Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Dk. Nyangassa (kushoto) akishirikiana na wenzake kumfanyia upasuaji mgonjwa mwenye ugonjwa wa moyo, Picha na mtandao

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MADAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Open Heart International (OHI) wamewapa mbinu mpya wenzao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ya kutibu magonjwa ya moyo.

Kwa kutumia mbinu hiyo waliyowapa sasa JKCI wataweza kufanya upasuaji ndani ya muda mfupi zaidi kuliko hapo awali.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Upasuaji, Bashir Nyangassa ameueleza mtandao huu kwamba kwa kutumia mbinu walizopatiwa za kisasa wanaweza kufanya upasuaji uliohitaji saa tatu, ndani ya saa mbili.

"Yaani kwa mfano ikiwa upasuaji ulihitaji kufanyika kwa saa tatu hadi kukamilika, sasa tunaweza kufanya kwa saa mbili na tukaukamilisha, tunawashukuru mno OHI," amesema.

Amesema tangu Machi 19, mwaka huu wamekuwa wakifanya upasuaji kwa watoto na watu wazima wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo na kwamba kambi hiyo inatarajiwa kukamilika Machi 24, mwaka huu.

"Tumekusudia kuwafanyia upasuaji watoto 50 na watu wazima 30 wenye magonjwa ya moyo, hadi leo tumeshawafanyia 19 ambapo kati yao watoto ni 11 na watu wazima wapo saba," amesema.

Amesema kesho wanatarajia tena kuwafanyia upasuaji wagonjwa wengine wanne.

"Tunashukuru wenzetu wa damu salama awamu hii hatukupata changamoto ya damu... tunapata ya kutosha, umeme nao haujatupa changamoto," amesema.

Amesema ikiwa watakamilisha idadi hiyo ya wagonjwa watakuwa wameokoa kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 500 ambazo serikali ingezitumia kama wangepewa rufaa kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa OHI, Dareen Wolfers alisema wamefanya kazi hiyo kama timu moja kwani lengo kuu ni kuokoa maisha.

“Kabla ya upasuaji huu tulikuwa na wiki moja ya mafunzo ya pamoja, tumejifunza wenzetu wanafanya vema na siku za usoni JKCI itakuwa Taasisi kubwa inayotibu magonjwa ya moyo si tu Tanzania bali Afrika kwa ujumla," amesema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement