*Mwaka huu kufanya tena kampeni Kitaifa *Lengo kuwafikia watoto milioni nne
Na Veronica Mrema - Dar es Salaam
HUENDA miongoni mwetu wapo watu ambao ukiwauliza leo hii
polio ni ugonjwa gani?, wasiweze kukupatia majibu hasa wale waliozaliwa kuanzia
miaka ya 1990 hadi sasa.
Inawezekana pia wakawepo baadhi ambao wataweza kukupa
majibu polio ni ugonjwa gani, dalili zake ni zipi? kwa ufahamu walionao baada
ya kuusoma kwenye vitabu na majarida mbalimbali lakini si kwa kuufahamu kiuhalisia.
Hili lipo wazi kwani kwa miaka ipatayo 23 sasa nchini mwetu
hakuna mtu yeyote aliyebainika kuathiriwa na ugonjwa huo.
Mafanikio hayo ni kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya chanjo kwa
kuhakikisha inaimarisha huduma za upatikanaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo na
mengineyo.
POLIO
NI NINI?
Ni muhimu kufahamu hili, kwa mujibu wa wataalamu wa afya
wanaeleza ni ugonjwa wa kuambukiza ambao husababishwa na virusi ambavyo hushambulia,
huathiri mishipa ya fahamu (neva) na kusababisha ulemavu wa kudumu (mwili
kupooza) au kifo.
Virusi hivyo hupatikana kwenye kinyesi cha binadamu,
huingia mwilini mwake kupitia kinywani kwa njia ya kula chakula au kunywa
kinywajikilichoathiriwa na virusi hivyo.
Wataalamu wa afya wanaeleza takriban asilimia 90 hadi 95 ya
watu wanaopata maambukizi ya ugonjwa huo huwa hawaoneshi dalili zozote.
Ni asilimia tano hadi 10 ya watu ndiyo ambao huonesha
dalili za homa, maumivu ya kichwa, kutapika, kuharisha, mishipa ya shingo
kukaza na maumivu katika miguu na mikono.
Hali hiyo hutokana na virusi hivyo vinapofika kwenye tumbo
huweza kusafiri hadi kwenye ubongo na uti wa mgongo ambapo mgonjwa huweza
kuhisi maumivu ya kichwa, kukakamaa kwa shingo pamoja na maumivu ya miguu na
mikono.
Kwa kawaida watu hawa hurejea katika hali ya kawaida baada
ya wiki moja au mbili, asilimia 0.5 ya waathrika huweza kupata udhaifu wa
misuli suala linalosababisha kushindwa kutembea.
Hali hiyo huweza kutokea katika masaa kadhaa baada ya
maambukizo.
Virusi vya polio vinapofika tumboni huweza kuzaliana na kuongezeka, hivyo kuanza kushambulia neva na kusababisha mgonjwa kupooza baadhi ya viungo.
HUATHIRI
WATOTO
Ugonjwa huu, huwapata zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka
miwili kuliko wale ambao wameshavuka umri huo.
Ingawa ni asilimia ndogo sana ya wanaopatwa na polio huweza
kupata ulemavu wa mwili wa kudumu, lakini hatari hiyo inalazimu ugonjwa huo
kupewa umuhimu mkubwa na kuzuiwa kupitia chanjo.
HALI
ILIVYO NCHINI
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Dafrosa Liymo
anasema hapa nchini tangu mwaka 1975 Serikali ilianza kutoa aina tatu za chanjo
hadi kufikia 2018 ziliongezeka kufikia tisa.
Anasema chanjo hizo tisa zinazotolewa zinawakinga watoto
dhidi ya magonjwa 13 ikiwamo, surua-rubella, saratani ya mlango wa kizazi, kifua kikuu, kifadulo, pepo punda na homa ya
ini na mengine.
“Ni jukumu la Serikali kuhakikisha chanjo zipo na
zinapatikana kwa wakati, hadi sasa hatuna upungufu wa chanjo nchini,”
anasema Dk. Dafrosa.
Anasema tangu mwaka 1996 Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazotambulika duniani na WHO kwamba haina mgonjwa mwenye polio.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu anasema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na matumizi
ya chanjo.
Anabainisha kila mwaka Serikali huipatia wizara hiyo kiasi
cha Sh bilioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo mbalimbali,” anasema.
Waziri Ummy anasema kwa kuwapa watoto chanjo idadi ya vifo
vya watoto chini ya miaka mitano imepungua kutoka vifo 112 katika kila vizazi
hai 1000 hadi kufikia vifo 67 kwa kila vizazi hai 1000 hivi sasa.
“Kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuwekeza katika masuala ya chanjo kwani tafiti zinaeleza
katika kila dola moja ambazo Serikali huwekezwa kwenye chanjo ili kukinga watu
wake dhidi ya magonjwa huokoa dola 16 ambazo hutumika kutibu magojwa,” anasema.
Anaongeza “Serikali itaendelea
kuchukua hatua zote kuhakikisha tunawakinga wananchi dhidi ya magonjwa,
tutaendelea kufanya usafi wa mazingira vile vile tutaendelea kutoa chanjo.
“Hivyo, kadri maendeleo ya
kisayansi na kiteknolojia yanavyopatikana ndivyo na sisi tutakavyojiridhisha na
kuhakikisha tunapata chanjo ili kukinga wananchi wetu,” anasema.
Anaongeza “Mwaka 2020 tunatarajia kufanya utafiti wa
Kitaifa kuhusu hali ya afya tunaamini kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika idadi ya
vifo itakuwa imepungua zaidi.
“Mafanikio yanaonekana wazi, kwa mliokuwa miaka ya nyuma
mtakumbuka zilianzishwa kambi maalum kwa ajili ya kuhudumia watoto wenye tatizo
la kuhara, kwa kuwekeza kwenye chanjo leo hii magonjwa ya kuhara, kifaduro na
mengine tumeweza kuyadhibiti,” anasema.
HALI
ILIVYO DUNIANI
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza hadi sasa bado
hakuna dawa inayoweza kutibu ugonjwa wa polio, ila unazuilika kwa kuhakikisha
watu wanapatiwa chanjo.
WHO linaeleza katika miaka ya 1980 ugonjwa huo ulikuwa
ukiathiri takribani watu 350,000 katika nchi 125 kila mwaka.
Kutokana na hali hiyo, mwaka 1988 juhudi za kuangamiza
ugonjwa huo zilianza tangu hapo idadi ya maambukizi imepungua kwa asilimia 99.
Takwimu zinaeleza hadi kufikia 2013 watu 416 duniani ndilo
walibainika kuathiriwa na ugonjwa huo ikilinganishwa na 1980.
Mafanikio hayo yametokana na kupewa umuhimu chanjo kwa
watoto takribani katika maeneo yote duniani suala lililoleta matumaini ya
kutokomezwa ugonjwa huo.
Lakini tangu mwaka 2014 ugonjwa wa polio bado umebaki kuwa tatizo katika nchi za Afghanistan, Nigeria na Pakistan.
KAMPENI TANZANIA
Dk. Dafrosa anasema chanjo dhidi
ya polio imeendelea kutolewa nchini japo hakuna mgonjwa ili kuendelea kuwakinga
watoto.
“Kila mwaka huwa kuna wiki ya
chanjo, kule katika Halmashauri huwa tunatoa chanjo hii ambayo ipo katika mfumo
wa matone, aidha, mwaka 2010/11 tulifanya kampeni ya kutoa chanjo hii katika
mikoa ambayo ilikuwa na kiwango kidogo cha utoaji chanjo,” anasema.
Anaongeza “Mafanikio ya
kuudhibiti ugonjwa wa polio ni kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi ambao
walijitokeza na kuleta watoto wao tukawapatia chanjo.
“Hivyo, tunaendelea kuhamasisha
wananchi kuendelea kuleta watoto ili wapatiwe chanjo, maana bado kuna nchi
ambazo zina mzunguko wa kirusi pori cha polio, ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo, Afghanistan, Pakistani na Nigeria.
“Kwa kuwa nchi yetu ina urafiki
na tunapokea wageni wengi, ndiyo maana tunazidi kujikita kuhakikisha watoto
wanapatiwa chanjo ili kuimarisha kinga,” anasema Dk. Dafrosa.
Anasema Tanzania bado inaendelea
kufanya uchunguzi kila mara inapobainika yupo mtu ambaye amepata ulemavu wa ghafla.
“Yale mafriji yaliyopo hapa ofisi
za mpango wa Taifa wa Chanjo, ni maalum kwa ajili ya kutunza sampuli za wale
ambao wanaripotiwa kupata ulemavu wa ghafla.
“Tunatoa rai pale wananchi wanapoona
mtu amepata ulemavu wa ghafla wampeleke hospitalini na sampuli yake iletwe ili
tuichunguze, kwa sababu kirusi kinabebwa na kinyesi, kinaweza kuenezwa hata na
wageni,” anasema.
Waziri Ummy anasema Septemba 26
hadi 30, mwaka huu Serikali kupitia Wizara hiyo itafanya kampeni ya Kitaifa
nchi nzima abapo itatoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Surua-Rubella na polio.
“Kampeni itafanyika nchi nzima,
kitaifa itazinduliwa Mkoani Morogoro katika Viwanja vya Jamhuri,” anabainisha.
Anaongeza “Japo kila siku chanjo
hizi zinatolewa katika vituo vya afya, takwimu zinaeleza tumeweza kufikia
watoto kwa kiwango cha asilimia 98 pekee.
“Hii inamaanisha katika kila
watoto 100 tumewafikia 98, watoto wawili bado hatujawafikia, changamoto ipo
zaidi maeneo ya mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi,” anasema Waziri Ummy.
Anaongeza “Hivyo, kampeni kubwa
ya kitaifa namna hii inakuwa ni sehemu ya kuongeza nguvu kuhakikisha tunamfikia
kila mtoto anayestahili kupatiwa chanjo.
Anasema katika kampeni hiyo wanakusudia kuwafikia watoto milioni nane wenye umri miezi tisa hadi 59 ambao watapatiwa chanjo ya surua-rubella na watoto milioni nne wenye umri wa miezi 18 hadi 42 watapatiwa chanjo ya polio.
Chapisha Maoni