Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi zawadi ya ngao yenye ramani ya Tanzania daktari bingwa wa magojwa ya moyo kwa watoto  kutoka nchini China Zhao Lijian ikiwa ni ishara ya kumshukuru baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi  kwa zaidi ya miaka miwili katika Taasisi hiyo. Katikati ni  kiongozi wa madaktari hao ambaye pia ni Daktari bingwa wa usingizi Qin Chengwei anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Madaktari Bingwa watatu wa magonjwa ya moyo ambao ni raia wa China wameagwa na uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) baada ya kumaliza muda wao wa kufanya kazi nchini.

Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kila baada ya miaka miwili huwa inatoa wataalamu wake kwenda nchi mbalimbali Barani Afrika kutoa huduma za matibabu.

Hivyo, madaktari hao akiwamo  daktari bingwa wa wagonjwa walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), daktari bingwa wa magojwa ya moyo kwa watoto na  daktari bingwa wa upasuaji wa moyo walikuwapo nchini baada ya kusainiana makubaliano hayo katika ya Serikali yao na Tanzania kupitia Wizaya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga madaktari hao mapema hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, amesema walikuwapo nchini kwa kipindi cha miaka miwili tangu tarehe 22 Juni, 2018 hadi kufikia mwaka huu.

“Madaktari hawa wamemaliza muda wao wa kufanya kazi nchini na wanatarajia kurudi nchini kwao katikati ya mwezi Oktoba, mwaka huu.

“Tumejifunza mengi kutoka kwao, tumeshirikiana nao kwa ukaribu, niliwaona ni sehemu ya timu yetu ya wataalamu mabingwa wa JKCI,” amesema.

Ameongeza “Wanarudi nchini kwao, tutaendelea kuwakumbuka kwa kazi nzuri waliyofanya hakika walishirikiana nasi kwa ukaribu mno, wameshakamilisha taratibu za kusafiri kurudi China.

“Wanapoondoka tunatarajia timu nyingine ya wataalamu kutoka China ambao wameshakamilisha taratibu za kuja nchini, tutaungana nao kuendelea kuimarisha huduma zetu,” amebainisha.

Akizungumza kiongozi wa timu hiyo ya madaktari kutoka China waliokuja nchini kushirikiana na JKCI ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Usingizi anayefanya kazi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Qin Chengwei, amesema kipindi hicho ya mashirikiano kimekuwa chenye manufaa kwa pande zote mbili.

“Binafsi naona miaka miwili imeisha haraka mno, mmeshirikiana vizuri mno na wataalamu wetu, tunashukuru, kwa zaidi ya miaka 50 sasa Serikali yetu imekuwa ikituma madaktari nchi mbalimbali za Afrika.

“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na kuipa kipaumbele Tanzania, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, kuendelea kuleta wataalamu wetu kufanya nao kazi,” amesema.

Ameongeza “Tunaamini kwa jinsi mlivyofanya kazi na timu hii inayomaliza muda wake, mtafanya hivyo pia kwa timu ya wataalamu tunayoitarajia kuja nchini Tanzania wakati wowote kuanzia sasa.

Mmoja wa madaktari hao, Dk. Hu Bin ameshukuru uongozi wa Taasisi hiyo na wafanyakazi wote kwa kufanya nao kazi vizuri katika kipindi chote walichoishi nchini.

“Niliishi hapa kama nyumbani, mmekuwa nasi katika nyakati zote, kila hatua, hakika niliona JKCI ni hospitali yangu, ya maisha yangu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi zawadi ya ngao yenye ramani ya Tanzania na cheti daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka nchini China Hu Bin ikiwa ni ishara ya kumshukuru baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi  kwa zaidi ya miaka miwili katika taasisi hiyo. Kulia ni  kiongozi wa madaktari hao ambaye pia ni Daktari bingwa wa usingizi Qin Chengwei anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi zawadi ya picha yenye mchoro wa tingatinga daktari bingwa wa wagonjwa walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutoka nchini China Cui Jian ikiwa ni ishara ya kumshukuru baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi katika Taasisi hiyo. Mwezi wa sita mwaka  2018 Serikali ya China ilitoa  madaktari bingwa 11 kuja kufanya kazi hapa nchini wakiwemo madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo.

Kiongozi wa madaktari kutoka nchini China ambao wanafanya kazi hapa nchini ambaye pia ni Daktari bingwa wa usingizi Qin Chengwei katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiishukuru menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa jinsi walivyoshirikiana na Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo watatu ambao wamefanya kazi katika Taasisi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini China mara baada kumaliza kuwaaga kutokana na  muda wao wa kufanya kazi  kwa zaidi ya miaka miwili katika Taasisi hiyo kumaliza. Mwezi wa sita mwaka  2018 Serikali ya China ilitoa  madaktari bingwa kuja kufanya kazi hapa nchini wakiwemo madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo.

Madaktari Bingwa wa magojwa ya moyo kutoka nchini China wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuagwa na Menejimenti  ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambako walikuwa wanafanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili. Mwezi wa sita mwaka  2018 Serikali ya China ilitoa  madaktari bingwa 11 kuja kufanya kazi hapa nchini wakiwemo madaktari watatu wa magonjwa ya moyo.

Picha na JKCI.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement