Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MARA kadhaa tumepata kushuhudia mizozo na migogoro
huwa inaibuka katika familia na jamii mtu anapofariki dunia.
Ugomvi huwa nani hasa mwenye haki na anayepaswa
kuuchukua mwili wa marehemu ili kwenda kuupumzisha katika ‘nyumba’ yake ya
milele.
Shida zaidi hujitokeza pindi tu mgonjwa anapofariki
dunia na ndugu zake kuanza kujitokeza kudai mwili wake licha ya kutojitokeza
wakati akiwa mgonjwa.
Ndugu hung’ang’ania kupatiwa mwili wa marehemu huku
ikiwa hakuwahi kuwataja kuwa watu wake wa karibu ambao wanastahili kupatiwa
taarifa zozote kuhusu yeye au hata kuchukua mwili wake kwa maziko ikitokea
amefariki dunia.
Wakili wa Mahakama Kuu aliyebobea katika Sheria ya Matibabu,
Maulid Kikondo ambaye anaeleza jinsi gani jamii inaweza kuepuka migogoro ya
namna hiyo.
“Wakati mgonjwa anaumwa sana, utaratibu wa kawaida
wa hospitali anatakiwa kujaza maelezo maalum ikiwamo kumtambulisha mtu wake wa
karibu anayeweza kuwajibika wakati yeye akiwa hospitalini hapo akipatiwa
matibabu,” anasema.
Anasema mtu huyo anayetajwa ndiye ambaye ikitokea
mgonjwa amefariki hospitali huwajibika kumtumia na hata kumkabidhi mwili wa
marehemu ili aende kuuzika.
“Shida hutokea pale ambapo mgonjwa anapokuja
hospitalini humtaja mtu ambaye hayupo karibu na familia yake labda ni rafiki tu
au jirani ambaye anamuuguza.
“Inapotokea amefariki dunia unakuta ndugu zake
wanaanza kujitokeza kuja hospitalini kutaka kupatiwa mwili wao wakati huo huo
unakuta hawajatajwa kwenye maelezo maalum ya mgonjwa,” anasema.
“Wakati aliyeandikwa anastahili kupatiwa mwili wa
marehemu unakuta ndugu labda wametoka mkoani wameshakuja pale hospitalini na
kuanza kulalamika wakitaka kupatiwa mwili wao, ni changamoto,” anasema.
Mzozo
Anasema inapofikia hatua hiyo mzozo mkubwa
hujitokeza juu hasa nani anapaswa kuchukua mwili ingawa maelezo ya marehemu
yanamtambulisha yule aliyemtaja ambaye ndugu wakati huo wanadai hawamtambui.
“Kisheria huwa ni mgogoro mgumu mno kwa sababu yule
wanayemgombea tayari ni marehemu hawezi tena kuzungumza chochote tujue ukweli
ni upi kati ya hao wanaomgombania,” anasema.
Hatua
Wakili Kikondo anasema inapotokea hali hiyo, ndugu
wanaodai kuwa na uhusiano na marehemu hutakiwa kwenda kuripoti katika ofisi ya
serikali ya mtaa na kuja na vielelezo vinavyoweza kuthibitisha uhalali wa wao
kupatiwa mwili wa marehemu.
“Lazima walete vithibitisho kutoka serikali ya mtaa
vitatusaidia sisi kutambua ikiwa kweli si mtu anayetaka kuchukua mwili wa
marehemu kwa ajili ya matumizi yake binafsi na ana nia nzuri kweli,” anasema Wakili Kikondo (pichani).
Anaongeza “Kwa sababu kule mtaani wanamtambua
kwamba ni ndugu halali wa marehemu na kweli ana uwezo wa kuhimili zile taratibu
zote zinazohitajika kufanikisha jambo hilo.
“Hata hivyo bado na sisi (wanasheria) huwa ni
jukumu letu pia kutambua kwamba yale maelezo yao ni ya kweli au si kweli
inabidi na wewe utafute uthibitisho juu ya hayo waliyoeleza.
“Kwa hiyo huo si mzozo rahisi, mwenyewe (marehemu) angekuwapo
angesema ukweli wa mambo lakini haiwezekani,” anasema.
Mgogoro
na hospitali
Anasema mizozo ya kugombea mwili wa marehemu huweza
pia kusababisha mgogoro kati ya familia ya ndugu wanaodai kuwa na uhusiano na
marehemu na hospitali husika.
