NA
VERONICA ROMWALD - DAR ES SALAAM
JICHO
ni sehemu ya mwili inayowezesha kuona, ni ogani inayotambua mwanga na kutuma
taarifa zake kwenye ubongo.
Binadamu ana macho mawili katika sehemu ya uso wake, moja upande
wa kulia na jingine kushoto.
Kila jicho la binadamu lina lenzi moja kama ilivyo kwa
viumbe wengine waliopo katika kundi la mamalia.
Muundo wa jicho huruhusu kuona vitu mbalimbali kama vile rangi,
umbali na mambo mengine mengi.
Pamoja na umuhimu wake mkubwa kwa viumbe hai wakati mwingine macho
hudhurika kwa maradhi mbalimbali.
Kutokana na maradhi mtu huweza kujikuta akipata tatizo la kuona
mbali, karibu na huono hafifu na hatimaye upofu.
Tunashuhudia katika jamii zipo familia ambazo baba, mama hadi
watoto hulazimika kuvaa miwani kuwasaidia kuona karibu au mbali.
Nimemtafuta mtaalamu wa afya na magonjwa ya macho na kufanya naye mahojiano maalum.
Katika makala haya, Daktari Asha Mweke wa Kituo cha Letasi eye
and Optical Centre kilichopo jijini Dar ea Salaam, anaeleza kwa kina juu ya
jambo hilo.
Anasema yapo matatizo ya macho ambayo hurithiwa kutoka kizazi
hadi kizazi na ikiwa wahusika huchelewa kupata matibabu huweza kujikuta
wakipata upofu moja kwa moja.
"Yapo matatizo au maradhi ya macho ambayo yanahusiana na
kurithi, kwa mfano mtoto anapokuwa hawezi kuona mbali kitaalamu inaitwa
myopic...yaani anaweza kuona vitu vya karibu lakini vya mbali hawezi kuona.
"Mara nyingi huhusianishwa na kurithi na ukiangalia
historia utakuta baba au mama yake lazima utakuta mmoja au wote walikuwa na
tatizo hilo na huenda walikuwa wanavaa miwani," anabainisha.
Anasema myopic ndilo tatizo ambalo linahusiana na uvaaji miwani
na ambalo hurithiwa kuliko matatizo mengine ya macho.
"Yaani ni tatizo la huoni hafifu ambapo mtu huwa hawezi
kuona vitu vilivyopo mbali lakini vile vilivyopo karibu anaviona,"
anasema.
Dk. Mweke anasema yapo pia matatizo mengine ambayo hurithiwa
ikiwamo tatizo la glaucoma ('pressure' ya macho) ingawa ni kwa asilimia ndogo.
"Kwa hiyo kabla ya kumtibu mgonjwa ni lazima tufuatilie
historia yake na kwa yule mwenye tatizo la glaucoma lazima tuangalie kwenye
familia kama kuna mtu alipata upofu bila kujitambua na mambo mengine
mengi," anasema.
Anaongeza "Tatizo la glaucoma hurithiwa lakini watu wengi
hawalifahamu tatizo hili na huwa linaleta upofu lakini halina dalili na
wala hauna maumivu.
"Ile 'pressure' ya macho huwa inapanda na matokeo yake huwa
inaua mishipa ya fahamu (optic nerve), mishipa hiyo huanza kufa taratibu
taratibu na mtu ghafla anajikuta haoni au huoni unapotea pole pole,"
anasema.
Daktari huyo anasema hata hivyo ipo aina nyingine ya glaucoma
ambayo yenyewe huja kwa ghafla na ambayo humsababishia mtu maumivu makali
mno upande mmoja wa kichwa.
"Utakuta mtu ghafla anaumwa na kichwa upande mmoja na
kinakuwa kinamuuma kweli kweli na akifanyiwa vipimo anakutwa 'pressure' ya
jicho lake ipo juu.
"Lakini ile ambayo ni 'chronic' yenyewe huanza taratibu na huwa
haina dalili wala maumivu, huhisi chochote lakini uwezo wa kuona hupungua
taratibu taratibu," anasema.
