Na Veronica Mrema - Dar es Salaam
Hatua hiyo inalenga kuboresha utoaji huduma ya matibabu kwa wagonjwa hao ili wasilazimike kulala wodini wakipata matibabu hayo, kupitia teknolojia hiyo wataalamu hufanya upasuaji mdogo na kuweka njia (tube) maalum kwa ajili ya kuweka dawa chini ya ngozi.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani Ocean Road, Dk.
Crispin Kahesa amesema hayo alipozungumza na MATUKIO NA MAISHA BLOG katika mahojiano maalum.
Dk. Kahesa amesema kupitia teknolojia hiyo kwa kuwa mgonjwa halazwi wodini ana uwezo wa kuendelea na matibabu huku akitekeleza majukumu yake ya kila siku.
“Serikali imeboresha huduma za upatikanaji wa dawa za
saratani ndani ya taasisi kwa sasa upatikanaji wa dawa ni wa kiwango cha
asilimia 94,” amesisitiza.
Ameongeza “Katika kuendelea kuboresha huduma zetu, tumepata
mfumo mpya mwingine wa utoaji dawa kwa wagonjwa tunaowahudumia, zamani tulikuwa
tunatoa dawa kwa njia ya dripu lakini sasa tuna maboresho.
“Tunao mfumo mwingine ambapo dawa ile ile badala ya mgonjwa
kuwekewa kwa njia ya dripu, tuna njia nyepesi ya kumuwekea chini ya ngozi hii
ni teknolojia ya kisasa, madhara ni madogo na inampa mgonjwa nafasi ya
kuendelea na shughuli zake za kila siku,” amesema.
Amefafanua “Kwa njia ya dripu ililazimu mgonjwa aje
hospitalini, akae wodini tumuwekee lakini kwa njia hii ya teknolojia ya kisasa,
atafanyiwa upasuaji mdogo kuweka ‘tube’ itakayokuwa inatumika kupitishia dawa
kwenda chini ya ngozi na kurudi zake nyumbani.
“Hatalazimika kukaa hospitalini, dawa itakuwa inatoka
taratibu kwenye ‘ki-pakti’ chake na kupita kwenye mishipa midogo ya damu kwenda
mwilini mwa mgonjwa kupambana na saratani.
“Kwa njia ya dripu tulikuwa tunalazimika kutafuta mshipa
mkubwa wa damu ndipo tumuwekee mgonjwa dawa ndiyo maana ilikuwa lazima mgonjwa
akae mule mule wodini,” amesema Dk. Kahesa ambaye pia ni Bingwa wa Magonjwa ya
Saratani katika Taasisi hiyo.
Amesema teknolojia ya kisasa wanayotumia ni rafiki kwa
mteja na inayobebeka kirahisi (portable).
“Changamoto iliyosalia ni kwa upande wa huduma ya upasuaji,
wagonjwa wetu wanaohitaji upasuaji sasa hivi wanalazimika kwenda kwenye
hospitali nyingine ambazo tunashirikiana nazo zikiwamo za kanda na za mikoa
ambako kuna mabingwa wa upasuaji.
“Wakishafanyiwa wanarudi ili tuendelee kuwahudumia kwa tiba
nyingine tulizonazo hapa, tunatafuta mwarobaini wa kuondoa adha hii bado kwa
huduma za upasuaji tunataka wagonjwa wapate bila kupata adha tupunguze muda wa
mgonjwa kuzungunka.
Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage amesema
wanatoa tiba hiyo ya teknolojia ya kisasa kwa kushirikiana na Kampuni ya Roche Pharmaceuticals.
“Tunazidi kuboresha huduma zetu, lengo letu ni kuhakikisha kwamba Taasisi hii inakuwa bora katika utoaji huduma za uchunguzi na matibabu dhidi ya saratani si tu Tanzania bali pia katika Bara la Afrika,” amesisitiza.
Chapisha Maoni