“Unakuta mtu anayejitokeza kuchukua mwili wakati
mwingine hajawahi kujitokeza hata siku moja, kwa mfano unakuta mtu amefariki
Dar es Salaam na ndugu zake wanaishi Mwanza.
“Ndugu hao hawajawahi kutokea hata siku moja kuja
hospitalini na unakuta ameuguzwa na rafiki yake sasa aliyeandikwa ni huyu
anayemuuguza akifariki ndugu wanakuja.
“Unakuta ni wageni hata wauguzi hawawatambui wala
mtu yeyote pale hospitali na wala hata mmoja wao hatajatajwa kwenye maelezo ya
marehemu na wanang’ang’ania wapewe mwili na waongoze kila kitu wao,” anasema.
Anafafanua mara nyingi katika karatasi ya maelezo
huwa anaandikwa mtu mmoja lakini ikiwa mgonjwa ataeleza maelezo ya tofauti
wanaweza kumpa nafasi au kwenye ile faili anaweza daktari akaeeleza japo
ametajwa fulani lakini mtu huyo bado ana ndugu wa kumsaidia.
“Unakuta hakuna maelezo ya ziada, inapofikia hapo…
ndugu wengi hudhani viongozi wa hospitali huwa wanafanya vile kwa kuwasumbua
jambo ambalo si kweli, kiuhalisia hospitali kama taasisi haiwezi kurahisisha
maamuzi kama ambavyo mtu hutaka iwe.
“Lakini ikiwa mtu (marehemu) mwenyewe amemtambulisha
fulani kwamba ndiye anayemtambua kama mtu wake wa karibu na hajakutaja wewe
kama mzazi au ndugu wa kuzaliwa naye, wao wana haki ya kufuata maelezo
yaliyotolewa,” anasema.
Nini
kifanyike
Wakili huyo anasema ili kupunguza matatizo ya namna
hiyo kujitokeza kwenye jamii ni muhimu mno watu kuandikisha watu wao wa karibu
na si vinginevyo.
“Ni vema kumtaja mtu ambaye anastahili
kushughulikia matatizo yanayokukabili wakati wa ugonjwa na ambaye atapaswa na
ataweza kusaidia kuhifadhi vema mwili wako ikiwa utafariki dunia,” anasisitiza.
Anaongeza “Kwa sababu inapotokea wakati mwingine
mtu anayetajwa mule wanatofauti kubwa mno kimtazamo hadi imani ya dini, wakati
mwingine huleta shida kwani huwa hawezi kufuata taratibu za mazishi kulingana
na dini ya marehemu.
“Hivyo ni muhimu kuandika mtu unayemuamini ili hata
ikitokea umepata shida na unahitaji upasuaji kwa mfano huku ukiwa huwezi kuzungumza
basi mtu huyo kwa mujibu wa taratibu huruhusiwa kusaini badala yako ili
ufanyiwe upasuaji husika.
“Hivyo, hakikisha unamuandika mtu ambaye ni wa
karibu na familia yako, anajulikana lakini pia ana uwezo wa kutimiza wajibu
wake kwako,” anasema.
Wosia
wa maziko
Anasema inashauriwa mtu anapokuwa katika hali ya
ugonjwa ana haki ya kuandika wosia wa maziko yake.
“Mgonjwa anaruhusiwa kuandika ikiwa imetokea
amefariki anawataja wale ambao wanaweza kushiriki katika maziko yake ipasavyo,
hata wauguzi wamefundishwa jinsi ya kusimamia hayo mambo,” anasema.
Anaongeza “Watu wamezoea kwamba wosia lazima
uhusishe mali zake zote lakini si kweli, unaweza kuandika wosia ukifariki dunia
nani asimamie maziko yako.
“Na mali zingine ambazo hazijatajwa kwenye wosia
huo zinaweza kuamriwa kwa kuzingatia sheria zingine zilizopo, na inashauriwa ni
vizuri unapotaka kuandika wosia ukamshirikisha muuguzi au daktari wako.
“Unaweza kumueleza kwamba hali yako si nzuri na
unahitaji kuandika watu ambao wanaweza kuhusika moja kwa moja ikitokea
umefariki dunia,” anasema.
Si
uchuro
Wakili huyo anasema jamii inapaswa kuondokana na
imani potofu kwamba kuandika wosia ni ‘kujiombea’ kufariki dunia mapema.
“Kufa hakuna dalili, unaweza kuwa mzima ukafa na
ukawa mgonjwa pia ukafa, kwa hiyo suala la kuandika wosia ni suala la msingi
mno katika maisha yetu.
“Na linasisitizwa mno kwa sababu migogoro mingi
inayotokea kwenye jamii, mtu baada ya kufariki watoto na wananyanyasika
inajitokeza kwa sababu wengi wanafariki na hawaachi maelezo ya msingi,”
anasema.
Anaongeza “Matokeo yake watu wanajitokeza wanadai
kumbe hawadai au mtu anajitokeza anaamua mali za marehemu ziuzwe na ukiacha
hayo kuna baadhi ya familia ama mama au baba anakuwa anamiliki mali ambazo
hazijulikani.
“Inapotokea umefariki ghafla ile mali inapotea
unakuta yule mnayejuana labda ni fundi alikuwa anasimamia basi anajimilikisha
labda awe mwaminifu sana aweze kuirudisha kwenye jamii (familia).
Wengi
hukosea
Anasema ingawa watu wengi huandika wosia lakini tatizo
ni kwamba hawazingatii taratibu za kisheria.
“Kwa sababu ile sheria inayoelekeza jinsi ya
kuandika wosia inatoa taratibu kwamba yule anayeandika wosia lazima ajue kusoma
na kuandika na lazima awe na mashahidi wawili ambao watashuhudia wakati
akiusaini.
“Lakini unakuta mtu anaandika wosia akiwa peke yake
anausaini halafu akishausaini anatafuta mashahidi wawili ili wamsainie hiyo
haitakiwi kisheria,” anasema.
Anaongeza “Inatakiwa wakati wewe unasaini wale
mashahidi nao wawe wanashuhudia ukiweka hiyo saini na hata watakapoitwa kwenye
mizozo mahakamani swali kubwa watakaloulizwa ni kwamba je walikushuhudia
ukisaini huo wosia, yule wa kwanza atajibu ndiyo kadhalika na wa pili.
“Lakini kama yule anayeandika wosia hajui kusoma
wala kuandika hapo huwa kuna shida, inabidi sasa mashahidi wake wawe watano na
mara nyingi hushauriwa kwamba shahidi mmoja awe miongoni mwa ndugu na ikiwa ni
ya kimila inashauriwa mume au mke awe sehemu ya ushahidi.
“Lakini pia ni muhimu kuepuka mno mashahidi kuwa
warithi kwa sababu wakati mwingine wosia unaweza kuwa chanzo cha migogoro katika
familia.
Mfano
hai
Anasema katika kitabu cha ‘The Law’s
Empire’ kinaelezea kuhusu kesi ya babu mmoja aliyetaka kumrithisha mali mjukuu
wake.
“Babu huyo aliamua kuoa lakini kwa kuwa mjukuu wake
alijua kwamba yeye ndiye mrithi basi akapata hofu kwamba mwanamke aliyeolewa na
babu yake atachukua ule urithi wake.
“Basi aliona njia rahisi ni kumuua babu yake ili
arithi mapema zile mali hata hivyo hilo lilijulikana na mjukuu huyo
hakurithishwa zile mali za babu,” anasema.
Anaongeza “Tangu hapo, ikatungwa kanuni ya kisheria
kwamba mtu hawezi kunufaika kwa makosa yake mwenyewe, hasa inapojulikana kwamba
mtu ameua ili arithishwe.
Ni
siri
Anasema ili wosia uheshimike unapaswa kutunzwa,
mahakama kuu, kwa wakili wako au katika taasisi maalum.
“Inapofika hapo ndiyo maana mmoja wa mashahidi awe
mtu wa familia ili aweze kusimamia wosia wako pindi utakapofariki dunia,”
anasema.
Anasema hata hivyo huwa zinahitajika gharama kidogo
katika kuutunza wosia husika na huwa zinategemea nani anakuandikia na wewe
unayeandikiwa vitu vyako ni kiasi gani na vipo wapi na wapi.
“Kuna wakati pia hutegemea wengine huwa
wanaandikiwa bila kulipia gharama yoyote, inategemea na mali za muhusika,”
anasisitiza.
Makala haya yametoka Februari 8, 2018 katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia.
Chapisha Maoni