Picha na mtandao
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
UJAUZITO
wa Miriam James mkazi wa Dar es Salaam ulipatwa na misuko suko mingi, ulipofikisha
umri wa miezi mitano ulionesha dalili za hatari.
Miriam
anasema ujauzito wake ulitaka kuharibika katika kipindi hicho alikuwa
akisumbuliwa mno na mamumivu ya tumbo mara kwa mara.
“Tuliogopa,
ilipofika miezi saba mume wangu aliona vema nije huku Muhimbili ili madaktari
waniangalie kwa ukaribu, nililazwa wodini (baby rest),” anasema.
Anasema
bado aliendelea kupata maumivu ya tumbo madaktari wake wakashauri ni muhimu
afanyiwe upasuaji ili kumtoa mtoto.
“Hivyo,
nilijifungua mtoto njiti… nilikaa mno wodini nikiendelea kujiuguza na wakati
huo madaktari wakiendelea kumuhudumia mtoto wangu.
“Wasiwasi
wangu mkubwa ulikuwa juu ya kupona kwake… alikuwa mdogo mno, namshukuru Mungu,
madaktari walijitahidi kumuhudumia na afya yake iliimarika tukaruhusiwa kurejea
nyumbani,” anasema.
Anaongeza
“Si kazi rahisi kulea mtoto njitii, inahitaji moyo wa uvumlivu, wakabiliwa na
matatizo mengi, kuna kipindi huwa anaishiwa damu mara kwa mara hivi sasa
ametimiza mwaka mmoja na miezi saba.
Jinsi ilivyo
Kibaiolojia
mtoto huishi ndani ya tumbo la mama kwa kipindi cha miezi tisa tangu kutungwa
mimba hadi kuzaliwa kwake.
Lakini
wakati mwingine huweza kutokea mtoto akazaliwa kabla ya kipindi hicho
kukamilika wengi wetu tunawaita watoto njiti.
“Mara
nyingi ngozi yao huwa haijakomaa. Ingawa viungo vyote vya ndani ikiwamo moyo,
figo, ini, mapafu na vinginevyo huwa vimeumbwa tayari ila navyo huwa bado
havijakomaa,” anasema Daktari Bingwa wa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Robert Moshiro.
Anafafanua
“Kwa kawaida mtoto hukamilika kuumbwa viungo vyake ndani ya wiki 24 tangu mimba ilipotunga lakini zile ogani za
ndani huwa bado hazijakomaa.
“Viungo
hivyo hukomaa katika zile wiki 12 za mwisho za ujauzito, mtoto huendelea
kupokea virutubisho vyote muhimu kutoka kwa mama yake ili kuwezesha kukamilika
kwa viungo vyake,” anabainisha.
Anasema
baada ya kumalizika kwa wiki hizo 12 za mwisho za ujauzito hapo mtoto huwa na
uwezo wa kupumua mwenyewe kwa sababu tayari mapafu yake huwa tayari
yamekamilika vema.
“Kila
kiungo hufanya kazi yake sawa sawa hata figo zake huwa zinakuwa na uwezo wa
kuchuja vizuri kwani zimekamilika,” anasema.
Anasema
lakini ikiwa mtoto atazaliwa kabla ya muda huo kukamilika hukabiliana na
matatizo mengi kwani viungo vyake vinakuwa bado havijakomaa.
Dk.
Moshiro anasema hali hiyo hutokea kwa sababu anakuwa amekuja kwenye mazingira ambayo
anakuwa hawezi kukabiliana nayo.
Hali mbaya zaidi
“Kwa
mfano mtoto aliyezaliwa kabla ya muda (njiti) huku akiwa chini ya kilo moja
ndani ya siku tatu (tangu azaliwe) mishipa yake ya damu huwa ni laini sana.
“Hivyo,
huwa kwenye uwezekano mkubwa wa kuvuja damu na hata mishipa yake kupasuka au
kuvilia damu.
Matatizo ya ubongo
Anasema
hali hiyo ikiwa itatokea kichwani huweza kusababisha ubongo wa mtoto kushindwa
kufanya kazi inavyotakiwa.
“Ubongo
wa mtoto huwa una-fail… matokeo yake anaweza kupoteza maisha kabisa au ikiwa
ataishi basi anakuwa na matatizo ya ubongo katika maisha yake,”
anabainisha.
Madhara mengine
Daktari
huyo anasema watoto wengine hupata matatizo mbalimbali kama vile ya usikivu
(uziwi), ulemavu wa kudumu wa kuona na mengineyo.
“Lakini
wakati mwingine matatizo hayo huweza kutibika ikiwa yatagundulika mapema,”
anabainisha.
Anaongeza
“Anapozaliwa kabla ya muda zile chembechembe za damu ambazo husaidia kinga ya
mwili huwa nazo bado hazijakomaa.
“Kutokana
na hali hiyo huwa anakuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya
vijidudu.
“Maambukizi
hayo huweza kumsababishia kupata homa ya uti wa mgongo, ambayo huenda pia
kuharibu ubongo,” anasisitiza.
Anasema
mtoto aliyezaliwa kabla ya muda huwa pia yupo kwenye uwezekano mkubwa wa kupata
homa ya manjano.
“Kwa
sababu ini lake huwa bado halijakomaa hivyo hushindwa kuondoa ile manjano na
ikiwa itaenda kwenye ubongo huuharibu kabisa,” anasema.
Anaongeza
“Huwa kunajitokeza changamoto nyingi mno… unaweza kujitahidi kwa kila namna
kumtunza mtoto lakini matatizo haya yakaja kujitokeza katika
kipindi
cha ukubwani.
Umri wa mimba
Anasema
matatizo mengi yanayowakabili watoto waliozaliwa kabla ya muda mara nyingi
huendana na umri wa mimba.
“Yaani,
kwa mfano mtoto akizaa katika wiki 34 ya mimba maana yake anakuwa amebakiza
wiki nne afike mwisho, mtoto huyu huwa na tofauti kubwa na mtoto
atakayezaliwa
katika wiki 28 ya mimba.
“Hivyo,
matatizo atakayoyapata mtoto atakayezaliwa katika wiki 28 ni makubwa zaidi
kuliko ya mtoto atakayezaliwa wiki 34,” anasema Dk. Moshiro.
Hula kwa shida
Anaongeza
“Jinsi ya kumlisha mtoto aliyezaliwa kabla ya muda nayo ni changamoto kubwa
hasa aliyezaliwa katika kipindi cha wiki 28.
“Mara
nyingi hawa ule mfumo wao wa chakula huwa nao haujakaa vizuri (haujakomaa)
kuweza kumeng’enya maziwa ya mama, kwa sababu alikuwa lazima
aendelee
kutegemea kondo la mama kupata chakula.
“Lakini
akishazaliwa tunakuwa hatuna jinsi lazima tumlishe chakula… huwa tunawaangalia
jinsi wanavyoweza kupokea yale maziwa akipokea vizuri tunaendelea kumpa,”
anasema.
Anasema
lakini hatua hiyo huwa inamuweka mtoto kwenye uwezekano wa kupata matatizo
ikiwamo kuoza utumbo.
“Hii ni
kwa sababu ule mfumo wake unakuwa haujakomaa… na ili uweze kuimarika huweza
kuchukua hata wiki nzima,” anabainisha.
Mama huathirika
Anasema
kutokana na changamoto hizo ambazo mtoto hukabiliana nazo mara nyingi
humsababishia mama naye kuathirika kwa namna moja au nyingine.
“Kwanza
jamii huwa inamchukulia tofauti, wapo watakamnyooshea kidole kutokana na
kujifungua mtoto kabla ya muda,” anasema.
Anasema
hali hiyo huweza kumsababishia mama kupata msongo wa mawazo tena hasa anapokuwa
akitafakari juu ya uwezekano wa mtoto wake kupona.
“Kwa sababu
wengi wanajua mtoto aliyezaliwa kabla ya muda huwa na uwezekano wa kufariki
dunia wakati wowote, huwa tunatumia nguvu kubwa kuwatuliza,” anabainisha.
Anaongeza
“Kwa sababu akiwa na msongo wa mawazo, maziwa yanakuwa hayatoki kutosheleza
mahitaji ya mtoto na watoto hawa huwezi kuwapa chakula kingine
zaidi ya
maziwa ya mama pekee.
“Kusema
ule ukweli, wakina mama hawa (wanaojifungua watoto kabla ya muda) huwa wanapata
shida mno, mara nyingi huwa wanalazimika kukaa muda mrefu
wodini.
“Ule muda
anaokaa hospitalini ni mwingi kwa mfano unakuta analazimika kukaa hadi wiki
sita tangu ajifungue ikiwa mtoto amezaliwa na kilo moja.
“Mtoto
wake akiendelea vema huyo atakaa kidogo kama miezi miwili hadi mitatu
tunamruhusu kurudi nyumbani lakini kama haendelei vizuri ataendelea kukaa
wodini tukiangalia hali yake na mtoto wake,” anasema.
Daktari
huyo anasisitiza kwamba kupona au kutokupona kwa mtoto mara nyingi hutegemeana
na umri wake tangu alipozaliwa.
Takwimu
Anasema
kwa kawaida asilimia 20 hadi 25 pekee ya watoto ambao huzaliwa kabla ya muda
wakiwa na kilo moja huwa wanapona.
“Hata
hivyo, ukienda sehemu ambayo hakuna huduma za kibingwa kwa ajili ya kuhudumia
watoto hawa kama ilivyo hapa Muhimbili tatizo huwa ni kubwa zaidi,” anasema.
Anasema
watoto waliozaliwa kabla ya muda wakiwa na zaidi ya kilo moja uwezekano wa
kupona nao huongezeka.
“Asilimia
40 hadi 50 huwa wanapona, na wale waliozaliwa juu ya hapo huwa wanapona vizuri
kabisa hasa wale wenye kilo mbili na zaidi,” anabainisha.
Anaongeza
“Hii ni tofauti na watu wengi kwenye jamii wanavyoamini… hakuna ukweli wowote
kwamba mtoto akizaliwa mimba ikiwa katika mwezi wa nane anafariki na kwamba
Yule anayezaliwa katika mwezi wa saba anaishi.
“Ukweli
ni kwamba anayezaliwa katika mwezi wa saba wa mimba ana uwezekano mkubwa zaidi
wa kufariki dunia kuliko yule aliyezaliwa katika mwezi wa nane wa mimba,”
anabainisha.
Majanga
Dk.
Moshiro anasema changamoto kubwa ambayo wanaiona ni kina mama wengi kushindwa
kujua umri wa mimba.
“Tanzania
hii ni changamoto, kina mama wengi hawajui umri wa mimba… na si kina mama wote
wanafanikiwa kufanya ultra sound.
“Kipimo
hicho kinaweza kutusaidia kujua umri wa mimba ikiwa kitatumika kwa uchunguzi
katika wiki ya 18.
“Ndiyo
maana tunshauri kina mama kuwahi kliniki wanapojihisi kuwa huenda wana ujauzito
lakini wapo ambao huja hospitalini tayari na hali ya uchungu unakuta kumbe
walipitiliza mwezi bila kujua,” anabainisha.
Hali halisi MNH
Katika
kipindi cha mwaka 2016/17 watoto wachanga wapatao 7,372 walilazwa katika katika Kitengo cha Watoto Wachanga Muhimbili.
Kati ya
watoto hao njiti walikuwa 1,313 sawa na asilimia 31.4.
Idadi ya
watoto njiti waliofariki katika kitengo hicho kwa mwaka 2016/17 ni 543 sawa na
asilimia 7.4 ukilinganisha na asilimia 19.8 ilivyokuwa mwaka 2015/16.
Watoto
njiti 65 walipatiwa dawa ya kukomaza mapafu katika mwaka 2016/17 huku idadi ya
watoto waliolazwa kwenye wodi ya kangaroo mwaka 2016/17 ikiwa 483.
Idadi hiyo
imeongezeka kutoka mwaka jana ambayo walikuwa watoto 399.
Takwimu
hizo zilitolewa Novemba 17, mwaka huu na Mkurugenzi wa Tiba Muhimbili, Dk.
Hedwiga Swai wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani.
Dk. Swai
anasema idadi ya watoto waliolazwa kwenye wodi ya kangaroo walikuwa kati ya
gramu 500 na kilo 1.5.
“Idadi
kubwa ya watoto waliotunzwa katika wodi hiyo walifanikiwa kutoka wodini na
uzito wa kilo 1.6 hadi 1.7 ambayo ni sawa na asilimia 99.5 ya watoto wote
waliokuwa wamelazwa,” anasema.
Anasema
hayo ni mafanikio makubwa waliyopata katika kipindi cha mwaka mmoja hasa
kupunguza idadi ya vifo vya watoto hao.
“Tumepata
mafanikio makubwa kwa kuwapo huduma ya kangaroo, tumeweza kupunguza idadi ya vifo
kutoka asilimia 19.8 mwaka jana hadi kufikia asilimia 7.4, vifo vya ghafla
kutokana na kupaliwa maziwa navyo vimepungua kwa asilimia 99.
“Muda wa
kukaa wodini nao umepungua pia ukilinganisha na wale wanaokaa kwenye incubator,
kwa kangaroo watoto hupata nafuu haraka kuliko wale waliokaa kwenye incubator.
“Kwa njia
ya kangaroo mtoto hunyonya kwa ukaribu na huwa faraja kubwa kwa mama, tumeweza
kupunguza msongamano wa watoto katika wodi yetu,” anabainisha.
Changamoto
Anasema
ni upungufu wa vifaa tiba ukilinganisha na idadi ya watoto wanaopokea na kwamba
hiyo inatokana na huduma ya kangaroo kutokutewa katika hospitali nyingine.
“Ufinyu
wa wodi ya kangaroo ukilinganisha na idadi ya watoto ikizingatiwa wengi kwa
sasa wana uwezo wa kuishi hata wale wenye kilo ndogo kama vile gram 700,”
anasema.
Anataja
changamoto nyingine kuwa ni gharama kubwa ya kununulia dawa za kukomaza mapafu
na idadi ndogo ya wauguzi na madaktari ukilinganisha na idadi ya watoto.
“Tunatoa
wito kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongeza
vitengo vya kutunzia watoto njiti katika hospitali nyingine kwani huduma hii ni
rahisi, haihitaji gharama kubwa na imeweza kupunguza vifo vya watoto njiti kwa
asilimia kubwa,” anasema.
Wizara
Mkurugenzi
wa huduma za Kinga wa Wizara hiyo, Dk. Neema Rusibamayila anasema takwimu
zinaonesha asilimia 13 hadi 17 ya watoto nchini huzaliwa njiti.
“Hivyo,
serikali kupitia Wizara hii imekuwa ikiratibu program mbalimbali lengo ni kupunguza
idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale walio chini ya umri wa miaka mitano.
“Program
hizo ni pamoja na kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kupanua huduma za
watoto wachanga kwa kujenga wodi katika hospitali za Manispaa na Wilaya na
kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya namna ya kuhudumia watoto wachanga
(essential newborn care),” anasema.
Anaongeza
“Ingawa program hizi zimekuwa na mafanikio makubwa bado tuna changamoto
kuhakikisha tunazidi kupunguza zaidi idadi ya vifo hivi.
Chapisha Maoni