Na Veronica Mrema - Dar es Salaam
Maendeleo ya sayansi na teknolojia sasa yanawezesha
wataalamu wa afya kutumia chupa moja ile ile ya damu kutoka kwa mchangiaji
mmoja kuweza kuokoa maisha ya watu watatu wenye uhitaji wa kuongezewa damu.
Wataalamu hao wanao uwezo wa kuvuna mazao yanayopatikana
kwenye damu na kuyahifadhi vema kitaalamu kwa ajili ya matumizi pale
yanapohitajika.
Kwa mujibu wa wataalamu chupa moja ya damu ina ujazo wa
mililita 450 sawa na chupa moja ya soda na kidogo, huenda msomaji wetu wa MATUKIO NA MAISHA BLOG unajiuliza mazao ya damu ni yapi?.
“Damu ina mazao makuu matatu ambayo ni chembechembe
nyekundu (packed Red Blood), chembe sahani (Platelets) na Plasma (Fresh Frozen
Plasma),” anabainisha Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama
Tanzania (NBTS), Dk. Magdalena Liymo katika mahojiano maalum na BLOG HII.
Dk. Magdalena anaongeza “Chembe nyekundu husaidia kubeba
oksijeni mwilini, chembe sahani husaidia damu kuganda, watumiaji wakubwa wa
chembe sahani ni wagonjwa wa saratani.
“Plasma ni kimiminika ambacho kinatengenezwa kutoka kwenye
damu na kina ‘protein’ ambazo husaidia kugandisha damu isiendelee kutoka hasa
kwa mama wajawazito, wanaotokwa damu wakati wa uzazi.
Dk. Magdalena anasema Tanzania hivi sasa inajikita zaidi
katika matibabu ya kibingwa na yale ya ubingwa wa juu, hivyo NBTS nayo inazidi
kuongeza kasi ya ukusanyaji wa damu (salama) na uzalishaji wa mazao ya damu.
“Imezoeleka kwamba NBTS huwa tunakusanya damu, ni jukumu
letu la msingi lakini kwenye kuboresha huduma za afya hatuwezi kuitumia damu
yote kama ilivyokusanywa (chupa moja nzima kwa mtu mmoja).
“Hivi sasa kuna huduma za kibingwa na za ubingwa wa juu ambazo
zinaendelea kufanyika kwenye hospitali zetu kubwa ikiwamo Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) na katika hospitali za rufaa za kanda.
“Kwa mfano upandikizaji figo, mishipa ya damu na hivi
karibuni nchi yetu inatarajia kuanza upandikizaji wa uloto Muhimbili, haya ni
matibabu ya ubingwa wa juu, maana yake ni kwamba, nchi yetu tunaongeza matumizi
ya mazao ya damu.
“Ili kuboresha huduma za afya hatuwezi kutumia ‘all blood’, NBTS tunataka kuboresha zaidi eneo hili la uzalishaji mazao ya damu ili… kwa mfano ikiwa kuna mtu anahitaji chembe sahani awekewe, akiwepo anayehitaji plazima awekewe, kila Mgonjwa anatakiwa apate 'right product',” anabainisha.
Chupa moja (unit moja) ya damu kutoka kwa mtu mmoja ina uwezo wa kutoa aina tatu za mazao ya damu na hivyo kuweza kuokoa uhai wa wagonjwa watatu wenye uhitaji.MASHINE
ZA KISASA
Anaongeza “Ndani ya kipindi cha uongozi wa Serikali ya
awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, tumepata mafanikio makubwa
ikiwamo kupata mashine za kisasa zenye uwezo wa kuchunguza sampuli nyingi
za damu ndani ya saa chache, tofauti na hapo awali.
“Tumepata mashine mpya 24 ambazo zimesambazwa katika kila
kituo kwenye kanda sita tulizonazo, kila kanda zimesimikwa mashine nne, mashine
hizi nne gharama yake ni Sh. bil 13.2,” anabainisha.
Dk. Magdalena anasema mashine hizo nne zilizosimikwa kwenye
kila kanda, mashine mbili ni maalum kwa ajili ya kuchunguza maambukizi
katika damu na mbili nyingine ni kwa ajili ya kutambua kundi
la damu.
Anaongeza “Mashine za kupima makundi ya damu zina
uwezo wa kupima sampuli 156 ndani ya masaa mawili.
