*Fedha hizo zimetoka
katika Chama cha Tiba ya Saratani cha nchini Marekani.
Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Taasisi ya Saratani
Ocean Road (ORCI) hivi karibuni imeshinda msaada wa fedha za utafiti na ubunifu
kutoka Chama cha Tiba ya Saratani cha Nchini Marekani (ASCO) kupitia shindano
lijulikanalo kama (International Innovation Grant – IIG).
Hatua hiyo ni kwa
ajili ya kutekeleza mpango wa kinga ya saratani ya ngozi kwa watu wenye ulemavu
wa ngozi nchini Tanzania.
Daktari Fidel Rubagumya
ambaye ni mfanyakazi wa Idara ya Taaluma na Utafiti ya ORCI ndiye ambaye
aliomba fedha hizo za utafiti mwaka 2017 katika shindano hilo la kimataifa
lililotangazwa na ASCO.
Desemba, 2017 ORCI
ilitangazwa mshindi wa fedha hizo kwa ajili ya utafiti na ubunifu ikiwa ni
taasisi pekee Barani AAfrika kushinda kwenye shindano hilo, taasisi nyingine
mbili zilizoshinda ni kutoka nchi za Mexico na India.
Akizungumza na mtandao huu
mapema leo, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI (Pichani), Dk. Julius Mwaiselage amesema mradi
huo wa utafiti wenye jina la ‘Use of Smartphone application for early
detection of skin cancers in people with albinism’ unalenga kupunguza matukio
ya ugonjwa na vifo vitokanavyo na saratani ya ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi
nchini kwa kupitia simu zinazotumia teknolojia ya kisasa.
Amesema kila mwaka, ASCO
kupitia IIG, huitisha mapendekezo ya mawazo bunifu ya utafiti yanayolenga
kuboresha matibabu ya saratani kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati
ambayo yataweza pia kufanyiwa kazi katika mazingira yanayofanana kwenye nchi
nyingine zinazoendelea.
“Mradi unaofadhiliwa kwa
msaada huu wa fedha za utafiti utaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja
utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya ORCI na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa
Ngozi Nchini Tanzania (TAS).
“Ni matarajio yetu kwamba
mafanikio ya mradi huu hapa Tanzania yatasaidia utekelezaji wa mradi kama huu
kwenye nchi nyingine Barani Afrika zinazopambana na tatizo la saratani ya ngozi
miongoni mwa watu wenye ulemavu wa ngozi,” amesema.
Amesema utafiti wa ORCI unaonesha
kwa mwaka 2016 pekee kulikuwa na wagonjwa wapya 177 wa saratani ya ngozi, na
95% ya wagonjwa hao ikiwa ni watu wenye ulemavu wa ngozi.
“Kutokana na udhaifu katika
ngozi zao, pamoja na kuchangiwa na kuchomwa na mionzi mikali ya jua, wengi wa
watu wenye ulemavu wa ngozi wataathiriwa na saratani ya ngozi iwapo hatua
maalum za kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo hazitochukuliwa.
“Kwa kuzingatia hilo,
uchunguzi na kugundulika kwa saratani ya ngozi ikiwa katika hatua za awali
itakuwa ni njia kuu ya kuhakikisha kuwa wagonjwa wa saratani ya ngozi
wanagundulika mapema na wanapewa rufaa ya kwenda ORCI ili kuanza matibabu
haraka iwezekanavyo.
“Utaratibu
uliozoeleka hapo awali katika kuchunguza saratani ya ngozi unakabiliwa na
changamoto za huduma hizo kuwa mbali na jamii na ucheleweshaji wa rufaa kwa
wagonjwa kwenda hospitali kupata matibabu.
Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi akiandikishwa jina lake kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya saratani ya ngozi hivi karibuni katika Taasisi ya Ocean Road wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani.
"Hivyo basi utaratibu huu mpya wa kutumia simu za mkononi tutahakikisha kuwa huduma za uchunguzi zinapatikana kwenye jamii husika kwa kutumia mbinu ya kupiga picha vidonda vilivyoleta mashaka kwenye ngozi na kuzituma kwa madaktari.
"Program hii ya simu za mkononi itasaidia kupiga picha za vidonda vilivyoleta mashaka kwa kuambatanisha na maelezo binafsi ya mgonjwa kisha kuzihifadhi picha hizo kwa njia ya mtandao," amesema Dk Nazima Dharsee, Mkurugenzi wa Idara ya Taaluma
na Utafiti, ORCI.
Ameongeza “Picha hizo zitachunguzwa
mtandaoni na wataalamu wa ngozi na saratani, kisha kufanyiwa uchunguzi zaidi wa
kitabibu. Wagonjwa watakaogundulika kuwa na vidonda visivyo vya kawaida
watapelekwa hospitali kuthibitisha kama wameathiriwa na saratani ya ngozi,
ambapo watakaokutwa na tatizo hilo watapewa matibabu stahiki.”
Chapisha Maoni