Athari yake
Anasema kitendo hicho husababisha mishipa ya pembeni ya macho
kuanza kufa taratibu na hadi mtu anakuja kujigundua hukutwa tatizo limekua
kubwa na pengine huoni umebaki kidogo sana.
"Huwa ana kiwango kidogo cha kuona inapofika hatua hiyo
kinachofanyika....hupatiwa tiba ya kushusha ile 'pressure' lakini haitasaidia
kuongeza ule uono wake.
"Hata kama atafanyiwa upasuaji, hakuna uwezekano wa
kurudisha ule uoni kama tayari tatizo ishaleta athari kwenye mishipa yake ya
fahamu," anasema.
Mtaalamu huyo akimfanyia uchunguzi mwanafunzi katika moja ya kambi za uchunguzi wanazofanya katika shule mbalimbali
Wanamsaidiaje mgonjwa
Anasema cha kwanza wanachofanya ikiwa 'pressure' ipo juu mgonjwa
hupatiwa dawa ya matone ambayo huiweka kwenye macho yake kwa ajili kuishusha
ili iwe sawa sawa.
"Lakini lazima pia tuangalie hiyo 'pressure' imesababishwa
na nini ndipo tumtibu," anabainisha.
Siri ya kufumba na kufumbua jicho.
Daktari huyo anasema kitendo cha jicho
kufumba na kufumbua (kukonyeza) husaidia kulainisha mboni ya jicho ambayo
haitakiwi kuwa kavu.
“Mboni ya jicho ikiwa kavu inapata
ukungu na hatimaye upofu… machozi husaidia kulainisha mboni ya jicho (cornea),”
anasema.
Anasisitiza “Machozi ni muhimu kwa
afya ya jicho la binadamu na huwa yanapita kwenye vifereji hadi kwenye pua.
Athari ya mishipa
Anasema kitendo hicho cha ‘pressure’ ya jicho kuongezeka
husababisha athari katika mishipa ya fahamu iitwayo ‘optic nerve’.
"Zile optic nerve huanza kuathika, kwa hiyo tiba yake mgonjwa
hupatiwa matone au dawa ambazo ni maalumu za kushusha ile 'pressure'.
“Ni vema mtu akawahi mapema hospitali ili ile ‘pressure’ isije
ikaleta athari kwa sababu itakapoleta athari kwenye mishipa ya fahamu haitaweza
kurekebishika zaidi.
“Yaani kama huoni wako ni hafifu utabaki hivyo hivyo, utapewa tiba
si kwa kukufanya urudi au uweze kuona zaidi isipokuwa utabaki na huono huo huo
ulionao,” anasema.
Dk. Mweke anasema tatizo ni kwamba magonjwa ya macho hatapewi
Kipaumbele na jamii.
“Tunaona kwenye kliniki yetu jambo hili kwa sababu macho yenyewe
si kama tumbo, tumbo linapouma 'likimsokota' mtu atakimbilia hospitali lakini
kwa matatizo ya macho unakuta mtu ana-ahirisha kwenda hospitalini,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo wagonjwa wengi wa macho huensa
hospitalini wakati hali imeshakuwa mbaya.
“Na ikishakuwa mbaya unakuta mgonjwa kwa mfano wa glaucoma
hakuna kitakachomsaidia zaidi ya kushusha ile 'pressure' ikae sawa sawa.
“Tunawapatia ushauri kuhusu huoni wao na kisha tunawapatia rufaa
kwenda kuwaona madaktari waliobobea kutibu tatizo la glaucoma ambako huko pia
hupewa ushauri na matibabu zaidi,” anasema.
Dk. Mweke anasema katika kituo chao wanapokea wagonjwa wenye
matatizo ya macho makundi yote kuanzia watoto hadi watu wazima.
“Wapo ambao wamepata kwa kurithi wengine kutokana na magonjwa
mengine ikiwamo kisukari, shinikizo la damu na mengine.
“Tunashauri jamii kujenga utamaduni wa kupima afya ya macho
angalau mara moja kwa mwaka hii itasaidia kubaini mapema kama wana matatizo
wapate matibabu mapema,” anasema.
Chapisha Maoni