako hata hivyo baada ya kumfanyia vipimo hawakugundua tatizo
lililokuwa likimsumbua.
“Waliniandikia dawa mbalimbali ambazo nilimpatia mwanangu
lakini hakupona wala hakupata nafuu, kila siku hali ilizidi kuwa mbaya,”
anasema.
Anasema aliamua kumshirikisha suala hilo rafiki yake ambaye
anaishi huko eneo la Mburahati jijini Dar es Salaam.
“Nilibaki njia panda, sikujua nifanye nini kumsaidia
mwanangu, rafiki yangu alinishauri nijitahidi nifike Dar es Salaam, kwamba
tatizo hilo linatibika kabisa,” anasema.
Anasema mumewe alijitahidi kutafuta nauli na fedha za
kujikimu na za matibabu, safari ikaanza kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam.
“Tulifika salam, nashukuru rafiki yangu alinipokea na
kunikaribisha nyumbani kwake, ilikuwa mwishoni mwa April, mwaka jana, nikaanza
matibabu pale katika Hospitali ya Amana,” anasema.
Anasema madaktari wa hospitali hiyo baada ya kumfanyia
vipimo mtoto wake walimueleza kuwa anahitaji huduma ya kibingwa ndipo
wakampatia rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Tayari
ametibiwa
Mariam anasema mwanawe amefanyiwa upasuaji wa kurudisha
ndani sehemu ya utumbo uliotoka nje.
“Nawashauri wazazi na walezi wanapoona mabadiliko yoyote ya
kiafya katika miili ya watoto wao wawapeleke hospitali na si kwa waganga wa
kienyeji, huko watapoteza muda na watoto wao watazidi kuugua na kuteseka kila
siku,” anashauri.
Elizabeth
alipatwa na nini
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Muhimbili, Zaituni Bokhary anasema Elizabeth alipata tatizo
linalojulikana kitaalamu Rectal Prolapse.
“Hii ni hali ambayo sehemu ya utumbo mkubwa iitwayo rectum
hutoka nje ya mwili katika njia ya haja kubwa. Hakuna sababu maalumu ambayo
wataalamu tunaweza kusema moja kwa moja, kwamba tatizo limesababishwa ama na
bakteria au wadudu. Lakini kuna viashiria au visababishi kadhaa ambavyo vinahusishwa
kusababisha tatizo hilo kutokea,” anasema.
Visababishi
vyenyewe
Dk. Bokhary anavitaja kwamba ni kuharisha muda mrefu hali
ambayo husababisha mtoto kupungua uzito na kukonda mwili.
“Hii ni sababu kuu, kuharisha muda mrefu hupeleka mtoto hukonda
mwili hadi ile misuli ya haja kubwa hushindwa kukaza vizuri kama inavyotakiwa hali
hiyo hupelekea ile rectum kutoka nje,” anafafanua.
Anasema kiashiria kingine cha awali ambacho mzazi anaweza
kukiona iwapo mtoto anakabiliwa na tatizo hilo ni kupata viotea (vinyama)
ambavyo hutoka katika nia ya haja kubwa.
“Vinyama hivyo hutoka nje ya mwili katika sehemu ya haja
kubwa. Wakati mwingine tatizo huweza kujitokeza iwapo kuna maambukizi katika utumbo
mkubwa,” anasema.
Daktari huyo anasema iwapo mtoto aliwahi kufanyiwa upasuaji
wa utumbo mkubwa, inaweza kusababisha akapatwa tatizo hilo kwa namna moja au
nyingine.
“Lakini wengine wanapata tatizo hili, ikiwa wamezaliwa na
hawana chembe chembe maalumu ambazo kazi yake kuu ni kusukuma choo nje ya
mwili, sasa kwa kuwa hajazaliwa na chembe chembe hizo mtoto huyo anakuwa katika
uwezekano utumbo wake kutoka nje kwani hutumia nguvu kusukuma choo,”
anabainisha.
Anasema kisababishi kingine kinaweza kuwa uvimbe unaotokea
katika njia ya haja kubwa.
“Mtoto anaweza kupata uvimbe ambao unaweza ukawa ni
saratani au si saratani, lazima afanyiwe uchunguzi mapema ili kumsaidia kwani
akikaa nao muda mrefu ni hatari,” anasema.
Anasema kisababishi kingine ambacho kinadhaniwa kuwa moja
wapo ya sababu zinazochangia mtoto kupata tatizo hilo ni maambukizi ya virusi
viitwavyo kitaalamu Rota Virus.
“Virusi hawa hula baadhi ya seli zilizopo kwenye utumbo
mkubwa (wanazishambulia) matokeo yake utumbo unakuwa unaingiliana, utumbo wa
binadamu umegawanyika katika sehemu nne na kila mmoja haipaswi kuingiliana na
nyingine, zikiingiliana kutokana na kushambuliwa na virusi hivi husababisha
tatizo,” anasema.
Hatua
za tatizo
Daktari huyo anasema ugonjwa huo hupitia hatua kuu nne na
kwamba iwapo mzazi atawahi kumfikisha mwanawe hospitalini ni rahisi kutibu
tatizo katika hatua ya kwanza.
“Katika hatua ya kwanza mzazi au mlezi ataona ule utumbo
unatoka na kurudi ndani wenyewe, sasa anapomleta hospitali mtoto tunamfanyia
uchunguzi kujua nini kinasababisha hali hiyo, tunatibu chanzo kwa kutumia dawa
maalumu na wala anakuwa hahitaji kufanyiwa upasuaji wowote,” anasema.
Anataja hatua ya pili ya tatizo kuwa utumbo unapotoka nje
hushindwa kurudi ndani bila kusaidiwa kuurudisha.
