Na Veronica Mrema - Dar es Salaam
KWA asilimia 99 saratani ya
matiti huathiri kundi la wanawake duniani, wanaume ikiwa ni asilimia moja
pekee, kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO).
Lakini pamoja na ukweli huo,
kundi la wanaume linashauriwa kwamba halipaswi kubaki nyuma katika suala zima
la uchunguzi wa afya ya matiti yao.
Hii ni kwa sababu ikiwa
mwanaume anakabiliwa na saratani hii na hatagundulika mapema huwa kwenye hatari
zaidi kuathiriwa mapafu yake kuliko ilivyo kwa kundi la wanawake.
“Kwa wastani hapa hospitalini
kwa mwaka, huwa tunaona wanaume wapatao 18 wanaokabiliwa na saratani hii,”.
Anasema Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Crispin
Kahesa.
Anaongeza “Ingawa huathiri
asilimia moja ya wanaume hata hivyo kwa upande wao ni hatari zaidi
isipogundulika mapema kwani huweza kuathiri mapafu yao kwa haraka.
“Changamoto kubwa tunayoiona
ni kwamba katika hao tunaowagundua wengi hufika hospitalini hapa wakiwa
wamechelewa na ugonjwa ukiwa katika hatua ya juu,” anasema.
Dk. Kahesa ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani katika taasisi hiyo anasema hali hiyo
hutokea kwa sababu wanaume wengi bado hawalipi kipaumbele titi kama ilivyo kwa
wanawake.
“Kwa mfano, wanaume wengi
hata wanapohisi kuna uvimbe hudhani ni hali ya kawaida tena hasa ikiwa uvimbe
huo hauwasababishii maumivu yoyote,” anasema.
Anaongeza “Hudhani ni hali
ya kawaida lakini la hasha! Jambo la msingi wanalopaswa kufanya ni kuwahi
hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
“Ili kama uvimbe ule ni saratani wapate matibabu mapema,” anasisitiza.
ISMAIL AFUNGUKA
Hivi karibuni katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Juma Ismail (50), Mkazi wa Gongo la Mboto, alikuwa miongoni mwa waliopanga foleni kwenda chumba cha daktari, kuchunguzwa saratani ya matiti.
“Mke wangu ndiye aliyekuja kunieleza kwamba kuna uchunguzi unafanyika hapa Mloganzila, alinieleza madaktari wanasema wanaume pia tunaweza kuathiriwa na saratani hii.
“Sikuwa najua kabla kwamba hili linawezekana, nikaona vema nije nichunguzwe maana wanasema ikigundulika mapema ni rahisi kutibika na kupona,” anasema.
Anasema elimu aliyopatiwa imemfungua mengi kuhusu saratani hiyo na kwamba atakwenda kuelimisha vijana wake nyumbani.
“Nimejaliwa
kupata watoto wa kiume watatu, nitakwenda kuwaelimisha na ikiwezekana nao waje
wachunguzwe, ni muhimu kufanya uchunguzi kuliko kusubiri mpaka athari zake
zijitokeze,” anasema Ismail.
Dk. Kahesa anafafanua “Ni
rahisi kugundua saratani ya matiti kwa wanaume kuliko kwa wanawake na kwamba dalili
za saratani ya matiti kwa wanaume ni tofauti kidogo na wanawake.
“Jinsi mwanamke alivyoumbwa,
kifua chake mafuta mengi kuliko cha mwanaume ndiyo maana huwa si rahisi
kugundua.
"Lakini kwa sababu
mwanaume ana mafuta kiasi kifuani, ni rahisi hata uvimbe unapotokea anaweza
kuwahi kugundua kwa sababu huwa unaonekana haraka sana.
“Lakini, nimeeleza awali
kwamba changamoto iliyopo, wengi wanapohisi uvimbe hudhani ni hali ya kawaida
kwa sababu mara nyingi katika hatua za awali huwa hauna maumivu.
"Ni kwa sababu hiyo wengi
huchelewa kuja hospitalini kwani huwa wanachelewa pia kufikia ile hali ya
chuchu kuanza kutoa majimaji au damu,” anasema.
Dk. Kahesa anaongeza "Saratani
ya matiti ni hatari kwa kina baba kifua chao hakina nyama nyingi ni rahisi
kuhamia kwenye mapafu na kuyaathiri, tatizo ni kwamba wengi huwa wanaona aibu
kuonesha titi kufanyiwa uchunguzi.
WALIO HATARINI
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Sikudhani Muya anasema kwenye taasisi hiyo, Saratani ya matiti inashika namba mbili kwa idadi ya wagonjwa wanaowaona kliniki.
“Kundi la wanaume walio hatarini zaidi kupata saratani hii ni wale ambao kwenye familia zao kuna historia kwamba wamewahi kupata mgonjwa wa saratani hasa hii ya matiti,” anabainisha.
Dk. Muya anaongeza “Saratani hiyo huwakumba zaidi wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea, hivi sasa tunaona wagonjwa hadi wale wenye umri wa kuanzia miaka 20 na kuendelea.
UCHUNGUZI UNAVYOFANYIKA
“Huwa tunafanya kwanza uchunguzi wa awali kwa kulikagua titi, tunapobaini wenye viashiria vya awali huwa tunawaweka kwenye hatua inayofuata ya uchunguzi.
“Tunafanya tena uchunguzi wa kina kwa kutumia mashine ya X- ray au ultra sound ya matiti kulingana na umri wa muhusika na vipimo.
"Hivyo hutuwezesha kujua iwapo viashiria hivyo ni ugonjwa au la! Maana si kila vivimbe ni saratani," anabainisha Dk. Muya.
KWA WANAWAKE
“Wanawake ndiyo wanaathirika zaidi kwa sababu ya maumbile wana chembechembe zaidi za matiti na wana vile vimeng'enyo ambavyo vinaweza kusababisha zaidi wapate saratani ya matiti kuliko wanaume,”.
Anasema Daktari Bingwa wa Radiolojia MNH- Mloganzila, Lulu Sakafu.
Anaongeza “Kwa mfano, uchunguzi tuliofanya hapa Mloganzila, Oktoba 26 na 27, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kaudhimisha mwezi wa uhamasishaji.
"Uelimishaji na uchunguzi wa saratani ya matiti, walifika wanawake zaidi ya 160, kati ya hao zaidi ya 40 tuliwakuta na viashiria vya awali saratani hii.
“Hatukupata mwanaume hata mmoja aliyejitokeza kuja kufanyiwa uchunguzi, wanawake tuliowabaini tumewaingiza katika mfumo wa matibabu.
"Tutaendelea kuwafanyia vipimo zaidi ili tuweze kujua iwapo vile viashiria tulivyowakuta navyo ni saratani ya matiti au la,” anabainisha.
Anasema
sambamba na uchunguzi huo, waliwapa elimu jinsi kuhusu saratani hiyo, dalili
zake na jinsi ya kujichunguza binafsi nyumbani maana wengi bado hawajui.
Dk. Kahesa anabainisha kwamba ORCI kwa mwaka huu pekee wameweza kuona wanawake 1443 ambapo kati yao 342 wamekutwa na uvimbe 170 walikuwa na dalili za awali za saratani hiyo.
“Katika hawa 170 tulipowafanyia
vipimo zaidi 68 tuliwagundua vivimbe vile
walivyokuwa navyo tayari vilikuwa ni ugonjwa wa saratani,” anasema.
Anasema miongoni mwa wanawake
hao wapo ambao tayari wamepatiwa matibabu ikiwamo za upasuaji na wengine za
mionzi, wapo waliomaliza na wengine wanaendelea kuhudhuria kliniki.
WENGI NI WA-MIJINI
Dk. Kahesa anasema idadi
kubwa ya wagonjwa ambao huwapokea ORCI huwa wanatoka katika maeneo ya mijini
hasa katika majiji makubwa.
“Tunaona wengi wanatokea
hapa Dar es Salaam, ukifuatiwa na mikoa ya kanda ya mashariki, nyanda za juu
kusini (Mbeya) na Mwanza,” anabainisha.
VISABABISHI
Dk. Kahesa anasema kiujumla
tafiti zinaonesha kasi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo hayo ya
saratani inazidi kuongezeka duniani.
“Kuna ongezeko kubwa la
unene uliokithiri, uzito mkubwa, matumizi ya poimbe, uvutaji wa sigara, na
ulaji usiofaa hasa vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi na vile vya
viwandani,” anabainisha.
“Ni muhimu sasa jamii yetu
kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia ulaji unaofaa, kuepuka unywaji wa
pombe, uvutaji sigara, kuzingatia kufanya mazoezi na kuchunguza afya mara kwa
mara,” anashauri.
Mwakilishi wa Chama cha Madaktari Wanawake (MEWATA), Mkoa wa Pwani, Dk. Deograsia Mkapa anasema.
uelewa wa jamii kuhusu saratani ya matiti na nyinginezo umeongezeka hivi sasa tofauti na miaka ya nyuma.
"Tunazunguka maeneo mbalimbali nchini tumeshuhudia, mwamko ni mkubwa watu kujitokeza kuchunguzwa, tunaona fahari maana ndicho hasa MEWATA tumekuwa tunatamani kukiona.
“Serikali imejitahidi mno kusogeza karibu zaidi na jamii huduma za uchunguzi wa magonjwa ya saratani hasa hii ya matiti na ile ya kizazi,” anasema.
Dk. Mkapa anaongeza “Miaka ya nyuma ilikuwa lazima watu waende Ocean Road lakini sasa hivi zinatolewa mpaka kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa, Wilaya na vituo vya afya maeneo mbalimbali nchini.
“Hivyo, tunaisisitiza jamii kwenda kufanyiwa uchunguzi kwa sababu ikigundulika mapema, hutibika na kupona,” anatoa rai.
Chapisha Maoni