*Mfumo huo wanaongeza makusanyo, upatikanaji wa damu salama
*Mgonjwa
anayehitaji huongezewa bila ndugu kuitwa kujitolea
*Anaporuhusiwa huwa balozi wa uhamasishaji kwenye jamii
*Utaratibu
huo waondoa kero ya kukosekana kwa damu salama
NA Veronica Mrema – Mtwara
KUKUSANYA damu kutoka kwa wachangiaji wa ndugu wa mgonjwa
aliyelazwa wodini ni miongoni mwa mbinu zinazotumika katika maeneo mengi nchini
ili kuweza kupata damu kwa ajili ya kusaidia wale wanaokuwa na uhitaji kuweza
kuokoa maisha yao.
Tathmini ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama Tanzania (NBTS)
zinaonesha pia kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wachangiaji damu ni wanafunzi na
wanavyuo.
Hata hivyo, mambo ni tofauti katika Ukanda wa Kusini ambako
kuna Kanda ya NBTS, kwenyewe kiwango kikubwa cha damu salama kinakusanywa
kutoka kwa wachangiaji wa hiyari.
Wachangiaji wa hiyari kutoka moja kwa moja kwenye jamii
katika maeneo mengine wapo lakini si kwa kiwango kikubwa kama ambavyo Kanda ya
Kusini imefanikiwa kufikia.
Hatua ambayo Meneja wa Mpango huo unaosimamiwa na Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Kanda hiyo, Dk. Pendael
Sifuel anasema imewawezesha kuondoa kero na malalamiko ya ukosefu wa damu hata
wakati wa mapambano dhidi ya Janga la Corona.
Namna gani Kanda hiyo imeweza kufanikisha jambo hilo?
“Mgonjwa yeyote aliyelazwa wodini katika Kanda hii ya
Kusini ya NBTS, ambapo tunahudumia mikoa mitatu, , Lindi, Mtwara na Ruvuma
pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Tunduru na Namtumbo, akihitaji damu, huku
hatulazimishi ndugu, jamaa na marafiki waje wachangie, wajitolee damu.
“Tulishaachana na utaratibu huo, tulichofanya ni kwamba
mgonjwa husika anapatiwa damu iliyopo, akishapata huduma na kupona,
anaporuhusiwa kurudi kijijini, lazima aende akaripoti kwa uongozi kwamba
alisaidiwa kupatiwa damu alipokuwa wodini,” anasema.
Anaongeza “Kwa hiyo, yule ambaye tulimpa huduma ya damu
salama, sasa anakuwa sehemu ya uhamasishaji katika jamii yake, tunapokwenda
kukusanya damu, anakuwapo na kutoa ushuhuda.
“Jamii inahamasika kujitolea damu, tuliamua kwenda moja kwa
moja vijijini kwa sababu eneo hili (Kanda) ni dogo kulinganisha na Kanda
nyinginezo, sisi hapa tumewekeza zaidi kukusanya damu vijijini kwa sababu hata
shule zilizopo hapa ni chache, wakati mwingine huwa zinafungwa au kunakuwa na
mitihani.
“Lakini kule vijijini ndiko waliko wananchi wanapata huduma zetu hospitalini, hivyo tuliona bora kupeleka elimu kule kule vijijini,” anasema.
Mtaalamu wa Maabara wa NBTS Kanda ya Kusini, Kassim Mmera akionesha mazao ya damu yaliyohifadhiwa kwenye friji zilizopo ndani ya maabara hiyo.JINSI
WALIVYOANZA
Dk. Sifuel anasema walianza kwa kuwashirikisha wazo hilo
viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji kwamba kila mtu anayepatiwa huduma ya
damu salama hospitalini, anaporuhusiwa na kurudi kijijini kwanza lazima aripoti
kwa uongozi wa kijiji husika.
“Tulikubaliana kwamba mgonjwa akifika kwa daktari,
ikihitajika kuongezewa damu atapatiwa huduma pasipo kuambiwa kitu chochote,
hatatakiwa kuleta ndugu zake kumchangia.
“Ataongezewa ile iliyokusanywa na kuandaliwa tayari
kusaidia wahitaji, lakini akirudi kijijini lazima akaelezee kwamba amepatiwa
huduma ya damu bure, anakuwa balozi wetu anasaidia kwenye uhamasishaji,”
anasema.
Anaongeza “Hili limetusaidia mno kuongeza hamasa kwa
wananchi baada ya kuona huduma kweli inatolewa bure na hakuna usumbufu wa
kulazimika kuleta ndugu wala nini.
“Tukifika kule vijijini, wenyeviti na watendaji wanatueleza
endapo wanapata wagonjwa ili tuhakikishe wanapata huduma,” anasisitiza.
UMILIKI
KWA WANANCHI
“Kwa hiyo wananchi hapa wanamiliki mpango wa damu salama, wao
ndiyo wanapanga tufanye nini, sisi tunafanya nao kazi, mwitiko ni mkubwa na
mafanikio tuliyopata pia ni makubwa,” anasema Dk. Sifuel.
Anaongeza “Hii imetusaidia pia hata lilipokuja janga la maambukizi
ya Virusi vya Corona (COVID – 19), sisi tulijiwekea kauli mbiu yetu tukisema
damu salama Kanda ya Kusini, Corona haituwezi.
“Tulihakikisha tunafuata miongozo iliyotolewa na Wizara kujikinga
dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
“Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia sanitizers (vitakasa mikono), vitanda pia tunaweka kwa kuzingatia umbali wa mita moja, wataalamu wetu wanazingatia mbinu zote za kujikinga na kuwakinga wale wanaokuja kujitolea kuchangia damu, tuliamini Corona haituwezi na tumefanikiwa kupigana nayo," anabainisha.
Dk. Sifuel anasema hapo kabla hawajaanza kufuata utaratibu huo (wa mfumo wananchi 'kumiliki benki ya damu) wagonjwa walipolazimika kuleta ndugu wa kuwachangia damu, walikuwa wakipata ndugu watano pekee.
“Lakini kwa kufuata utaratibu huu mpya tuliojiwekea, kwa mgonjwa mmoja anapohamasisha, tunapokwenda kijijini tunakusanya chupa 25 hadi 50,” anabainisha.
Mkuu wa Maabara wa NBTS Kanda ya Kusini, Hamis Mohamed akifafanua jinsi wanavyotumia mfumo wa kulebo mazao ya damuWANAKIJIJI
WALIUMIA
Anaongeza “Utaratibu wa zamani tuliona ulikuwa unawaumiza
wagonjwa na hata ile kauli kwamba huduma hii ni bure, wengi wao walikuwa
hawaoni maana yake.
“Kwa mfano kama mtu amepanga, hana ndugu hapa mjini atapataje
hao ndugu wa kumchangia damu ilia pate huduma,!?,” anahoji.
Anasema kwa hiyo kwa utaratibu mpya, akilazwa anapewa damu
akitoka anakwenda kuhamasisha, kule kwenye jamii ndiko tunapopata wachangiaji
wa hiyari wengi.
“Kuliko kutegemea ndugu wa mgonjwa aliyelazwa wodini ambapo
pia tulibaini kwamba wengi wanapopona huwa hawaoni tena umuhimu wa kurudi
kuchangia damu, sasa kwa mfano kama watakaa miaka mitano hadi 10 hawajapata
mgonjwa, hautawapata kuja kuchangia,” anasema.
Daktari huyo anaongeza “Lakini akipewa mgonjwa mmoja, akienda akihamasisha tunapata wachangiaji wa hiyari wengi, kwa hiyo sasa kila mtu anamiliki damu salama.
MAHITAJI YA KANDA
Anasema kwa siku ni wastani wa chupa 100 ikiwa hakuna
mahitaji ya dharura na kwamba endapo dharura inatokea huweza kutuka chupa kati
ya 120 hadi 150 kwa siku.
“Kwa siku mahitaji yetu si makubwa, damu tunayokusanya
inatosheleza, kwa mfano kwa Hospitali ya Mkoa mahitaji yao kwa mwezi ni chupa
300, si matumizi makubwa sana,” anabainisha.
WAJAWAZITO
WAONGOZA
Anasema katika Kanda hiyo kundi linaloongoza kwa matumizi
ya damu salama ni lile la wajawazito kwa zaidi ya asilimia 60 hasa katika
kipindi cha kujifungua likifuatiliwa na kundi la watoto kwa asilimia 20.
“Kundi jingine ni la majeruhi wa ajali na wale
wanaokabiliwa na magonjwa mengine mbalimbali. Ndiyo maana tunasema tusiwasumbue
hasa hawa wakina mama, wakija kujifungua, wanahudumiwa, wanaenda nyumbani,
wakienda huko wanatusaidia kuhamasisha jamii,” anasema.
Anaongeza “Tunakusanya na kusambaza hata kwa hospitali binafsi na zile za ‘misheni’ zilizopo kwenye kanda hii ikiwa wanahitaji na si kwa hospitali za Serikali pekee.
UWEZO
WA MAABARA
Dk. Sifuel (pichani) anasema NBTS katika Kanda hiyo ilianzishwa mwaka 2007
wakati huo ikiwa chini ya CDC na kwamba ilifanya kazi vizuri hadi mwaka 2015
wafadhili hao walipoondoka na kuchukuliwa rasmi na Serikali chini ya Wizara
hiyo.
“Tangu hapo utendaji kazi kwa asilimia 100 unatekelezwa
chini ya Serikali, tangu ilipochukuliwa na Serikali hadi sasa tumepata
mafanikio mengi ikiwamo hiyo ya kuongezeka kwa hamasa ya wananchi,” anasema.
Anaongeza “Aidha, kiwango cha ukusanyaji damu nacho
kimekuwa kikiongezeka, mwaka 2017/18 tulikusanya chupa za damu 6,444, mwaka
2018/19 tulikusanya chupa 9,510 na mwaka 2019/20 kufikia sasa tumekusanya chupa
11,500.
“Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 113, tumevuka lengo
kwa sababu tumeweza kukusanya zaidi ya asilimia moja ya wakazi (population),
ushirikiano tunapata kule vijijini, idadi ya wachangiaji inaongezeka mwaka hadi
mwaka.
Anasema hata katika Halmashauri wanazoshirikiana nazo kwa
mwaka jana ziliweza kuvuka lengo ambapo zilikusanya chupa za damu 24,780 sawa
na 112% ya malengo waliyojiwekea.
“Tunafanya vizuri tunaishukuru Serikali kwa sababu imekuwa
ikisimamia vizuri, tumepata mashine za kisasa za upimaji kwa makundi ya damu na
magonjwa manne (Ukimwi, Homa ya Ini B na C na Kaswende).
“Kwa mashine tulizokuwa nazo awali majibu yalikuwa yanatoka
ndani ya siku tatu tangu tulipopokea sampuli na kuzichunguza, kwa mashine hizi
mpya sasa tuna uwezo wa kutoa majibu ndani ya siku moja,” anabainisha.
Anaongeza “Ikiwa kuna dharura, kwa mfano labda Halmashauri
inahitaji haraka, kwa mashine tulizonazo sasa tunao uwezo wa kuzifanyia kazi
sampuli tulizopokea na kutoa majibu ndani ya saa tatu na kuwarudishia.
“Uwasilishaji wa matokeo ya majibu ya sampuli tulizopokea
unafanyika kupitia mfumo maalum na mashine hizi zina uwezo wa kuchunguza zaidi
ya sampuli 100 kwa saa moja na dk. 10,” anasisitiza Mkuu wa Maabara hiyo, Hamis
Mohamed.
Anasema wanao uwezo pia ndani ya maabara hiyo kuchakata
mazao ya damu na kwamba plasma na chembe hai nyekundu ndizo ambazo hutumika kwa
wingi kuliko chembe sahani katika Kanda hiyo.
“Hata hivyo, chembe sahani huwa tunatengeneza kwa oda
maalum kutoka kwa daktari kwa sababu huwa zina uwezo wa kukaa ndani ya saa moja
hadi nane ziwe zimetumika, vinginevyo inaharibika, haifai tena kwa matumizi,”
anabainisha.
Anaongeza “Kwa upande wa plasma zenyewe huweza kukaa hadi
miezi 11 tangu imetengenezwa ndipo inaharibika, ndani ya dakika 14 hadi 20 tuna
uwezo wa kupata pakiti nne za damu na kuzihifadhi kwenye friza katika kiwango
cha baridi kinachoshauriwa kitaalamu tayari kwa matumizi.
Chapisha Maoni