“Yaani mtoto akijisaidia utumbo unatoka nje katika njia
yake ya haja kubwa na hauwezi kurudi ndani hadi mzazi asaidie kuurudisha, bado
katika hatua hii tunaweza kumtibu mtoto bila kumfanyia upasuaji, tunamchunguza
na kutibu chanzo cha tatizo,” anafafanua.
Dk. Bokhary anasema hatua ya tatu huashiria kwamba tatizo
linazidi kuwa kubwa na kwamba utumbo wa mtoto huweza kujitokeza nje hata kama
hakujisaidia.
“Hata akiwa amekaa chini unakuta utumbo wake umejitokeza
wenyewe na wala hajajisaidia haja kubwa, na lazima umsaidie kuurudisha ndani,”
anasema.
Anasema katika hatua ya nne utumbo unapotoka nje huweza kukaa
wiki au mwezi kwani hata unaporudishwa ndani hutoka tena wenyewe.
“Unaona wazi kwamba katika hatua ya kwanza na ya pili ni
rahisi kutibu tatizo kwa kutumia dawa maalumu baada ya kumfanyia uchunguzi wa
kina mtoto husika lakini ikifika hatua ya tatu na nne tatizo linakuwa
limeongezeka hivyo inakuwa lazima tumfanyie upasuaji,” anasema Daktari huyo.
Upasuaji
unavyofanyika
Anasema kuna njia mbili za upasuaji ambazo huzitumia
kumtibu mtoto husika ambazo ni njia ya matundu (Laporascopic-Rectal
Sigmoidopexy na ile ya kufungua sehemu ndogo ya tumbo (Open Rectal-
Sigmoidopexy.
“Lakini tunaweza tusifungue sehemu ya tumbo badala yake
tukashona pale kwenye misuli (iliyopo kwenye sehemu ya haja kubwa) kuikaza kwa
sababu inakuwa imelegea ndiyo maana utumbo hutoka nje,” anasema.
Anaongeza “Au tunafungua kidogo sehemu ya tumbo katika
upande wa kushoto, tunashona ule utumbo kwa ndani kidogo kwa kutumia uzi
maalumu ambao kwa kawaida huwa mgumu.
“Huwa tunashona kwa utaalamu wa hali ya juu, hatugusi hata
kidogo kwenye misuli hivyo mgonjwa huwa si rahisi kuhisi maumivu makali,
maumivu hutokea pale misuli inapoguswa,” anafafanua.
Anasema hata hivyo upasuaji kwa njia ya matundu ni mzuri
zaidi kuliko ule wa kufungua sehemu ya tumbo.
“Kwa njia ya matundu mgonjwa anaweza kuruhusiwa kurejea
nyumbani hata kesho yake baada ya kufanyiwa upasuaji, kwa sababu sehemu ndogo
ya mwili huwa imefunuliwa kutibu tatizo, tofauti na ule wa kupasua lazima akae
wodini kwa uangalizi kwa siku kadhaa,” anasema.
Mama
Daudi
Suala hilo linamshtua Bahati Mwakiborwa Mkazi wa Mbezi ambaye
ni mama wa mtoto mmoja Elius (6), anasema mwanawe aliwahi kutokwa kinyama
sehemu ya haja kubwa.
“Aliwahi kupatwa hali hiyo, si unajua tena huku mtaani huwa
tunapeana ushauri nilikwenda duka la dawa nikanunua dawa fulani ambazo
nilielekezwa, nilimpa kwa muda mrefu lakini tatizo liliendelea.
“Baadae niliamua kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala,
walimfanyia uchunguzi na daktari alimpatia dawa ambazo zilimsaidia,” anasema.
Anasema alifanya uamuzi sahihi kumfikisha mwanawe
hospitalini kwani hali ingekuwa mbaya baadae na kwamba ataendelea kuchunguza
afya ya mtoto wake kwa karibu.
Hali
ipoje Muhimbili
Daktari huyo anasema watoto wengi wanaowapokea wamepata
tatizo hilo kutokana na maambukizi ya kuharisha.
“Wengi hufikishwa general pediatric (kwa Madaktari Bingwa
wa Watoto) wazazi wanakuwa hawajajua watoto wao wanasumbuliwa na nini na
kwanini utumbo unatoka nje.
“Wale wa Pediatric wakiona ni tatizo hilo, ndipo
wanawahamishia kwenye idara yetu ya upasuaji, kwa mwezi tunaona watoto kati ya wanne
hadi watano wanaosumbuliwa na tatizo hilo,” anasema.
Kwanini
kuharisha sababu kuu
Anafafanua kwamba watoto wengi ni rahisi kupatwa na hali
hiyo hasa wale wanaoishi katika mazingira machafu.
“Inaaminika kwamba ukipata tatizo la kuharisha maana yake
umekula kinyesi, sasa watoto wanapocheza hushika vitu vingi, na wengi hupenda
kuweka vidole mdomoni.
“Sasa mazingira yanapokuwa machafu maana yake ni kwamba
anakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi, ni vema mazingira
yakasafishwa kila wakati yawe rafiki kwa watoto ili kuwaepusha,” anasema.
Changamoto
Daktari huyo anasema changamoto kubwa ambayo huweza
kujitokeza baada ya upasuaji kumtibu mtoto mwenye tatizo ni uzi kumsababishia
maambukizi.
“Anaweza kupata ‘infections’ hasa anapofanyiwa upasuaji wa
kufunua sehemu ya tumbo, ndiyo huwa tunalazimika kuwalaza wodini ili tuwape
uangalizi wa karibu hadi kidonda kinapofunga, lakini sasa hivi Muhimbili
tumeanza kufanya upasuaji kwa njia ya matundu ambao tunaona ni salama zaidi,”
anasema.
Chapisha Maoni