NA VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA MOROGORO
Mei 5, mwaka huu Tanzania iliungana na mataifa mengine
duniani kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo kwa mwaka
huu yalipewa Kauli mbiu isemayo 'Wakunga ni Chachu katika Utoaji Huduma bora kwa mama na mtoto'.
Tanzania iliadhimisha siku hii ya pekee, maadhimisho hayo
yalifanyika huko mkoani Morogoro katika viwanja vya sabasaba.
Upo msemo wa wahenga usemao, usitukane wakunga na uzazi
ungalipo, msemo huu unalenga kuhamasisha jamii kumthamini mkunga kulingana na
nafasi yake ‘nyeti’ aliyonayo.
Mkunga ni mtu muhimu
mno katika kusaidia kufanikisha kuanza kwa safari ya mwanadamu duniani,
huhitajika katika kusaidia na kufuatilia hali ya mama tangu anapogundulika kuwa
mjamzito, kipindi cha ujauzito na hadi kujifungua.
Hata baada ya mama
kujifungua mkunga huendelea kufuatilia hali yake na mtoto au watoto waliozaliwa
hadi wanapofikisha kipindi cha umri wa miaka mitano.
Ili kufanikisha
safari hiyo salama mama anapaswa kuanza kuhudhuria kliniki pindi tu anapojihisi
kuwa ni mjamzito, ili afya yake na maendeleo ya mtoto aliyepo tumboni
ifuatiliwe kwa ukaribu na watumishi wenye ujuzi.
Wapo ambao wanaufananisha uhai wa mwanadamu na ‘bidhaa adimu’ ambayo kamwe mtu hawezi kuipata
popote duniani akainunua.
Ni zawadi maalum na
ya pekee ambayo Mwenyezi Mungu humjalia kila mmoja kwa mapenzi yake.
Kibaiolojia
wataalamu wa afya wanasema uhai wa mwanadamu huanza rasmi pale tu mbegu ya baba
inaposafiri hadi kukutana na yai la mama na kutunga mimba, baada ya kujamiiana.
Wanasema suala la uzazi
linahusisha jinsi zote mbili (ya kike na kiume) lakini kujifungua mtoto au
watoto ni jukumu la msingi la mama, ni haki ya msingi pia ya kila mwanamke
duniani.
Wanasema pamoja na
hilo siku hizi wengine huweza kutumia njia ya kupandikiza (IVF) kitaalamu na
kupata mtoto au watoto hasa wale wanaokabiliwa na matatizo ya uzazi, hayo ni
matokeo ya kukua kwa sayansi na teknolojia.
Lakini kiasili,
baada ya mbegu na yai kutunga mimba ndani ya mfuko wa uzazi wa mama, mimba hiyo
hukua na kuishi humo kwa muda wa miezi tisa.
Inapotimia miezi
hiyo tisa mama hujifungua na mtoto au watoto hao huanza rasmi ‘safari’ yao ya
maisha hapa duniani, ni tukio la kipekee.
Pamoja na hayo,
wanasisitiza afya ya mama na mtoto ni jambo la msingi kuzingatiwa kwani kadiri
mtoto anavyokuwa na afya njema ndivyo ambavyo naye atakuwa na uwezo mzuri wa
kuzaa (wa kike) au kuzalisha (wa kiume).
Zamani mabibi zetu
walilazimika kujifungua kwa msaada wa wakunga wa jadi ingawa hadi sasa bado
zipo jamii ambazo hujifungua kwa wakunga hao hata hivyo kutokana na maendeleo
ya sayansi na teknolojia wengi leo hii wanajifungua kwa msaada wa wakunga
wataalamu.
Pamoja na umuhimu
huo wa wakunga kwa miaka ya hivi karibuni baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi (wajawazito) na hata jamii kwa
ujumla kwamba wanatenda kazi bila kuzingatia misingi ya taaluma yao.
Wapo ambao
wanatuhumiwa kuwatolea lugha zisizofaa wajawazito wakati wanapokuwa
wakiwahudumia huko kliniki au katika vyumba vya kujifungua (labour).
Simulizi ya Frida
Frida Eliud Mkazi wa
Morogoro ni mama wa watoto wawili, anasema mtoto wake wa kwanza alijifungulia
katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mwaka 1998.
Anasema wakati wa
ujauzito wake huo wa kwanza alipatwa wasiwasi mwingi wa kuanza kuhudhuria
kliniki hasa alipokuwa akikumbuka simulizi alizosimuliwa na wanawake wenzake
kuhusu lugha zinazotolewa huko kliniki.
“Walikuwa wakinisimulia
jinsi walivyopokelewa katika hospitali walizokwenda kwamba baadhi ya wakunga na
wauguzi wanatoa lugha za kuudhi, lakini ilifika mahali nikasema wacha niende tu
kwa sababu sina jinsi na lazima nifuatilie maendeleo ya hali yangu na mtoto
wangu aliye tumboni.
“Nilianza kuhudhuria
kliniki, sitasahau siku ile ya kwanza, muuguzi aliyenipokea hakuwa na lugha
nzuri, hata siku nilipokwenda kujifungua mkunga aliyenisaidia naye hakuwa na
lugha nzuri, kusema ukweli wapo wanaofanya vema lakini kuna wengine
wanawaangusha kwa kufanya yasiyofaa,” anasema.
Anaongeza “Mkunga
yule kila nilipomuita aje anisaidie alikuwa akiniambia nisimsumbue, kwamba kuna
wengine pia waliokuwa wakihitaji kusaidiwa na yeye hakuwa na uwezo wa kujigawa
atusaidie wote.
“Nilipelekwa pale
hospitalini usiku sikujifungua hadi ikafika asubuhi, mume wangu alikuja
nikamsimulia kilichokuwa kikiendelea, alisikitika mno.
“Lakini hakuwa na
jinsi ilibidi wasubiri hadi nilipojifungua majira ya saa nne hivi, tukarudi
nyumbani, ujauzito wangu wa pili nilikwenda tena hospitali nyingine ya
serikali,” anasema.
Anaongeza
“Nilipokelewa na mkunga wa kiume, nilichelewa kujifungua lakini aliendelea
kunihudumia kwa upendo na kwa kunithamini mno.
“Alikuwa na lugha
nzuri, muda wote alikuwa akija kuniangalia na kunitia moyo kwamba nisiogope,
nitajifungua salama kwa kweli nilistaajabu, nikajifungua salama nikarudi
nyumbani kwangu na furaha,” anasema.
Anasema hivi sasa
ana ujauzito mwingine na kwamba anatamani kwenda kujifungua kwenye hospitali
hiyo na anatamani akifika huko apokewe na mkunga wa kiume na si wa kike.
Mama mwingine
Mariam James (50)
Mkazi wa Morogoro Mjini ni mama wa watoto watatu, anasema awali alikuwa akiishi
Jijini Dar es Salaam eneo la Sinza kwa Remmy.
Anasema alipojihisi kuwa
ni mjamzito mnamo mwaka 1990 aliamua
kufanya uchunguzi hospitali ipi itamfaa kwa huduma ya kliniki.
“Wanawake wenzangu
walishanisimulia changamoto walizokumbana nazo katika hospitali mbalimbali,
lakini nikasema kwa kuwa ninahisi ni mjamzito nifanye uchunguzi kwanza
hospitali ipi itanifaa nianze kliniki.
“Basi nilikwenda
kwanza Hospitali ya Tandale, nikakaa kwenye benchi nikaangalia namna ambavyo
wauguzi na wakunga walivyokuwa wakipokea wagonjwa na kuzungumza nao,” anasema.
Anasema
hakuridhishwa na watumishi wa hospitali hiyo, hivyo aliondoka tena hadi
Hospitali ya Mwananyamala akakaa kwenye
benchi na kufanya tena uchunguzi wake.
“Hapo napo
sikuridhika na huduma, nikaondoka hadi Hospitali ya Mnazi Mmoja nikafanya hivyo
hivyo, kidogo hapo niliridhishwa na huduma, kulikuwa na wauguzi na wakunga
wenye umri wa utu uzima tofauti na kule nilipokwenda awali, walikuwa wakipokea
watu kwa kauli nzuri mno.
“Lakini nikasema ngoja
niende na Hospitali ya Taifa Muhimbili nikaangalie huduma zilivyo, huko sikuridhishwa, nikaamua kurudi Mnazi
Mmoja wale watumishi wakaniambia muda ulikuwa umekwisha, ilikuwa siku ya ijumaa
basi wakanishauri niwahi mapema asubuhi nianze kliniki,” anasema.
Mariam anasema
aliondoka akiwa na furaha na kwamba aliwahi mapema jumatatu hospitalini hapo na
kuanza kliniki ya uzazi.
“Wale watumishi
walikuwa wakiongea nasi kwa lugha nzuri, walikuwa wanahudumia kwa upendo,
wanafariji na wanabembelea mtu unajisikia amani muda wote tofauti na wale
watumishi wa hospitali zingine ambazo nilikwenda walikuwa wakizungumza vibaya
na wagonjwa,” anasema.
Anaongeza
“Niliendelea kuhudhuria kliniki Mnazi Mmoja lakini nilipofikia kujifungua
walinishauri nitafute hospitali nyingine kwa sababu wakati ule pale walikuwa
hawana huduma ya kujifungua bali ya kliniki tu.
“Ingawa nilitamani
kujifungulia pale lakini sikuwa na jinsi ilibidi nirudi Mwananyamala
nikajifungulia hapo, kusema ukweli jinsi wauguzi na wakunga wenye umri wa utu
uzima walivyokuwa wanahudumia ilikuwa tofauti kabisa na wale wenye umri wa
ujana wakati huo,” anabainisha.
Anasema hadi sasa
anaona kuna utofauti mkubwa kati ya watumishi wenye umri mkubwa jinsi
wanavyohudumia wagonjwa na wale watumishi wenye umri mdogo.
“Wenye umri mkubwa
wana hudumia kwa upendo zaidi kuliko hawa wenye umri mdogo (wa ujana), kwa
msingi huo, ikiwa inawezekana basi naishauri serikali iangalie hii kazi ya
uuguzi na ukunga ifanywe na watu wenye umri wa utu uzima kuliko vijana,”
anashauri.
Ukweli wa mambo
Pamoja na umuhimu wa
kada hii katika sekta ya afya hata hivyo kwa muda mrefu sasa yamekuwako
malalamiko kutoka kwa jamii wakidai baadhi yao wamekuwa wakizungumza lugha
zisizofaa (za kejeli au matusi) kwa wajawazito hasa wanapokwenda kujifungua.
Itaendelea
Chapisha Maoni