Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Mtaalamu Bingwa wa Matumizi ya Mionzi katika uchunguzi wa magonjwa ya saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Stephen Mkoloma (mbele) akiwasilisha mada wakati wa semina hiyo mapema leo.

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Michoro ya alama za tattoo kifuani (kwenye matiti) ni kikwazo katika kufanikisha uchunguzi wa saratani ya matiti kwa kutumia kipimo cha Mammography.

Yamebainishwa hayo leo na Mtaalamu Bingwa wa Matumizi ya Mionzi katika Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Stephen Mkoloma.

Mkoloma alikuwa akiwasilisha mada katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi zaidi ya 25 wa taasisi hiyo, iliyolenga kuwapa uelewa juu ya kipimo hicho cha kisasa kilichosimikwa na Serikali hivi karibuni ndani ya taasisi hiyo.

Amesema licha ya kipimo hicho kuwa na uwezo mkubwa katika  kugundua saratani ya matiti kwa kiwango cha wastani wa asilimia 80 hadi 90 lakini endapo mgonjwa husika amechora tattoo kifuani mwake huwa changamoto kubwa katika kutambua picha za majibu yake.

“Tatoo ni miongoni mwa vitu ambavyo havipitishi mionzi wakati wa upimaji ili kuweza kugundua kama mgonjwa ana saratani ya matiti au la!, ‘tunapoituma’ mionzi kwenye matiti zile tattoo kwa kuwa hazipitishi mionzi, zitaonekana moja kwa moja kama zilivyo kwenye picha zetu, hii ni changamoto.

“Ni rahisi kuchanganya katika mtiririko wa matibabu ya mgonjwa, kwa sababu si mtaalamu mmoja ambaye anamuona mgonjwa, wapo ambao huiona picha tu, sasa mtaalamu anapoiona picha anaweza kudhani ni tatizo kumbe la hasha ni urembo tu wa muhusika,” amesema.

Ameongeza “Tunaishauri jamii hasa vijana kuepuka kuchora tattoo kwenye maeneo ya mwili hasa matiti, kwa sababu tunapata tabu kufanya uchunguzi.

“Kuna wengine wanaweka hereni kama urembo, hawa wakija hatutaweza kuwafanyia uchunguzi kwa mashine hii, labda kama wataondoa kwanza vinginevyo tutatumia mashine nyingine ambazo tunazo kuwachunguza,” amebainisha.

Mtaalamu hiyo amesema mashine hiyo ya Mammography ni maalum ikitumia mionzi midogo katika uchunguzi wa saratani hiyo kwenye titi kwa sababu matiti ni sehemu ambazo seli zake zinaweza kuathirika zaidi mionzi inapokuwa mikubwa.

Amesema wenye umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea ndiyo wanaoshauriwa kuchunguzwa kwa kutumia mashine hiyo.

“Mgonjwa akija tunashauri asipake ‘diodolant’ (pafyumu), ‘losheni’, poda au mafuta eneo la kifua, matiti na kwapa, maana bidhaa hizo zina kemikali ambazo hazipitishi mionzi zinaweza kuonekana kwenye picha ya titi la mgonjwa ikatuchanganya tukadhani ni tatizo kumbe la hasha.

“Mwanamke akiwa kwenye hedhi hawezi kufanyiwa uchunguzi kwa kipimo hiki au akiwa katika kipindi cha kushika ujauzito (ovulation),” amebainisha.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa amesema pamoja na jitihada za Serikali kuboresha huduma za uchunguzi na tiba katika taasisi hiyo bado kuna mwamko mdogo kwa wananchi kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani hiyo.

“Ushiriki wa wananchi kufanya uchunguzi wa awali wa saratani hii tunaona mwitiko si mkubwa kulinganisha na tatizo lilivyo katika nchi yetu, taasisi imejikita kutoa elimu kuhusu vihatarishi na visababishi vinavyoweza kuchangia mtu kupata saratani hii na nyinginezo.

“Tumeboresha huduma zetu katika kitengo cha uchunguzi wa awali, Serikali imenunua mashine hii ya kisasa iliyotengenezwa mwaka 2019 kwa Sh. milioni 189, yenye uwezo wa kugundua saratani ya matiti mapema sana.

“Tumeboresha huduma za upatikanaji wa dawa za saratani za kemikali sasa ni wa kiwango cha asilmia 94,” amesema.

Ameongeza “Tumeanza mafunzo kwa wafanyakazi wetu kuwapa uelewa wa mashine hii kwa sababu tumefanya maboresho kuhakikisha hospitali hii inakuwa ya mfano katika utoaji matibabu katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

“Saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa kwenye taasisi yetu, kati ya wagonjwa 100 wanane wanaugua saratani hii na kundi linaloathirika hivi sasa linaonekana ni la wenye umri mdogo kulinganisha na miaka ya nyuma,” amesema.

Amesema hata wastani wa umri umepungua kutoka miaka 70 hadi 57 na hata wale wenye umri wa miaka 24 kitu ambacho hakikuwa cha kawaida na wengi hufika ugonjwa ukiwa kwenye hatua za juu.

Wafanyakazi wa Ocean Road wakiendelea kumsikiliza mtaalamu huyo (hayupo pichani) wakati wa semina hiyo mapema leo.
Wataalamu wa Ocean Road wakimsikiliza mtaalamu huyo (hayupo pichani) wakati wa semina hiyo mapema leo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement