Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema –Aliyekuwa Uswizi

MAPEMA Januari, 2019 nilipokea mwaliko rasmi wa kuchaguliwa kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za masuala ya kisayansi hususan afya, mazingira na teknolojia (World Conference of Science Journalists – WCSJ).

Fursa hiyo tulipata waandishi wapatao 100 wa mataifa mbalimbali, wanaoandika masuala hayo, nilikuwa mshiriki pekee kutoka Tanzania, kwangu niliona ni fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka.

Mwaliko ule niliupokea kwa furaha kubwa kwani katika mkutano huo ambao ulifanyika Julai mosi hadi 4, huko Lausanne, Uswizi, yaliandaliwa mafunzo mbalimbali ambayo kimsingi yalilenga kutuimarisha kitaaluma.

Nimepata kusafiri mara kadhaa hasa nchi za Afrika Mashariki, awamu hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kwenda Barani Ulaya, nilijawa shauku kubwa kujifunza mengi, waswahili husema 'tembea uone'.

Kama vijana wengine wenye shauku ya kutembelea nchi mbalimbali hasa za Ulaya, hamu yangu ilikuwa kujionea namna wenzetu wanavyoyafanya mambo yao na kufanikiwa.

Huku nikiamini mafunzo yaliyoandaliwa yatakuwa ya manufaa kwangu, yatanisaidia kuimarika na kufanya ripoti bora zaidi za masuala hayo ya kisayansi kuliko hapo awali.

Katika muda niliokuwa najiandaa kwa safari nililazimika kuperuzi mitandaoni kupata uelewa juu ya kule ninapokwenda, hakika kila nilipoperuzi hamu ya kufika huko ilizidi kuongezeka.

Nilichagua kupita njia ya Istanbul ambako nilitakiwa kubadilisha ndege kwa ajili ya kuelekea Geneva na hapo nichukue usafiri wa treni kuelekea Lausanne.

Nikaperuzi kuangalia uwanja wa Istanbul ulivyo 'nilichoka', kwa jinsi ulivyokuwa unavutia huku ukitambuliwa kwamba ni miongoni mwa viwanja bora, vikubwa duniani.

Hapo taswira ya uwanja wetu wa terminal II ikanijia kichwani, nikahuzunika, lakini nilijipa moyo kwamba uwanja wetu wa terminal III upo mbioni kukamilika (ilikuwa kabla ya ufunguzi), nasi tutakuwa na uwanja mzuri japo bado haujafikia ukubwa ule wa Istanbul.

Waandaaji walinitumia pia ramani mbalimbali za Lausanne, nikalazimika kuperuzi kuhusu mji huo, kuanzia uwanja wa ndege Geneva mpaka Lausanne, kisha nikasubiri siku ya safari.

Hatimaye Juni 29, ikafika, saa tisa usiku nilianza safari yangu Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Juni 30, nikafika salama Geneva, ni safari ya wastani wa saa 12 angani.

Nilipokamilisha taratibu za ukaguzi wa vibali, nilielekea dawati la mapokezi ambalo WCSJ liliandaliwa pale uwanjani, nilipokewa na mwenyeji wetu alinielekeza mahala pa kwenda kupata usafiri wa treni.

Nilizidi kujionea mambo, japo hapa Tanzania tunao usafiri wa treni, kwangu ilikuwa mara yangu ya kwanza kutumia usafiri huo, pia ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusafiri kwa treni ya umeme.

Nikiwa ndani ya treni ile, kadiri  ilivyokwenda, fikra zangu nazo ‘zilinirudisha’ tena nyumbani Tanzania, ambako tunao usafiri wa treni nafahamu ile ya Deluxe hadi ile ya Mwakyembe, imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Nikajikuta namkumbuka rafiki yangu, James Kandoya, mwandishi wa masuala ya afya, Gazeti la The Guardian, hunisimulia jinsi treni hiyo ya Mwakyembe inavyowasaidia kukabiliana na changamoto ya usafiri.

Fikra zangu zilinisafirisha hadi kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (Standard Gauge), unaoendelea, chini ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Reli hiyo itakapokamilika itakuwa ikitumiwa na treni za umeme, yaani kama ile niliyopanda Uswizi, ndoto inakwenda kuwa halisi.

Nikakumbuka, ujenzi utakapokamilika Tanzania itakuwa  miongoni mwa nchi zenye huduma ya usafiri wa haraka zaidi duniani.

Reli hiyo ambayo awamu yake ya kwanza itakuwa na urefu wa kilometa 300, itaiwezesha Tanzania kutumia treni ya umeme yenye kusafiri kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa.

Kukamilika kwake kutaifanya nchi yetu kwenda sanjari na India ambayo nayo tayari ina treni yenye kusafiri kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa kutoka New Delhi hadi Agra.

Kwa bara la Afrika, Morocco tayari ina kilometa 1,300 zilizounganishwa kwa reli ya aina hiyo yenye uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 200 kwa saa.

Mazingira hayo yameifanya nchi hiyo kumiliki treni ya umeme yenye kasi zaidi barani Afrika ambayo kiwango chake cha juu cha mwendokasi ni kilometa 320 kwa saa.

Pia nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Ethiopia nazo zina reli ya kiwango cha Standard Gauge yenye uwezo wa mwendokasi wa kilometa 120 kwa saa, wao wameweza sisi tushindwe kwanini?.

Nikamkumbuka Rais Magufuli, ambaye mara kwa mara husema wenzetu wapo mbali mno, sisi tumechelewa mno, lazima tufanye kazi, nchi yetu ni tajiri, tuijenge nchi yetu, inawezekana.

Wakati nikiendelea kufikiri nikajiona kama vile tayari nimo ndani ya treni yetu, eti, naelekea Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, ghafla nikashtuka kutoka kwenye fikra hizo, kumbe nipo Ulaya.

Nikashusha pumzi ndefu, nikajisemea kimoyo-moyo ‘kweli tumechelewa siku moja na sisi tutafika’, nikatabasamu.

Nikafika mwisho wa kituo cha kwanza, ambako nilitakiwa kupanda treni nyingine ya umeme ‘Metro’ kuelekea hoteli ya Aquatis ambako tuliandaliwa mahala pa kukaa.

Nikiwa chumbani kwangu niliendelea kutafakari namna mji ule ulivyojengwa kwa ustadi mkubwa, si tu usafiri wa reli bali hata barabara.

Wana fly-over telee… nikakumbuka namna nchi yetu inavyopambana kuimarisha miundombinu, nikajisemea tena, tutafika.

Nililala nikitamani pakuche, ili tuanze rasmi mkutano, hatimaye palikucha, Julai mosi, baada ya salamu na kujenga mahusiano ya kitaaluma na washiriki wenzangu, jioni siku hiyo ulifanyika uzinduzi rasmi.

Rais wa Shirikisho la Waandishi wa Habari za Kisayansi Duniani (WFSJ), Mohammed Yahia alisema kutokana na umuhimu mkubwa uliopo sasa wa habari za kisayansi, waliona vema kuwaita pamoja waandishi wa habari za kisayansi wa mataifa mbalimbali duniani, kujifunza na kujadiliana.

“Karne ya sasa ni ya ulimwengu wa sayansi na teknolojia, kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo ambavyo uhitaji wa taarifa (habari) za kisayansi unavyozidi kuongezeka duniani."

Unaweza kusema sayansi ni maisha kwani husaidia kumpa mbinu mbalimbali binadamu zinazoweza kumsaidia kutatua changamoto zinazozomzunguka,” alisema.

Aliongeza “Tafiti za kisayansi humuwezesha kupata majibu kwa maswali ambayo hujiuliza ambazo humuwezesha kutatua changamoto zinazomkabili kwa wakati huo.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kufikisha ujumbe kwa jamii kwa kuangazia matokeo mbalimbali ya tafiti zilizofanywa na wataalamu katika lugha rahisi inayoeleweka kwa wengi.

Kamishna na Umoja wa Ulaya (EU), anayeshughulikia masuala ya tafiti, Carlos Moedas, alisema “Ujumbe wangu kwenu (waandishi wa habari za kisayansi), mnao uwezo mkubwa hasa katika kusimulia hadithi zinazohusu masuala ya kisayansi.

“Kimsingi, dunia inahitaji taarifa zilizo sahihi za kisayansi mno katika kipindi hiki pengine kuliko wakati wowote ule hapo kabla.

“Shahidi (tafiti) za kisayansi zina umuhimu mkubwa kwa jamii zetu, hivyo mnawajibu wa kuhakikisha mnawaeleza watu katika usahihi unaotakiwa na katika namna iliyo bora zaidi, mkihusisha moja kwa moja na maisha yao halisi,” alitoa rai.

Alisema ni muhimu kuchambua tafiti za kisayansi kwa namna ambayo itaisaidia jamii kwani zinazo nafasi ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinakuwa zinawakabili.

Thierry Zomahoun alisema pamoja na changamoto zote zilizopo, ni muhimu sana kubobea katika masuala ya tafiti na uandishi wa habari za kisayansi.

“Kwa mfano Afrika ni bara lililosheheni watafiti mbalimbali wenye uwezo wa juu mno lakini ukweli ni kwamba tafiti nyingi zimekuwa zikibakia kwenye makaratasi, hazifanyiwi kazi.

“Ni wakati mwafaka wa kuzifanyia kazi, waandishi kuziandika tafiti hizo kwa lugha ambayo jamii na watunga sera wataielewa, ili basi ziweze kusaidia hata matatizo mbalimbali ambayo yanazikabili jamii zetu duniani,” alitoa rai.

Msisitizo hapa ulikuwa watafiti kushirikiana bega kwa bega na waandishi wa habari katika kufikisha ujumbe sahihi kuhusu matokeo ya tafiti walizofanya, kwa jamii.

Julai 2, mafunzo yalianza rasmi, tuligawiwa majarida mbalimbali, nilivutiwa zaidi na jarida lilioandaliwa na Lausanne Univeristy Hospital kupitia Facult of Biology and Medicine.

Ndani ya jarida hilo ambalo lilibebwa na agenda kuu ‘The Future of Medicine’, kumeelezwa huduma za kibingwa zinatolewa ndani ya nchi hiyo.

Wamewekeza ipasavyo kuanzia majengo, wataalamu, vifaa tiba, hata masuala ya tafiti na matibabu dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani, moyo, mifupa na mengineyo.

Simulizi ya Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo Rene Pretre, ilinivutia zaidi kuisoma ndani ya jarida hilo, anaeleza kwa mara ya kwanza ilikuwaje pindi alipohitajika kufanya upandikizaji moyo kwa mgonjwa.

“Ilikuwa 2004, msichana mdogo ambaye alihitaji kupandikizwa moyo ili aweze kuendelea kuishi, nilimfuata haraka ‘director’ wangu, ili tujadili naye, tulipata ‘artificial heart’ tulimpandikiza, akaishi,” anasimulia.

Simulizi hii ilinirudisha nyumbani Tanzania, nikakumbuka jinsi mabingwa wetu pale Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi.

Nikaikumbuka pia Hospitali ya Benjamin Mkapa, wanavyopambana kusaidia kuhudumia wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo hayo.

Wenzetu wamefanikiwa hadi kupandikiza moyo, nikajisemea hii ndiyo hatua pekee ambayo Tanzania tunaitarajia.

JKCI ni taasisi ya umma ambayo sasa inang’ara ndani na nje ya mipaka ya bara la Afrika, mpaka Ulaya kwenyewe, kwa matibabu ya kibingwa dhidi ya magonjwa ya moyo, nikajisemea tena ipo siku tutafika.

Nikafikiri pia namna huduma mbalimbali za kibingwa zinavyoendelea kuwekezwa hapa nchini kuanzia matibabu ya saratani pale Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), imewekezwa mashine ya kisasa ya uchunguzi na matibabu dhidi ya saratani.

Matibabu ya upandikizaji figo, vifaa vya usikivu (cochlea implant), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo sasa inatarajia kufanya upasuaji wa kupandikiza ini na uloto kwa wagonjwa wa siko seli.

Pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambayo nayo sasa inajipanga kuanza rasmi upasuaji kutibu matatizo ya ubongo bila kufungua fuvu la kichwa.

Hakika tutafika, ipo siku Tanzania itakuwa kama Uswizi.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement