NA VERONICA ROMWALD - DAR ES SALAAM
Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) inatarajia kuanza kutoa
huduma ya uchunguzi wa awali dhidi ya saratani ya utumbo ambayo kwa mujibu wa
takwimu inaonesha idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo imeongezeka.
Akizungumza na MATUKIO NA MAISHA hivi karibuni ofisini
kwake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa ORCI, Crispin Kahesa alisema
saratani hiyo imepanda kutoka nafasi ya 20 kati ya saratani zenye idadi kubwa
ya wagonjwa hadi kuwa miongoni mwa saratani 10.
“Tayari tumeagiza vifaa vya uchunguzi, kwa kutumia kifaa
hcho tunaweza kuona dalili za awali za saratani hii kwa kupima kinyesi cha mtu
husika na hivyo kuanza kumpa matibabu kwa wakati,” alisema.
Alisema miongoni mwa mambo yanayochangia mtu kupata saratani
hiyo ni unywaji wa pombe kupindukia hasa zile kali na ulaji wa nyama uliopita
kiasi.
“Kiujumla mfumo wa maisha unachangia kwa kiwango kikubwa mtu
kupata saratani hii na hatari zaidi ipo kwa kundi la wanaume kuliko wanaume,”
alisema.
Alisema vifaa hivyo vitakapowasili ORCI itatoa taarifa kwa
umma lini hasa itaanza uchunguzi huo wa awali na kwamba hivi sasa inaendelea
kutoa huduma mpya ya uchunguzi wa awali wa saratani ya ngozi kwa watu wenye
ualbino, saratani ya matiti na kizazi.
Chapisha Maoni