Anasema kwa upande wa mashine zinazopima maambuki, kila
chupa inayokusanywa hupimwa maambukizi ya magonjwa manne ukiwamo ugonjwa wa
Ukimwi, Virusi vya Homa ya ini B na C pamoja na kaswende.
“Hivyo, katika kila chupa ya damu inayokusanywa
huwa tunapima maambukizi hayo manne, mashine zina uwezo wa kupima sampuli 100
kila moja ndani ya masaa mawili, maana yake ni kwamba mashine hizi zinatupa
majibu 400 ndani ya masaa mawili,” anabainisha.
Anaongeza “Tunazo pia mashine nyingine mbili ambazo
zimefungwa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza zenye uwezo wa kutoa majibu, 600
ndani ya saa moja.
“Kwa kusimika mashine hizi, mafanikio ni kwamba zinahitaji
rasilimali watu wachache zaidi, inatusaidia kukabili ule upungufu wa watumishu,
kwa sababu hatuwezi kuwa na watumishi wa kutosha asilimia 100.
“Kwa mashine hizi mtaalamu anaweza kukaa mtaalamu mmoja,
akaweka sampuli mashine ikaendelea kufanya kazi na tukapata majibu ya sampuli
600 kwa wakati mmoja,” anasema.
Anaongeza “Tukilinganisha na awali kabla ya kupata mashine
hizi tulitumia zile za 'semi-automated' ambazo sampuli 88 zilichukua saa tatu
hadi nne kupata jibu moja (maambukizi ya ugonjwa mmoja.
“Ililazimu wakae watalaamu wanne 'full time' kufuatilia
kila sampuli moja, kila ugonjwa mmoja,” anabainisha.
“Sasa hivi tunao uwezo wa kupima kwa ‘speed’ (kasi) mara
sita zaidi ya ile ya zamani, kazi zinaweza kufanyika ‘hand off’ yaani zile
mashine zinaweza kufanya kazi zenyewe baada ya mtaalamu kuweka sampuli na
‘ku-set’ mashine.
“Majibu ya sampuli nayo yanakuwa ya uhakika zaidi, tunaishukuru
mno Serikali kwa kuboresha eneo la maabara na upimaji, uhakika na ubora wa
huduma zetu umeimarika kwa wateja wetu wote (mchangiaji na anayechangiwa),”
anasema Dk. Magdalena.
NYOTA
NJEMA
Anasema Mpango huo hivi sasa umefanikiwa kuongeza kiwango
cha ukusanyaji damu nchini kimeongezeka kwa asilimia 20 kutoka
asilimia 40 ilivyokuwa mwaka 2015 hadi asilimia 60 mwaka 2019
“Haya ni matokeo ya kufanya kazi kwa ushirikiano, hamasa ya
jamii imekuwa kubwa, kila mtu sasa anaelewa umuhimu wa damu, tumepiga
hatua kubwa ingawa bado hatujafikia asilimia 100,” anasema.
Anasema kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani
(WHO) ili nchi itosheleze mahitaji ya damu inahitaji kukusanya
asilimia moja ya wananchi wake.
“Tanzania, tunakadiriwa kuwa tupo watu milioni 50, maana
yake tunatakiwa kukusanya chupa 50,000 za damu kila mwaka, mwaka
2016/17 tulifanikiwa kukusanya chupa 196,735, mwaka 2017/18 chupa 257,557 na
mwaka 2018/19 idadi iliongezeka hadi kufikia chupa 309,379,” anabainisha.
MTANDAO
NCHINI
Anasema NBTS ina vituo saba vya Kanda ukanda wa Kaskazini
(Kilimanjaro), Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Magharibi (Tabora), Kusini
(Mtwara), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya).
“Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Morogoro Pwani) na
Kanda ya Kati (Dodoma),” anasema Dk. Magdalena.
Anaongeza “Pia tunashirikiana kwa ukaribu na Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Kanda ya Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ).
“JWTZ wenyewe hawana mipaka ya mikoa wanayohudumia,
wanahudumia nchi nzima.
“Ili kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa ukaribu kwenye kila mkoa na wilaya kuna mratibu wa damu salama lengo ni kuhakikisha kote huko kuna mtu ambaye anahakikisha damu ipo,” anasisitiza.
Chapisha Maoni