NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KITAALUMA si daktari, ni
mhudumu wa Mochwari, hiki ni chumba maalum kinachotumika kuhifadhia miili ya
marehemu ikisubiri uchunguzi na maandalizi (kusafishwa) kwa ajili ya maziko.
Ingawa ni chumba muhimu mno lakini
kwenye jamii yetu wapo baadhi ya watu ambao hukiogopa na hata kuwashangaa wale
wanaoamua kufanya kazi ndani ya chumba hicho.
Hata hivyo, wakati wengine
wakiogopa kufanya kazi hiyo wapo wanaifanya na ndiyo inayowasaidia kuendesha
maisha yao ya kila siku hapa duniani.
Miongoni mwao ni Seleman
Mbiza (57), Mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam ambaye JAMVI LA HABARI limefanikiwa kufanya naye mahojiano haya.
Mbiza anasema tangu 1984
amekuwa akifanya kazi hiyo baada ya kushawishiwa na ndugu yake ambaye wakati
huo alikuwa mhudumu wa mochwari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
“Sikuwahi kufikiri wala
kutarajia kwamba ipo siku nitakuwa muhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti
(mochwari), awali nilikuwa mfanyabiashara, nikiuza kahawa kule maeneo ya uwanja
wa ndege (kipawa).
“Nilianza rasmi kazi hii
(mochwari) 1984 baada ya kushawishiwa na huyo ndugu yangu (si wa
kuzaliwa tumbo moja, tulisoma wote Shule ya Msingi), alikuwa anafanya kazi hii
hapa Muhimbili,” anasimulia
Anasema kabla ya kuanza
kufanya kazi hiyo naye pia alikuwa anawashangaa wale waliokuwa wakiifanya
na alikuwa akiogopa kuingia ndani ya
chumba hicho.
“Ndugu yangu huyo alikuwa
kila akija kunitembelea ananisimulia na kunisisitiza kwamba si kazi ngumu na
naweza hata mimi kuifanya,” anasimulia.
Mbiza anasema kuna wakati alikuwa
anakwenda Muhimbili kumtembelea ndugu yake huyo na ndipo alipata nafasi
kushuhudia jinsi ambavyo mwili wa marehemu huhifadhiwa.
“Taratibu nikajikuta naanza kupenda kazi aliyokuwa akiifanya, nikawa natafuta nafasi zaidi na kwenda kuangalia namna anavyofanya.
"Woga ukanitoka kabisa, nikaona ni jambo la kawaida na
nikajikuta na mimi natamani kuifanya,” anasema.
Anaongeza “Nilikuwa nakuja
na kuangalia anavyofanya kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja, nikachukua hatua,
nikaamua kuandika barua ya kuomba kazi kwa uongozi wa hospitali, ikapokelewa.
NDANI YA CHUMBA
Anasema aliitwa kazini mara
moja na kuanza kipindi cha majaribio ambacho kilikuwa miezi sita kumpima uwezo
wake wa utendaji kabla hajapewa mkataba.
“Sikuwa na hofu, wasiwasi wala woga kwa sababu tayari mazingira yale nilikuwa nimeshayazoea ingawa katika siku za mwanzo niliona ilikuwa ngumu kidogo,
".., yule ndugu yangu alinitia moyo
kwamba ipo siku nitazoea kabisa,” anasimulia.
Anasema alikuwa akifanya
kazi hiyo kwa kusimamiwa na madaktari waliobobea akiwamo Profesa Kitinye, Dk.
Mushi na Profesa Kahaya.
“Kumbuka hadi nilipoomba hii
kazi mimi sikuwa nimesomea, sijawahi kwenda darasani kusomea jinsi ya kuhudumia
maiti wala chumba cha kuhifadhia maiti.
“Hivyo hao wataalamu watatu
ndiyo walikuwa walimu wangu, walinifundisha pia miiko ya kazi hii kwamba
natakiwa kuzingatia usafi na kuwa na lugha nzuri kwa wafiwa.
“Walinifundisha jinsi ya kubeba mwili, jinsi ya kuuosha, kuuweka dawa, kuhifadhi mochwari na yale yanayopaswa kufanyika wakati wa uchunguzi.
"Nilikuwa najifunza pia mambo mengi
kupitia kwa yule ndugu yangu,” anasimulia.
Anaongeza “ Baada ya miezi sita ya majaribio kupita nilionekana kuwa ninaweza kufanya kazi hiyo, nikapewa mkataba.
NYAKATI NGUMU
Mbiza anasimulia wakati
mgumu kwake katika kazi hiyo ni kipindi mwili wa marehemu unapokuwa ukifanyiwa
uchunguzi kubaini kifo hasa ikiwa kinaonekana ni cha utata.
“Kwa hakika, kipindi cha
‘postmortem’ ndicho ambacho naona huwa
ni kigumu, tena afadhali hivi sasa nina ule uzoefu awali ilikuwa changamoto
kubwa mno kwangu.
“Maana daktari ataeleza
wanahitaji kufanya uchunguzi, hivyo wanataka baadhi ya viungo vya marehemu kwa
mfano moyo, figo, ini, matumbo ili wayachunguze, inabidi achanwe ili kupata
viungo hivyo.
“Wanakueleza pa kuchana na
kuvitoa lakini kabla ya kuchana lazima uvae mavazi maalum ya kujikinga kwa
sababu kuna magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.
“Kwa mfano, ikiwa marehemu
inasadikika amekufa kutokana na ugonjwa wa tauni, baada ya kumaliza kazi hiyo
lazima muhudumu amuone daktari kuna dawa maalum atampatia za kutumia ili
kujikinga.
“Lakini wakati mwingine
inaweza kutokea bahati mbaya muhudumu amemchana marehemu, kisu kikapitiliza na
kumkata yeye pia, wanasema baada ya hapo lazima akachome sindano maalum,”
anasimuliza.
Anaongeza “Ndiyo maana
nasema kipindi cha uchunguzi huwa ni kigumu kwa sababu inabidi muhudumu uwe
makini mno kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa namna moja au nyingine.
‘MIKWARUZANO NA WAFIWA’
“Mabosi wangu wana imani
kubwa na mimi na siku zote nahakikisha nafanya kazi kwa weledi na kwa
kuzingatia maadili na miiko, lakini wakati mwingine hutokea mikwaruzano ya hapa
na pale na wafiwa.
“Naelewa sipaswi kukwaruzana nao lakini wakati mwingine huwa inatokea tu najikuta tumekwaruzana, basi kuna ambao nawaomba radhi wanaridhia.
"Lakini wengine huenda ofisi za utawala
kulalamika, nimewajibu vibaya, naomba radhi, kwa sababu na mimi ni binadamu
kuna wakati nakosea,” anasema.
Anaongeza “Kimsingi
anayefanya kazi hii hapaswi kuwa mwenye ghadhabu ingawa wakati mwingine wafiwa
wanaweza kumsababisha kughadhibika lazima ajifunze kuwa mtulivu na mvumilivu.
“Ukiwa mwenye ghadhabu ikatokea kwa mfano umempiga kofi mfiwa kumbe ni mgonjwa anaishia kudondoka na kufa unajikuta umepata kesi bila kutegemea, uvumilivu ni jambo la msingi,” anasema.
SHUGHULI ‘PEVU’ KUPATA MKE
Mbiza anasimulia kwamba
haikuwa kazi rahisi kwake kupata mke wa kuoa na kwamba ilimlazimu kutumia mbinu
mbadala kufanikisha nia yake hiyo.
“Kutokana na mtizamo uliopo kwenye jamii, muhudumu wa mochwari anaogopwa na kuonwa mtu asiye wa kawaida kumbe la!, kwa msingi huo niliona wazi nikipata msichana na kumueleza ninafanya kazi hiyo ni wazi atanikimbia.
“Hivyo niliamua kujiita
daktari na kweli nilifanikiwa, nilipata mke ambaye nimebahatika kuzaa naye
watoto wanane, awali hakubaini kabisa kwamba ninafanya kazi mochwari hadi siku
nilipoamua kumueleza.
“Sasa anajua lakini hawezi
kunikimbia kwa sababu kama ni maji tayari yameshamwagika,” anasema Mbiza na
wote tunajikuta tukiangua kicheko.
MUDA WA MAITI MOCHWARI
Anasema kulingana na
utaratibu uliowekwa hospitalini hapo, maiti inapaswa kukaa mochwari kwa muda wa
hadi siku 21 pekee.
“Zikiisha siku hizo ikiwa
ndugu hawatajitokeza uongozi uandika barua maalum ambapo huwapa kibali
hamashauri ya jiji kuuchukua mwili huo na kwenda kuuzika,” anabainisha.
Anaongeza “Nimeshuhudia
maiti nyingi tu zikizikwa na halmashauri kwa sababu ndugu zao hawakujitokeza,
siwezi kukumbuka idadi kamili kwa sasa nadhani ni zaidi ya 80.
IDADI KWA SIKU
Anasema idadi hutofautiana
siku na siku kwamba kuna wakati hupokea maiti sita had inane na au asipokee
kabisa hata moja.
“Lakini muda wa kuisafisha
maiti na au kuifanyia uchunguzi hutegemeana na sababu ya kifo chake, kwa mfano
kama mtu amefia majini unakuta mwingine ameanza kuoza pale huwa ni kesi ngumu
kidogo.
KUHUSU MAJI YA MAITI
JAMVI LA HABARI liliuliza ukweli juu ya madai kwamba maji ya
maiti huweza kumsaidia binadamu kupata mafanikio kama wengi wanavyosema.
“Nimeyasikia hayo madai, ni
mambo yanayosikitisha na kushangaza mno, hakuna ukweli juu ya hilo, ni imani
potofu kabisa, binafsi siamini katika hilo,” anasema.
Anaongeza “Sisi hapa
Muhimbili haturuhisiwi kabisa kuuza maji ya maiti, ni kosa tena kubwa mno
kimaadili, marehemu anastahili heshima
pia.
MAFANIKIO LUKUKI
Anasema anajisikia fahari
kufanya kazi hiyo kwani ameweza kuwasomesha watoto wake hao na kujenga nyumba
huko Tandale ambako ndiko anakoishi.
“Nimeweza kujuana na watu wengi, leo hii naweza kufanya kazi popote pale, watu wananiamini, kumbuka nimekuambia sijasomea fani hii.
"Sina hata cheti lakini kuna vijana wanasoma
fani hii huko chuoni, wanakuja mafunzo kazini hapa Muhimbili, ninawapokea na
kuwafundisha kazi.
“Hili kwa hakika najivunia
kwamba wananisikiliza na wanavuna maarifa kutoka kwangu pia, wakienda chuoni
wanafaulu vizuri na kutunukiwa,” anasema.
Anaongeza “Nawasihi vijana wasiogope kufanya kazi hii, si kazi mbaya, binafsi najisikia fahari kumsaidia kumsitiri binadamu mwenzangu ambaye ametangulia mbele za haki.
".., na naamini siku
nikiondoka duniani na mimi nitasitiriwa vizuri na watakaokuwa wamebaki.
“Sijachoka kufanya kazi hii, bado natamani kuifanya ingawa mkataba wangu unaonesha utaisha mwaka 2021, ikiwa wataniongezea nipo tayari kuendelea kuifanya.
Chapisha Maoni