Baadhi ya vyombo vya kulia chakula.
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WATU wanaogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa
wa Kifua Kikuu (TB) wamekuwa wakinyanyapaliwa
kwenye jamii, ikiwamo kutengewa vyombo vyao maalum vya chakula.
Imeelezwa hatua hiyo huchukua kwa hofu ya kupata
maambukizi ya ugonjwa huo hata hivyo dhana hiyo si sahihi kwani TB haiambukizwi
kupitia vyombo vya chakula.
Akizungumza Dar es Salaam juzi katika mafunzo ya
siku moja kwa waandishi wa habari za afya yaliyolenga kuwajengea uwelewa kuhusu
ugonjwa huo, Mfuatiliaji wa Tathmini wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Zuweina Kondo alisema huambukizwa kwa njia ya hewa.
“Jamii bado haina uwelewa wa kutosha juu ya namna
TB inavyoambukizwa, ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya hewa na si vyombo vya
chakula.
Inashauriwa uwahi hospitalini kwa uchunguzi ikiwa unakohoa kwa zaidi ya wiki mbili.
“Kibaya zaidi ni kwamba mtu hutengwa pale tu
anapogundulika lakini kabla ya kugundulika huwa wanashirikiana naye bila
wasiwasi wowote.
“Jambo hili si sahihi, kimsingi mtu ambaye
amegundulika kuwa na maambukizi na ameanza matibabu anakuwa salama na unaweza
kushirikiana naye vyombo vya chakula.
“Kibaya ni kwamba mtu mwenye maambukizi ambaye hajagundulika ili kuanza matibabu ndiye anakuwa na uwezo wa kuambukiza wenzake TB,” alisema.
Alisema kitendo cha wale waliogundulika kuwa na
maambukizi ambao wameingizwa kwenye mfumo wa matibabu kutengwa na
kunyanyapaliwa kinafanya wengine kuwa na hofu ya kufanya uchunguzi juu ya afya
zao.
“Wanaogopa watatengwa na hii ni changamoto katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania ipo miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa ya TB,” alisema.
Alisema ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2017 inaeleza kiwango cha maambukizi ya TB nchini ni wastani wa watu 287 katika kila watu 100,000, sawa na wagonjwa 160,000 kila mwaka.
“Lakini ripoti yetu ya mwaka 2016 inaeleza katika
mwaka huo pekee tuliweza kugundua na kuwaingiza katika mfumo wa matibabu watu
64,000 sawa na asilimia 40,” alisema.
Alisema asilimia 90 ya watu wanaogundulika kuwa na
maambukizi hayo na kupatiwa matibabu mapema hupona hata hivyo changamoto ni
namna ya kuipata asilimia 60 ya wagonjwa iliyobakia.
Alisema kulingana na ripoti hiyo ya WHO ya mwaka
2016 inakadiriwa ya watu bilioni mbili duniani wanaishi na maambukizi ya
ugonjwa huo duniani.
“Ni ugonjwa ambao unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa
ya wagonjwa kwa upande wa magonjwa ya maambukizi (yanayosababishwa na vimelea) kuliko hata
Ukimwi kulingana na WHO,” alisema.
Chapisha Maoni