Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Alipofikisha umri wa miaka 40, Nyakolema Silla Bhoke
aligundulika ana ugonjwa wa saratani ya matiti, ilikuwa ni miaka minne tangu
alipofunga ndoa na mwenza wake (hakupenda jina lake liandike).
Nyakolema anasimulia kwamba aliolewa akiwa na umri wa miaka
36, katika kipindi chote cha mapenzi yao ‘motomoto’ hawakubahatika
kupata mtoto na mumewe.
“Ndoa yetu ilijawa furaha na mahaba tele, tulipendana mno
na mume wangu, kipindi chote hatukukata tamaa ya ‘kutafuta’ mtoto,” anasema.
Anaongeza “Lakini nilipogundulika nina saratani ya matiti
na daktari kushauri ziwa langu likatwe ili kutibu, hapo ndipo penzi letu
‘liliota mbawa’.
ALIVYOHISI TOFAUTI
Nyakolema anasema mkasa aliokutana nao katika
maisha yake ni mtihani mzito anaokabiliana nao lakini hajakata tamaa akiamini
ipo siku Mwenyezi Mungu atamfuta machozi.
“Kabla sijagundulika hospitalini, mimi mwenyewe siku moja nilihisi tofauti katika mwili wangu,
nilipojikagua maziwa yangu, nilistaajabu nilipoona chuchu ya ziwa langu la
kushoto imeingia ndani tofauti na chuchu ya ziwa langu la kulia.
“Nilianza kulifuatilia kila siku, mimi ni mkazi wa Dar es
Salaam, lakini kipindi kile nilikuwa safarini Kanda ya Ziwa, Mkoani
Mara, ziwa langu lilizidi kuvimba na kunistaajabisha,” anasimulia.
Anaongeza “Nilianza kuperuzi mitandaoni, nilisoma maandiko
mengi, katika andiko moja niliona wakieleza kwamba chuchu kuingia ndani ni
miongoni mwa dalili za awali za saratani ya matiti.
Anasema aliporudi Dar es Salaam aliamua kwenda Taasisi ya
Saratani Ocean Road, kwa sababu alikuwa anafahamu ndiyo taasisi ya Umma inayohusika na magonjwa ya saratani.
“Nilifanyiwa uchunguzi wa awali (kulipapasa ziwa) wakabaini
kweli kulikuwa na uvimbe, wakanichukua sampuli ya majimaji ili wahakikishe kwa
vipimo vya maabara iwapo uvimbe ule ulikuwa wa kawaida au saratani.
“Vipimo vilipotoka, majibu yalionesha nina saratani ya
matiti, daktari alishauri nirudi baada ya siku kadhaa ili wachunguze tena
kujiridhisha, ikionekana tena ni saratani basi matibabu yake ni kukatwa ziwa,”
anasema.
Nyakolema anasimulia “Dah!... baada ya kuelezwa hayo,
kwangu ikawa changamoto, nikatwe ziwa?... nikajiuliza itakuwaje?... maana
ukiangalia ni kitambulisho cha mwanamke, halafu kiondolewe!... ilikuwa mtihani
mzito kwangu.
ALIHANGAIKA
“Basi kabla sijarudi tena Ocean Road, niliamua kwenda
hospitali nyingine ili nako wanichunguze, nilikwenda Aghakan majibu yalipotoka
bado yalionesha nina saratani ya matiti,” anasema.
Anaongeza “Daktari alinieleza vile vile kwamba matibabu ni
kukatwa ziwa.
“Ilibidi nilimuuliza. Hamuwezi kuondoa hako ka-uvimbe maana
wakati ule kalikuwa bado kadogo? Daktari alinieleza kulingana na sehemu
ka-uvimbe kalipokaa ilikuwa lazima waondoe ziwa lote.
“Maana waki-kiondoa tu chenyewe (ka-uvimbe), titi
lisingekuwa na ‘shepu’ (muonekano),” anasema.
Anasema ingawa alielezwa hayo bado aliamua kwenda tena
hospitali nyingine kufanyiwa uchunguzi akiamini huko pengine angepata majibu
tofauti.
“Nilikwenda hospitali moja huko Temeke, majibu yalikuwa
yale yale kama niliyoelezwa kule kwengine, nilifika hadi Hospitali ya Taifa
Muhimbili, majibu bado yalikuwa yale yale,” anasema.
Anaongeza “Niliamua kurudi Ocean Road, kwa sababu niliona
kadri ninavyohangaika kuzunguka huku na kule, ndivyo nilivyokuwa najiweka
kwenye hatari ya kusambaa kwa saratani kwenye mwili wangu.
UPASUAJI KULIONDOA
Nyakolema anasema daktari alimchunguza tena na
kujihakikishia ni saratani, alimuandikia rufaa kwenda Muhimbili (Mloganzila)
kwa ajili ya upasuaji wa kuliondoa titi lake.
“Nililazwa Mloganzila, nilichukuliwa vipimo kwa ajili ya maandalizi ya upasuaji, yalipokamilika, nilifanyiwa upasuaji, walilikata, hali yangu ya afya ilipoimarika, niliruhusiwa,” anasimulia.
Nyakolema Silla Bhoke ambaye sasa anatumia titi la bandia akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya hivi karibuni.HOFU YA KIFO
Anaongeza “Waliponiruhusu walinieleza upasuaji wa kuliondoa ni sehemu ya mwanzo ya matibabu, hivyo lazima nirudi Ocean Road kwa matibabu zaidi ya mionzi, nilipata hofu kubwa maana nilishawahi kusikia simulizi kwamba inaua.
“Watu walidai wanaotibiwa huko wanakufa,
wakati huo sikuwa najua kwamba kuna tiba nyingine ya kemia (chemotherapy),
daktari alinisaidia kunielewesha, hofu ikanitoka.
HOMONI ZILICHANGIA
Nyakolema anasema kwenye ukoo na familia yao yeye ndiye wa
kwanza kugundulika kuugua ugonjwa huo hospitalini, hali iliyomshangaza.
“Hivyo, niliwauliza wataalamu kitu gani kilichangia mimi kupata saratani hii, niliulizwa kama niliwahi kupata ujauzito na kunyonyesha... nilijibu hapana... basi nilielezwa kwamba homoni zangu za mwili kwa sababu nilichelewa kuzaa na kunyonyesha, nilichelewa kuolewa,” anasimulia.
Anaongeza “Kwa mujibu wa wataalamu homoni zimechangia, kwa sababu ... wanasema mwanamke
akinyonyesha inavyotakiwa kuna kemikali inaachiliwa mwilini mwake na kumkinga dhidi ya
saratani ya matiti na mtoto lazima anyonyeshwe miaka miwili.
“Daktari alinieleza pia kubadilika badilika kwa mzunguko wa
hedhi si suala la kupuuzia, sasa mimi nilikuwa nakaa hata miezi miwili, sijaona
siku zangu niliona ni jambo la kawaida, kumbe la hasha! Nilipaswa kwenda
hospitalini kufanyiwa uchunguzi na tiba.
MUME ‘AMKIMBIA’
Nyakolema anasema alisubiri hadi kidonda kilipofunga vizuri, alianza ‘safari’ ya tiba kemi pamoja na ile ya mionzi, katika hatua zote za
awali mume alikuwa bega kwa bega pamoja naye alimtia moyo asikate tamaa atapona
maradhi hayo.
“Kwa kweli, nilipogundulika nina saratani, yeye alikuwa
mbali, safarini kikazi, hivyo kipindi chote tulikuwa tunawasiliana kwa njia ya
simu, taratibu mawasiliano yetu yalianza kupungua.
“Hakuwa ananitafuta kama alivyokuwa anafanya awali, alianza
kunikwepa taratibu, mwisho ‘akaenda na upepo wa kisulisuli’, akaniacha, mpaka
sasa nipo mwenyewe, sijui aliko.
“Nikitafaki huwa najisemea mwenyewe labda aliona simfai
tena kwa sababu sijamzalia hata mtoto mmoja na sasa sina ziwa moja tena,”
anasimulia kwa huzuni.
Anaongeza “Lakini sijakata tamaa bado napambana na matibabu,
sijawahi kutetereka, afya yangu inaimarika, ukweli kuna changamoto kwenye hizi
dawa mtu anapoanza matibabu.
“Lakini mimi hazijawahi kunisumbua, wapo wanaopata
kichechefu, wanatapika, wanashindwa kula na hata kutotamani kuhisi harufu
yoyote, kwangu haijawahi kunitokea hali hizo.
“Kila ninapokwenda kliniki wataalamu wananipima kinga zangu
za mwili na wingi wa damu, nilipatiwa mizunguko minne ya tiba mionzi, ingawa
awali niliandikiwa mizunguko sita, walinipunguzia kwani hali yangu inaimarika,
sasa nimemaliza, namshukuru Mwenyezi Mungu,” anasema.
Anaongeza “Kwa sasa naendelea kupata dawa kidonge kimoja
kila siku kwa muda wa miaka miwili ambazo ni kama kinga, ili kuzuia saratani
isirudi kwa sababu hizi ni seli za mwili ambazo huwa zinajiongeza bila
utaratibu.
“Sasa mimi ni shujaa, nimepona saratani naendelea
kufuatiliwa hali yangu ili kuzuia isirudi, watanifuatilia kwa miaka mitano,
naendelea na maisha yangu kama kawaida, 'nakula bata' (raha).
Anasema bado ana matumaini makubwa kwamba atakapomaliza
matibabu ataweza ‘kushika’ ujauzito kama wanawake wengine, kuzaa na
kunyonyesha.
DAKTARI ANENA
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Kitengo cha
Uchunguzi wa ORCI, Maguha Stephano anasema ingawa jinsi zote wana matiti lakini
kwa asilimia 99 huathiri wanawake na wanaume asilimia moja.
“Kuna visababishi mbalimbali vinaweza kuchangia, naweza
kuviweka katika makundi mawili, vinavyozuilika na visivyozuilika,” anasema.
Anaongeza “Visivyozuilika ni vile tunavyozaliwa navyo, ukiwa
jinsi ya kike upo kwenye hatari zaidi kuliko jinsi ya kiume. Kurithi pia ni
kisababishi kingine ambacho hakizuiliki, kama ndugu wa karibu (wa damu) kwa mfano shangazi, bibi, mama aliwahi kuugua nawe upo hatarini.
Dk. Maguha anasema inashauriwa mwanamke anyonyeshe angalau
miaka miwili lakini ikiwa hatanyonyesha kabisa au akanyonyesha kwa kipindi
kifupi anajiweka kwenye hatari ya kupata saratani hiyo.
“Mwili wa mwanamke una homoni iitwayo oestrogen,
anaponyonyesha kiwango cha homoni hii hushuka na hivyo kumkinga dhidi ya
saratani ya matiti, kuliko yule asiyenyonyesha,” anafafanua.
Anaongeza “Mwanamke anaponyonyesha kuna faida nyingine pia
kwa mtoto kupata virutubisho muhimu kwa ukuaji wa afya ya mwili na akili na
‘kujenga’ ukaribu na mama yake.
VISABABISHI VINGINE
Dk. Maguha anasema licha ya kichocheo hicho cha oestrogen
vipo pia visababishi vingine vinavyoweza kuchangia mwanamke kupata saratani
hiyo.
“Suala la mtindo mbovu wa maisha, unene uliopitiliza, uzito
mkubwa, kutokufanya mazoezi mara kwa mara, kujifungua katika umri mkubwa.
“Siku hizi wapo wanaopata hedhi mapema na wengine
wanachelewa kukoma, maana yake ni kwamba kiwango kile cha homoni ya eoestrogen
huwa kingi kwa wakati mwingi na hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata saratani
hii,” anabainisha.
Anaongeza “Ndiyo maana tunashauri kufanya uchunguzi wa mara
kwa mara ili kama mtu ana saratani hii aweze kugundulika na kutibiwa mapema,
kwani ikigundulika mapema katika hatua ya kwanza na ya pili ni rahisi kutibika na kupona kuliko akichelewa hadi hatua ya tatu na nne ya ugonjwa.
MAKADIRIO YA WHO
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa
anasema kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Globalcan za 2018, inakadiriwa kila mwaka kuna zaidi ya wagonjwa 42,060 wa saratani nchini Tanzania,
asilimia 7.2 kati ya hao ni wa saratani ya matiti.
“Takwimu zetu nchini zinaonesha mwaka 2018 wagonjwa wa saratani walioweza kuhudhuria hospitalini ni zaidi ya 12,215 kati ya hao 42,060 wanaokadiriwa, kati ya hao 12,215 walioweza kuhudhuria wanawake waliogundulika kuugua saratani ya matiti walichukua asilimia 16 ya wagonjwa wote.
Dk. Kahesa anasema takwimu za ORCI zinaonesha saratani ya
matiti ni tatizo kubwa ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya
wagonjwa, baada ya saratani ya kizazi na saratani ya tezidume.
“Wastani wa umri wa wanawake wanaogundulika kuugua hii ORCI nao umeshuka, takwimu zetu zinaonesha mwaka 2008/09 wanawake waliokutwa wakiugua
walianzia miaka 64 lakini mwaka 2019 walianzia miaka 56 na wapo hadi wenye umri
wa miaka 25 wamegundulika," anabainisha.
HUDUMA YA UPANDIKIZAJI
Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage anasema “Saratani ya matiti ni saratani inayoongezeka kwa kasi nchini.
"Miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa hapa ORCI sasa hivi inashika nafasi ya pili.
“Changamoto tunayoiona hivi sasa kwenye jamii ni wimbi la
taarifa potofu zilizopo kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wagonjwa
hushawishiwa kwenda kupata dawa za kienyeji ambazo hata hazijafanyiwa utafiti
na hivyo huacha tiba za hospitalini.
“Hatujafanya utafiti kamili ila tunakadiria asilimia 10 ya
wagonjwa wa saratani zote tunaowatibu hukacha matibabu, huondoka wodini na
kwenda kwa waganga wa kienyeji au kwenye maombezi.
“Wengine hupoteza maisha huko na wale wachache wanaorudi
ugonjwa huwa upo hatua za juu, tiba huwa ngumu, wanapoteza maisha,”
anabainisha.
Anaongeza “Tunasisitiza wazingatie matibabu, hata wakienda
huko, wasiache matibabu, Serikali inazidi kuboresha huduma, sasa tunao uwezo wa
kuigundua mapema na kuitibu pasipo kuondoa titi lote, ikiwa mtu atagundulika
mapema.
“Kila mwaka tunatibu kwa njia hii ya upasuaji pasipo kuondoa titi lote, wanawake 100 ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya wagonjwa wote tunaowatibu, tunayo, kwa wale waliofanyiwa upasuaji na kuondolewa katika titi lote jitihada zinafanyika.
"Hivi sasa wataalamu wetu wapo China wakijifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza matiti, walikuwa wawe wameshamaliza masomo yao na kurejea nchini tayari kuanzisha huduma hii,” anasisitiza.
Chapisha Maoni