Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Wajumbe wa  Baraza la  Wafanyakazi wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada ya sheria za kazi wakati wa kikao cha  nne  cha baraza hilo  kilichofanyika leo jijini Dar es salaam.Jumla ya wajumbe 59 walihudhuria kikao hicho. 


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Kila mwaka Tanzania itapata wataalamu mabingwa 10 wa moyo wanaofundishwa ndani ya nchi kupitia madaktari bingwa wakufunzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Yamebainishwa hayo leo na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alipozungumza na waandishi wa habari mafanikio mbalimbali ambayo taasisi hiyo imeyapata wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichokutana leo jijini hapa.

“JKCI tunatoa mafunzo kwa kushirikiana na MUHAS Baraza hili limekuwa la mafanikio linatuunganisha uongozi wa juu na wafanyakazi kuweza kufahamu huduma tunazotoa, changamoto ni zipi na wapi tunaelekea, lina wawakilishi 62 kutoka kila idara.

“Tunajivunia Baraza hili, JKCI ni Taasisi pekee ya umma kubwa inayotoa matibabu haya nchini, lakini hii si hospitali tu, imekuwa pia sehemu kubwa ya mafunzo kwa madaktari na wauguzi, kwa kuwa sisi si chuo, tunashirikiana kwa ukaribu na MUHAS, mwaka huu watahitimu wataalamu saba na kuanzia mwaka ujao wa masomo tunatarajia watahitimu wataalamu 10,” amesema.

Ameongeza “Kwa mfano hizi digrii za pili za uzamili kwa mfano ‘masters in cardiology’ ya miaka miwili, asilimia 96 ya walimu wanatoka JKCI kwa ushirikiano na Muhas tunatoa hizi kozi.

“Kuna kozi mpya ya upasuaji wa kifua ambayo imeanzishwa kati ya walimu sita kati ya wanane wanatoka JKCI, ni hatua kubwa ambayo taasisi imepitia kuwa kitivo cha ‘uzalishaji’ wataalamu mabingwa wa moyo nchini.

“Zaidi ya asilimia 90 ya wataalamu mabingwa wa moyo nchini hivi wapo JKCI, uwiano kwa nchi zetu zote Afrika bado si mzuri, kwa mfano sisi ndiyo hospitali kubwa kuliko zote si tu Tanzania bali katika Ukanda wote huu wa Afrika Mashariki na Kati.

“Juhudi zimefanyika kubwa sasa hivi Dodoma (Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeanzisha kitengo cha moyo tunashirikiana nao kwa ukaribu vile vile KCMC (Hospitali ya Rufaa ya Kanda) nayo imeanzisha kitengo na tunafanya nao kazi kwa ukaribu,” amebainisha.

Ameongeza “Hivyo kila mwaka Tanzania tunatarajia ‘tutazalisha’ madaktari kati ya 10 na 13, hii ni namba kubwa mno.

“Kwa hiyo tunajivunia utulivu mkubwa uliopo kwenye Baraza hili, menejimenti inaongoza wafanyakazi 310 na wote wanahitaji kupata huduma wanazostahili ili wananchi wapate huduma ambazo nchi inafikiria kuzitoa kwao.

Awali, Katibu wa Baraza Hilo, Dk. Samwel Rweyemamu, amesema baraza hilo limekuwa likihakikisha linasimamia kwa dhati maslahi ya wafanyakazi ili kuimarisha morali ya utendaji kazi kwa maslahi mapana ya wananchi wanaowahudumia.

“Kwa mfano kila mwaka tumekuwa tukitambua mfanyakazi bora, tumependekeza pia iwe wafanyakazi watatu bora kila mwaka, yaani mshindi wa kwanza, pili na tatu ili kuwapa motisho na hamasa wafanyakazi kuendelea kufanya vema zaidi,” amebainisha.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wajumbe wa baraza hilo wakati wa kikao cha  nne cha baraza kilichofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Katibu Msaidizi wa Baraza hilo Renatha Miiruko.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya  Tiba Shirikishi wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delila Kimambo akieleza kazi zilizofanywa na kurugenzi yake  wakati wa kikao cha nne cha  baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo  kilichofanyika leo jijini Dar es salaam. 

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement